*Unahusu kada wa CCM anayechimba urani

*Profesa Tibaijuka amtwika mzigo Jaji Werema

*Naibu Spika aagiza Waziri Muhongo ajiandae

*Sinema nzima imeibuliwa na Halima Mdee

 

Wafanyabiashara ndugu wanaodaiwa kubadili matumizi ya ardhi kutoka uwindaji wa kitalii na kuanza harakati za uchimbaji madini ya urani, wameibua mgongano mkubwa bungeni na serikalini. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amemwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, asaidie kupata utatuzi kashfa hiyo.

Hoja hiyo iliibuliwa bungeni wiki iliyopita na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema). Wabunge wengi waliozungumza na JAMHURI wameonyesha kushitushwa na taarifa hizo, huku wakihoji uadilifu wa watendaji serikalini na dhima ya Usalama wa Taifa, hasa kwa masuala hatari kama hili linalohusisha uchimbaji wa madini ya urani.

Wafanyabiashara ndugu, Mohsin M. Abdallah na Nargis M. Abdallah ni makada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mohsin ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii (TAHOA). Chama hicho kimekuwa karibu mno na viongozi waandamizi ndani ya CCM na serikalini, huku wanachama wake wakiwa wanahodhi maeneo mengi na manono ya uwindaji wa kitalii.

Katika hoja yake, Mdee alisema; “Kwa muda mrefu sasa ardhi ya Tanzania imegeuzwa ‘shamba la bibi’ na kikundi cha mafisadi! Kambi ya Upinzani imeshuhudia mkataba ulioingiwa baina ya kampuni za Uranium Resources PLC, Western Metals Limited na Game Frontiers of Tanzania Limited, mkataba ambao umetengenezwa na Kampuni ya Kitanzania ya Rex Attorneys, na ulisainiwa Machi 23, 2007.

“Mkataba husika, ambao vipengele vyake vinaainisha kwamba unatakiwa uwe wa SIRI unaihusu kampuni ya uwindaji inayofahamika kwa jina la Game Frontiers of Tanzania Limited inayomilikiwa na Mohsin M. Abdallah na ndugu Nargis M. Abdallah.”

Kampuni hiyo ya uwindaji imeingia mkataba na kampuni mbili za kigeni kufanya utafiti wa uchimbaji wa madini ya uranium katika Kijiji cha Mbarang’andu kwa malipo yafuatayo:-

Mosi, malipo ya dola 6,000,000 za Marekani ambazo zitalipwa kwa awamu mbili ya malipo ya dola 3,000,000. Malipo ya kwanza yatafanyika pale uzalishaji wa urani utakapoanza. Pili, malipo ya dola 250,000 za Marekani baada ya kampuni za madini kukamilisha utafiti wa madini ya urani na kupata kibali cha uchimbaji wa madini hayo.

 

Tatu, malipo ya dola 55,000 za Marekani kila mwaka kama fidia ya kushindwa kufanya biashara na usumbufu unaotokana na shughuli za machimbo kwenye kitalu! Malipo hayo yatafanyika kila Machi 31.

 

Nne, wenye mali hiyo, yaani wanavijiji wanaambulia malipo ya dola 10,000 kwa vijiji vitakavyoathiriwa na utafiti huo wa urani, malipo ambayo yametokana na makubaliano baina ya kampuni ya uwindaji na kampuni za madini.

 

“Mheshimiwa Spika, nimepitia sheria za uhifadhi wa wanyamapori, The Wildlife Conservation Act, 1974 (sheria ya zamani) na Sheria mpya ‘The Wildlife Conservation Act, No. 5 of 2009. Sheria hizi zinamruhusu mtu aliye na leseni ya uwindaji, kuwinda wanyamapori tu.

 

“Hali kadhalika, Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, Sheria namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sheria namba 5 ya mwaka 1999 inatamka bayana kwamba ardhi inajumuisha vitu vyote vilivyo juu ya ardhi na chini ya ardhi isipokuwa madini au mafuta…

 

Na kwa mujibu wa sheria za Tanzania, linapokuja suala la madini, umiliki unatoka kwa mtu binafsi na kurudi serikalini. Na ni Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ndiyo pekee yenye mamlaka ya kutoa leseni ya kutafuta madini kwa kampuni za madini.

 

“Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge lako tukufu uhalali wa mkataba kati ya Game Frontiers na Uranium Resources PLC na Western Metals. Ni sheria ipi inayoipa kampuni ya uwindaji haki ya kualika kampuni ya nje kwenye eneo ambalo haina umiliki kufanya utafiti na hatimaye kuchimba madini hatari kama urani?

 

“Ni Serikali ya aina gani yenye uwakilishi mpaka ngazi ya kitongoji na Usalama wa Taifa mpaka ngazi za chini kabisa za utawala, inashindwa kuyaona haya?” Amehoji Mdee.

