Moja ya hotuba za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere zinazowakuna Watanzania ni ile ya Dhambi ya Ubaguzi. Mwalimu Nyerere aliwaonya Watanzania kuepuka dhambi ya ubuguzi. Alituasa Watanzania kuwa ubaguzi ni sawa na kula nyama ya mtu, ukiishaanza hauachi. Mwalimu aliwaonya Watanzania kujiepusha na dhambi hii.

Alitwambia kuwa tutafanya kosa kubwa mno iwapo siku moja tutaamka tukavunja Muungano. Akatumia maneno haya: “Kwa sababu ya ulevi tu, ulevi wa madaraka, mkaamua kuvunja Muungano. Kwa kusema ninyi ni Wazanzibari na wao ni Watanganyika,” akasita kidogo, na kuongeza: “Hamtabaki salama.”

Sitanii, Mwalimu alifanya utabiri ambao leo naushuhudia unatokea Uingereza kwa kusema: “Mkiishamaliza kujitenga mkidhani kwamba ninyi ni Wazanzibari, mtakuta kuna Wazanzibari na Wazanzibara. Hamtabaki salama.”

Katika hotuba hiyo akasema mara Wazanzibari ukiacha Uzanzibari na Uzanzibara watakuta kuna Wapemba na Waunguja. Kwa Tanganyika, akasema kwa Watanganyika watajikuta kuna Wahaya, Wachaga, Wamakonde na wengine wengi kila mtu atataka kuwa na taifa lake na huo ndiyo utakuwa mwanzo wa kugawanyika kwa kiwango cha kutisha.

Maneno haya ya Mwalimu Nyerere tumeyashuhduia mwezi uliopita Uingereza ilipoamua kujitoa kwenye Muungano wa Ulaya. Uingereza imekuwa mwanachama wa Muungano wa Ulaya kwa miaka 43, umri ambao ni wa mtu mzima.

Ghafla wakaibuka watu wanaojiita wazawa, akina Boris Johnson. Huyu Johnson akaanzisha kampeni ya kutaka Uingereza ijitoe kwenye EU. Waziri Mkuu wake, anayetoka naye chama kimoja, David Cameron yeye akaendesha kampeni ya Uingereza kubaki. Kambi ya Johnson hatimaye imeshinda kwa kupata asilimia 52 ya kura dhidi ya asilimia 48 ya wale waliotaka wabaki kwenye EU.

Kabla sijaendelea, niseme kidogo hapa. Nimevutiwa na aina ya demokrasia ilivyokomaa nchini Uingereza. Demokrasia imekomaa kwa kiwango ambacho Waziri Mkuu, ambaye anaongoza taifa hilo anaweza kupigwa na watu wa ndani ya chama chake na asiwepo hata mtu mmoja anayepata tatizo.

Sina uhakika sana hapa kwetu kama mtu anaweza kupingana na mwenyekiti wake na akabaki salama. Nigusie mifano kidogo. Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alipotofautiana kimtazamo na Waziri Mkuu wake, Edward Lowassa tunajua kilichotokea.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipotofautiana na Zitto Kabwe aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, tunajua yaliyomfika. Mwenyekiti wa UDP a.k.a Mzee wa Out/Mapesa, John Cheyo alipotofautiana na akina Danih Makanga, tunajua yaliyowafika.

Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema alipotofautiana na akina Leo Rwekamwa akiwa Katibu Mkuu wake, tunajua kilichotokea. Mrema huyo huyo, alipotofautiana na akina Mabere Marando akiwa NCCR Mageuzi tunajua yaliyotokea. Labda niseme, Rais John Magufuli akiwa Mwenyekiti wa CCM pekee ndiye atakuwa na uvumilivu sawa na aliouonyesha Cameron kwa watu wenye mawazo tofauti na yeye ndani ya chama!

Sitanii, Cameron baada ya kushindwa kura ya maoni, ameonyesha hatua ya pili ya kukomaa kwa demokrasia. Kwanza ikumbukwe alikuwa na anaendelea kuwa Waziri Mkuu kwa sasa. Cameron kwa nchi nyingi za Afrika angeweza kukamata watu wote wanaojumulisha matokeo kabla ya Tume kutangaza ‘matokeo rasmi.”

Sisi wengine tumefahamu mapema alfajiri kupitia BBC kuwa kambi ya Cameron imeshindwa kura ya maoni. Hakuzuia watu kujumulisha matokeo. Si hilo tu, baada ya kuona kuwa ameshindwa kura ya maoni akatangaza kung’atuka uwaziri mkuu ndani ya miezi mitatu kwa maelezo kuwa anahitajika mtu mwingine mwenye uwezo wa kutetea dhana ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Kujiuzulu kwa Cameron ni hakikisho jingine la kukomaa kwa demokrasia katika nchi ya Uingereza. Kwa Afrika viongozi wetu walio wengi wanasema kwa kawaida nzi hufika kwenye kidonda. Matokeo kama hayo yangetangazwa chini ya mtutu wa bunduki. Sikusikia bomu la machozi hata moja likipigwa Uingereza au Tume ya Uchaguzi kuwekewa ulinzi wa ziada iweze kutangaza matokeo hayo, yanayompa ushindi mpinzani wa Cameron. Yatupasa kuinga mazuri.

Ukiacha upande huo wa shilingi, nirejee kwenye hoja ya msingi. Wale waliotetea kujitoa kwa Uingereza kwenye EU wanasema kazi za Waingereza, heshima ya Uingereza na mamlaka ya kufanya biashara na nchi waitakayo kama Waingereza yamepokwa na EU. Kimsingi, ni hali fulani ya kiburi ya kuhoji kwa nini watuamulie wengine na si sisi tujiamulie.

