Sehemu ya kwanza ya makala hii, mwandishi alieleza namna Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alivyowazuia wafuasi wa TANU kuandamana wakati wakoloni walipomfungulia kesi ya uchochezi mwaka 1958. Kwa ufupi mwandishi anapinga njia ya maandamano inayotumiwa na wanasiasa kufikia malengo yao, akiiona kuwa ni ya hatari. Endelea…..

Waheshimiwa wabunge wote mimi naona ni wasomi na kwa hiyo wanajua wanachofanya. Swali langu ni kwa haya wanayoyafanya. Je, wanayafanya kwa faida ya nani? Moyo wa maridhiano ulioanza kuonekana wakati wa Bunge Maalum la Katiba (BMK) linaanza ulipaswa kuendelezwa kwa faida ya Taifa letu.

Maridhiano na siyo mapambano ndio msingi wa amani duniani. Katika mapambano kunatumika dhana ya mabavu, kutunishiana msuli ili kuona nani ni mshindi. Tabia hiyo haina tija kwa wapambanao au wafuasi wao, bali sana sana huzaa uhasama katika jamii. Uhasama kati ya vyama vya siasa – kunaweza kusambaratisha Taifa zima kwa kukosekana utulivu na amani.

Maridhiano ni moja ya kanuni za maisha katika ulimwengu (one of the natural laws). Sisi tuliosoma sayansi somo, lile la fizikia tunaelewa vizuri sana ile kanuni ya ‘JOTO’ kwa Kiingereza Heat Equation.Ni kanuni fupi isemayo HEAT LOST BY A HOT SUBSTANCE IS EQUAL TO HEAT GAINED BY A COLD SUBSTANCE). Kanuni hii ya maridhiano inasema: “UNACHOTOA kiasi hicho hicho ndicho UTAKACHOPOKEA”. Ni sawa kabisa. Falsafa yote ya maridhiano inategemea kutoa na kupokea. Waingereza wanaita ‘The Principle of GIVE and TAKE’. Hii ni tofauti kabisa na neno la Kiingereza linalosema compromise – huku ni kuafikiana na wala siyo kuridhiana.

CHADEMA kuna wakati walionesha ujasiri na utayari wa kuridhiana na vyama vingine vya upinzani. Kama tunakumbuka vizuri baada ya Uchaguzi ule wa mwaka 2010, CHADEMA hawakuwa na moyo wala fikra ya kushirikiana na vyama vingine vya upinzani katika Bunge.

Lakini pole pole walipata ung’amuzi na uhalisia wa hitaji la kuunganishwa nguvu kubwa za upinzani wa pamoja ili kuwa na uwezo au nguvu kubwa za upinzani kushinikiza mabadiliko ndani ya Bunge na hata nje ya Bunge katika Serikali kwa ujumla.

Ilipotokea nafasi (when an opportunity arose) katika BMK, CHADEMA wakawa mstari wa mbele kutaka maridhiano na vyama vya CUF (Chama cha Wananchi) na NCCR – Mageuzi, National League for Democracy (NLD) na Democratic Party (DP) na wakaunda kitu- UKAWA. Kila chama kilikuwa wazi tayari KUTOA ili kipokee kitu katika ushirikiano huo. Maridhiano namna hiyo yanafaa. Sasa yaendelezwe kwa vyama vyote vya siasa.

Lile wazo la wenyeviti wa vyama vya siasa kukutana na Rais ambaye ndiye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mazungumzo ni hatua nzuri sana kuwafanya wabadilishane mawazo kama wenyeviti na viongozi wa siasa katika nchi. Lakini wazo hili jipya la mapambano mimi linanitisha, na wala siliafiki.

Maana yake wanaopambana siyo wanasiasa bali ni ITIKADI NA DOLA- hapo siyo sahihi. Siasa wana silaha ya itikadi – ya kudai haki za kibinadamu zinazoonekana kunyimwa wahusika kumbe dola wana silaha za moto za mapambano kusimamia sheria zilizotungwa na siasa bungeni na kulinda maslahi ya raia wote.