 

“Nini mustakabali wa Watanzania wanaoishi kwenye vijiji vinavyozunguka mbuga hiyo, ambao wanaishi maisha yao ya kila siku pasipo kujua kama kuna utafiti wa madini hatari ya urani unaoendeshwa kwa siri kubwa?

 

“Kama mtu ana leseni ya kuwinda katika ‘land surface’, akaingia mkataba na mtu wa kuchimba, suala hilo linabadilika,” amesema.

Kwa upande wake, Profesa Tibaijuka akijibu hoja za wabunge wakati wa kupitisha bajeti ya wizara yake, alisema wazi kuwa ni makosa kwa mtu mwenye leseni ya uwindaji kuitumia kufanya utafiti au kuchimba madini.

Akaliambia Bunge kwamba atarejea kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili aweze kutoa mwongozo wa kisheria.

“Sheria ya madini inasema bayana kuwa huwezi  kuanza kuchimba madini kabla hujafidia wale wenye surface right. Wanyama wako juu ya ardhi, hawako chini ya ardhi. Anatakiwa yeye afidiwe, aachie wale wanaochimba. Sasa kama utaratibu huo umekiukwa, sheria ya madini, kifungu cha saba, tunalipeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” amesema.

 

Unyeti wa suala hilo ulimfanya Naibu Spika Job Ndugai, atoe maelezo. “Kwa sababu bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini itakuja, wajiandae vizuri ili waje watoe ufafanuzi wa jambo hili kwa sababu wengi wetu hatujui limekaakaaje,” amesema.

 

Watumishi wa Serikali ndiyo wasaliti wakuu

Wawindaji wengi wamekuwa wakiendesha vitendo vya hujuma, lakini licha ya hujuma hizo kuanikwa, watendaji wa Serikali wamekuwa wakiwabeba. Tukio la karibuni ni la wawindaji wa kitalii kuikosesha serikali mapato.

 

Gazeti moja hivi karibuni limeandika kuwa ukwepaji kodi wa kutisha umebaika kuwapo kwenye tasnia ya uwindaji wa kitalii kupitia kwa wawindaji bingwa, yaani Professional Hunters (PH). Ukwepaji kodi huo unajulikana kwenye Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini umefumbiwa macho.

 

Taarifa zinaonyesha kuwa PH ambao ni raia wa kigeni, kwa sasa wanaendelea kuwinda katika mapori mbalimbali nchini ambako kila mmoja ana kibali cha kuwinda cha kampuni moja, lakini wanawinda katika kampuni nyingi tofauti.

 

Kwa kawaida, PH mgeni hutakiwa apate kibali cha kuwinda kupitia Idara ya Uhamiaji na anatakiwa kisheria kuwinda katika kampuni moja.  Anapotaka kwenda kuwinda katika kampuni nyingine tofauti na ile aliyoombea kibali, hupaswa apeleke maombi na kisha alipe ada ambayo ni ya mamilioni ya shilingi.

 

Baadhi ya kampuni ambazo zina vitalu vingi, ambazo ni wanachama wa TAHOA, ndizo zinazoongoza katika suala hili ambalo viongozi wa Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii wameendelea kulinyamazia.

 

Baadhi ya wanachama wa TAHOA wana kampuni zaidi ya nne walizosajili kwa majina tofauti, na hivyo wamejikuta wakitumia fedha nyingi katika ada za ma-PH. Baada ya kuona fedha nyingi zinalipa vibali vya PH vya Uhamiaji na Wizara, wameamua kuwafanya ma-PH hao kutumia kibali kimoja kufanya shughuli za uwindaji katika kampuni zaidi ya moja.

 

“Kwa kawaida kisheria inatakiwa PH apate vibali vya kuwinda katika kampuni moja, anapotaka kwenda kampuni nyingine kuwinda ni lazima alipie kibali kipya. Sasa hilo wanalikwepa. Tunavyozungumza kuna PH wamepata kibali cha kuwinda katika kampuni moja, lakini wengine sasa wameshafikisha kampuni nne kwa kibali hicho hicho kimoja,” kimesema chanzo chetu cha habari.

 

Ujanja huo umewezesha Serikali kukosa mapato ya mamilioni ya shilingi. Aidha, utaratibu huo ni kinyume kabisa na Sheria za Idara ya Uhamiaji na Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 kifungu 49 (1), (2), (3) & (4). Kisheria, Idara ya Uhamiaji nayo hairuhusu kibali kimoja kitumike kampuni nyingine.

 

Uchunguzi umebaini kuwa mwaka jana wenye kampuni walifaidi kwa namna fulani mbinu hiyo, lakini baadaye ikasitishwa. Lakini sasa imerejea kwa kasi.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Paul Sarakikya, anatuhumiwa kubariki suala hilo.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

936 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!