*Mabilioni ya makusanyo yayeyuka

Wakati Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, January Makamba, alitarajiwa kukutana na wafanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) jana, viongozi wakuu wake wanatuhumiwa kufanya ufisadi unaoiangamiza kampuni hiyo ya umma.

Kila mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi analipwa Sh milioni moja kwa siku; hizo zikiwa nje ya marupurupu mengine. Wakati wajumbe wakitafuna mamilioni hayo, imebainika kuwa mamilioni ya shilingi hupotea kutoka kwenye makusanyo ya kanda, huku Dar es Salaam ikichukuliwa kama kitovu cha ufisadi huo.


Chanzo cha habari cha uhakika kutoka ndani ya TTCL kimeiambia JAMHURI kuwa kwa sasa Kampuni hiyo imekuwa “shamba la bibi” kwa kuwa viongozi wa juu wameanzisha mtandao unaotafuna fedha za umma.


“Mkoa wa Kaskazini unaongoza kwa makusanyo ya fedha. Mwaka jana ulizalisha Sh bilioni 7.9. Lengo lilikuwa kukusanya Sh bilioni 4.8 kwa mwaka, lakini cha kushangaza katika kumbukumbu za TTCL Sh bilioni tatu hazionekani katika hesabu. Katika Mkoa wa Dar es Salaam Kati hesabu Makao Makuu ya TTCL Sh bilioni 3.5 nazo hazionekani katika hesabu,” kimesema chanzo cha habari.


Ufisadi huo umewashtua wafanyakazi, kiasi cha kutoa wito kwa uongozi wa juu kumtumia Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kuichunguza kampuni hiyo.


Wafanyakazi wanahoji uhalali wa kutumiwa kwa kampuni moja ya ukaguzi wa hesabu, huku baadhi ya viongozi wa TTCL wakiwa wameshawahi kufanya kazi katika kampuni hiyo ambayo ni ya kimataifa. Taarifa za ndani ya kikao kilichofanyika katika moja ya hoteli katikati ya Jiji la Dar es Salaam zinaeleza kuwa mameneja wa mikoa wametishia kuishtaki menejimenti hiyo wizarani iwapo haitatoa hesabu sahihi za makusanyo.


Hata hivyo, kuna taarifa inadai kuwa Meneja Mishahara, Hamida Masoli, amekimbilia nje ya nchi baada ya Kitengo cha Usalama ndani ya kampuni hiyo (CIA) kubaini kuwa anamiliki akaunti yenye Sh bilioni moja.


Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na wafanyakazi hao kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, fedha hizo zinadaiwa kuchukuliwa katika kampuni hiyo.


Akijibu shutuma hizo, Mkurugenzi wa Idara wa Fedha, Shaban Mrisho, amesema kuwa tatizo katika kampuni hiyo ni uhusiano mbaya kati manejimenti na wafanyakazi.


Amesema kamapuni hiyo imejaa siasa kwa kuwa  wafanyakazi wamekuwa  wakipeleka maneno katika vyombo vya habari hata yale yasiyo na ukweli ndani yake.


Akijibu kuhusu manejimenti kula fedha za makusanyo, amesema hakuna fedha yeyote inayoliwa kwa kuwa hesabu zote ziko sawa bali wafanyakazi wanashindwa kuelewa kuwa hesabu hizo zimeunganishwa na Ongezeko la Thamani (VAT).


“Katika hesabu walizosema hawa watu wanashindwa kuelewa kuwa kuna mambo mengi pindi tunapowapangia malengo.


“Tunapopanga malengo  huwa hakuna VAT,  bajeti inakuwa nje na VAT, sasa wanapoleta hesabu zao huku lazima tulipe VAT ndio hapa sasa unaona kuwa kuna hela inazidi.


“Lakini katika hesabu hizo pia kuna makusanyo yanayotokana na mali za kampuni kama kodi za majengo nazo wanaingiza kwenye bajeti yao jambo ambalo ni kosa, huko wanatakiwa kukumbuka kuwa kodi zote za nyumba za kampuni katika maeneo yao zinaingia makao makuu.


“Tatizo siku zote linatoka katika Kanda ya Kaskazini huko ndio kwenye chokochoko, kuna watu wanajiita wanaharakati, meneja wao ndio mtu wa kwanza ambaye ameshindwa kuwasilisha bajeti lakini amekuwa wa kwanza kulalamika, jamani hatuwezi kuiba kupitia bajeti,” amesema Mrisho.

 

Akizungumzia wizi uliofanywa Masoli amekiri kuwapo kwa wizi huo lakini amekanusha kuwa si kwa kiwango kilichotajwa.


Amesema kuwa Masoli alichoiba ni fedha kidogo ambayo alikuwa  kwa ajili ya kununua mafuta, hata hivyo alishindwa kutaja ni kiwango gani alichoiba.


“Jamani huyu mama mie sijui kama amekimbia nchini lakini kiasi kinachotajwa ni kikubwa mno kwani amekuwa akichukua kidogo kidogo tangu mwaka 2007 ni hela ya mafuta tu au labda kama baba, mjomba au bibi walikuwa  wanaumwa anachomoa kidogo hadi kimefika kiasi hicho,” amesema.

By Jamhuri