Basi kule kwetu Songea, Wangoni wanasema kwa mtu yule asiye na mabavu anayeng’ang’ania kupambana na mwenye mabavu – anaitwa ‘mfwiliku’ yaani mfia haki na yuko tayari kufia hilo analoligombea hadi alipate. Tabia hiyo ndiyo inaitwa kilugha UFWILIKU. Sikuweza kabisa kupata neno la Kiswahili kwa neno hilo.

Wazee wengine tunakumbuka msamiati wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alioutoa katika ukumbi wa Kizota, Dodoma katika mkutano wa CCM mwaka 1987 alipotumia neno la Kizanaki ‘KUNG’ATUKA’ kuonesha hali ya wazee kustaafu au kupumzika ili kuwapisha vijana mahali pao. Sasa neno hili ‘kung’atuka’ limezoeleka katika msamiati wa Kiswahili serikalini. Mtu akitimiza umri wa miaka 60 anang’atuka. Alishindwa kupata neno sahihi kumaanisha hali ya kupumzika kwa uzee, na mimi hapa nimeshindwa kupata neno sahihi kuonesha ung’ang’anizi katika kudai haki.

Neno ‘ufwiliku’ linaonekana vizuri kwa mfano huu. Pale mwaka 2010 nakumbuka kulikuwa na baadhi ya viongozi wa chama fulani cha upinzani walioamua kuandamana kupeleka ujumbe wao ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) pale Matsalamat Building (zilipo ofisi za sasa za gazeti hili). Serikali iliwakataza wasiandamane, maana hawakuwa na kibali cha Polisi. Wao, kwa vile kiongozi wa mbele kabisa katika maandamano yale alitokea kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) mstaafu, basi wakavunja sheria. Walipofika pale Matsalamat Building, ofisi za UN, waliombwa na polisi watawanyike. Hawakufanya vile. Ndipo polisi kwa kutumia sheria zilizopo waliwatawanya kwa nguvu (walipigwa maji ya washawasha). Nakumbuka kabisa kiongozi wa maandamano yale alikuwa hoi. Ni mzee wa heshima aliwahi kuwa kada wa CCM, Mwalimu wa Siasa katika Jeshi la Polisi, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya na hatimaye RPC mkoa fulani. Tangu hapo ‘ufwiliku’ ulimshinda, hata chama chenyewe sijui kama bado anashiriki vikao – alikiona kilichomtoa kanga manyoya na wala hataki tena upuuzi ule wa kuandamana kinyume cha sheria.

Ndipo nami najiuliza ni kweli kuna mantiki kwa uongozi wa upinzani kuendeleza hiyo tabia ya huo ‘ufwiliku’? Mbona siasa na dola nguvu zao siyo sawa? Ni kweli Tanzania tumeshindwa kufuata hekima na busara za Baba wa Taifa alipotahadharisha wafuasi wake wasiandae mazingira ya uchokozi, ili dola isipate kisingizio cha kutumia mabavu kutuweka sawa?

Mimi ni mwamini wa maridhiano, wala siyo mapambano. Napenda njia sahihi ya kulinda amani na utulivu wetu hapa nchini. ‘Ufwiliku’ siyo njia sahihi hata kidogo.  Laiti wangefuata busara za Mwalimu kuwa kususa ni kuwapa nafasi vyama vingine kupata matakwa yao kupitia Bunge, wapinzani wasingesusia vikao hivi vya BMK.  Michango yao ingekuwa na ‘impact’ kubwa sana katika kupata Katiba mpya wala yaliyofanyika hivi sasa yasingewezaka.

Maadam, sheria za nchi zinatungwa bungeni, basi kuzipinga kwa ubabe siyo njia sahihi kwa upinzani. Wabadilike ki-approach. Iddi Amin alitamka pale Uwanja wa Ndege Nakasongola – “I withdrew tactfully” kumbe alikimbia mapigo ya Watanzania. Upinzani yafaa watafute njia mbadala kuepuka aibu ya kushindwa.

Upinzani wanajua kuwa ipo Sheria Na. 254 waliyoshiriki kuitunga bungeni, hivyo kudai mapesa mengi yanateketea katika kuliendesha BMK ni geresha tu kwa wananchi. Je, kutoa tangazo la tishio la migomo na maandamano nchi nzima hakuna athari kifedha? Jeshi la Polisi litatumia fedha kujiandaa utayari (alertness/standbye) kulinda usalama wa wananchi. Hapo fedha kiasi gani kinateketea kwa kauli hatarishi hizi?

Sote tukifuata sheria za nchi kutakuwa na amani, fedha za walipakodi zitasalimika. Fedha zilizoteketea bungeni zimekubaliwa na Bunge kwenye bajeti, lakini hizi za ulinzi wa dharura kwa Polisi nchi nzima kuzuia maandamano batili na yasiyokuwa na tija ni hasara kubwa sana kwa uchumi wa Taifa hili. Wanasiasa mnalionaje hilo? Elimu ya uchumi ya kawaida tu inahitajika kuliona hili.

Ama kweli, mzungu mkoloni mmoja huko nyuma aliwahi kuniambia Francis, common sense is not common among people who are mayopic in thinking” kwa tafsiri yangu, nilikumbushwa kuwa fikra za kawaida hazionekani kama jambo la kawaida miongoni mwa wale wenye mitazamo finyu duniani. Ndiyo hivyo tena. Tunalalamikia fedha zilizoidhinishwa na wabunge wenyewe, lakini fedha hizi za matokeo ya dharura walizozisababisha hao hao wabunge hawazihesabii. Je, sawa hiyo wananchi?

Vyama vyote vya siasa wawaandae wafuasi wao kisaikolojia kuelewa wazi kuwa AMANI na UTULIVU tulionao ni zao la busara za Baba wa Taifa. Huyu daima amehimiza utulivu na mshikamano. Kamwe hajawahi kuonesha wazo la kuvunja sheria za nchi wala kuandaa mazingira ambamo vyombo vya usalama vitalazimika kutumia nguvu au mabavu kukomesha vurugu. Tuachane na tabia ya ‘UFWILIKU’ hiyo! Kule India, hayati Mahatma Gandhi alitumia sana njia hii ya ‘passive resistance’ wakati anapigania Uhuru wa India; na akafanikiwa.

Mimi huwa ninafikiri makala zangu ni sehemu ya uraia kwa wasomaji. Kule kukumbusha historia ya tulikotoka na sasa tuko wapi nadhani kunasaidia kuamsha mawazo ya baadhi ya wasomaji. Aidha, ninapoandika mawazo yangu wazi wazi natumia ile haki yangu ya kikatiba ya nchi yetu ya mwaka 1977 toleo la 2005, SURA I, sehemu ile ya III ibara ndogo ya 18(a).

Nafurahi kusema huwa napokea ujumbe mwingi wa simu ya kiganja (SMS). Upo ujumbe wa kunikosoa, kunipongeza, kubeza kuwa nimepitwa na wakati au ni kibaraka wa CCM, na kadhalika. Moja ya ujumbe niliopokea unasomeka hivi, “Mzee wangu retired Brig. Gen. nasoma makala yako katika gazeti la JAMHURI. Mzee wangu mbona unaangalia upande mmoja wa shekeli? Nikifuatisha maneno yako ‘sisimizi au kapi’ tafsiri ya muono wako ina maana tuna Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni TUMBILI? Pili, nadhani walichochoka nao ni kupokea watu walioharibiwa na mfumo uliopo, ni kazi kubwa sana kuwabadili. Mfano, nadhani husikii tena kelele nyingi toka kwa mwakilishi wa Maswa. Tatu, nani asiyependa pesa za wafadhili? Hivi nchi ya Japan au za Scandinavia wakisusa itakuwaje? Mimi ningekuomba kilichopo sasa hewani ni RASIMU YA KATIBA. Kama unaye ndugu yako unampenda katika BMK ajitoe lakini tu kama ni mbobevu katika taaluma yoyote ile na anapenda kulinda hadhi na heshima yake katika jamii ajitoe kabla hajachelewa. Samahani kwa msg ya usiku ndiyo muda wangu, kusoma magazeti, usiku mwema”.

Imetoka simu na. 0714 197178;p Agosti 06, 2014. Muda 22:10:37.

By Jamhuri