Sitanii, kundi hili linataka kujifungia ndani. Ndilo linaloita watu wengine wahamiaji haramu. Lilikuwa sharti kuu ya Uingereza kubaki kwenye Umoja wa Ulaya, wakisema wananchi wa Ulaya wakiwamo Wapoland waingie Uingereza kwa visa. Umoja wa Ulaya unalikataa hilo.

Ni kwa msingi huo wamevutia wapigakura wengi bila wengine kujua kwa nini wanapiga kura na wakajikuta wanajiondoa kwenye EU. Yaliyotokea baada ya nia yao ya kujiondoa EU ndiyo fundisho kubwa. Paundi sarafu ya Uingereza iliyokuwa na nguvu kwa miaka mingi, imepoteza thamani kwa kiwango ambacho hakijapata kutokea katika miaka 35 iliyopita.

Masoko ya fedha yameshuka na kupoteza mtaji kwa wastani wa dola trilioni 2. Nazungumzia dola si shilingi. Nchi wanachama wa EU 27 waliosalia, wamewambia Waingereza waondoke haraka. Wanawataka sasa kutoa taarifa ya kimaandishi chini ya kifungu cha 50 cha Mkataba wa EU kuwajulisha wenzao nia yao ya kujitoa.

Sitanii, huko nyumbani Uingereza hali si shwari tena. Raia zaidi ya 100,000 wamejiandikisha kupinga nchi yao kujiondoa EU kwa sababu za wazi. Sababu wanazozitaja ni pamoja na kupoteza masoko (soko la pamoja), watoto wao kukosa fursa ya kusafiri kwa uhuru katika nchi 27 wanachama wa EU, kujijengea chuki na mataifa mengie hivyo kuzaa ubaguzi. Bunge sasa linasubiriwa lipitishe au liikatae kura hiyo ya maoni.

Si hilo tu, mparaganyiko mkubwa umeanza. Uchumi wa Uingereza umeanza kusinyaa. Wametangaza nia ya kuokoa uchumi wao kwa kuongeza paundi milioni 250 kutoka Benki Kuu yao. Mtu aliyeongoza kampeni ya kujitoa EU, Brexit, Boris Johnson aliyetarajiwa kuwa angechukua mikoba ya Cameron kwani aliijua njia aliyowashawishi Waingereza kuifuata, sasa ametangaza kuwa yeye hataki kuwa Waziri Mkuu.

Wandani wake wanasema hakujua maana ya Uingereza kujitoa EU na baada ya kuona masoko yanavyoshuka, paundi ya Uingereza inavyopoteza thamani, akaona nchi itampasukia mikononi. Ameogopa, amebwaga manyanga. Hagombei Uwaziri Mkuu.

Sitanii, maajabu hayaishi duniani. Theresa May, Waziri wa sasa wa Mambo ya Ndani wa Uingereza aliyekuwa anapiga kampeni ya kubaki, sasa amegeuka jiwe la chumvi. Mwana mama huyu kwa kuwa anaona upepo wa kisiasa unavuma kuelekea kwake, sasa anasema yeye anaweza kusimamia Uingereza kujitoa EU na anaomba ateuliwe kuwa Waziri Mkuu.

Maneno ya Mwalimu Nyerere kabla wino haujakauka, Uingereza inayathibitisha. Uingereza inaundwa na nchi nne. England, Scotland, Wales na Northern Ireland. Mwaka 2014 Scotland ilitaka kujitoa Uingereza, ikabakizwa kwa hoja moja tu kuwa Uingereza haitajitoa EU.

Hata kura ya maoni iliyopigwa mwezi uliopita, Scotland katika majimbo yote 32 imepiga kura ya kubaki EU. England nayo imepiga kura ya kubaki EU kwa asilimia kubwa. Wales ndiyo iliyopiga kura ya kujiondoa EU kwa kishindo. Scotland sasa inasema mazingira yamebadilika na sababu zilizoifanya isalie katika Muungano wa Uingereza hazipo tena, hivyo inaangalia uwezekano wa kuitisha kura ya kujitoa katika Muungano wa Uingereza.

Uingereza wamejitoa EU wakidhani kuwa watakabi salama, wao ni Waingereza sasa walipofika Uingereza wakakuta kuna Walodoner, Wascotish, Wawelish na Wairish. Sasa wanagawana mbao. Maneno ya Mwalimu Nyerere yanatimia. Uingereza inapasuka vipande.

Yapo mambo ninayoyaona na kujifunza katika hili. Moja, naamini Wamarekani hawatafanya kosa kumchagua Donald Trump aliyewapongeza Waingereza kwa kujiondoa EU akisema wamepata uhuru wa kweli. Pili, kwa idadi ya wapigakura waliojitokeza na kura walizopata mwezi uliopita, matokeo hayo yanaweza kupinduliwa.

Katiba ya Uingereza inataka wapigakura wajitokeze asilimia 75 ya wapigakura wote waliojiandikisha. Katika hili walijitokeza asilimia 72. Inataka asilimia 60 ya wapigakura kati ya hiyo asilimia 75 au zaidi wapige kura kuunga mkono uamuzi kama huo wa kujitoa, wamepata asilimia 52.

Vigezo hivi pekee huenda vitalifanya Bunge la Uingereza ama kuitisha kura ya pili ya maoni, ambayo nina uhakika ikiitishwa matokeo yatapinduliwa, kwani hata waliopiga kujitoa tayari wanajuta au watatumia mamlaka ya Bunge kuuweka kando uamuzi huo.

Ikiwa uamuzi huo utawekwa kando, namuona David Cameron akiendelea kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, ila hiki kinachoendelea Uingereza kinapaswa kuwa somo kubwa kwetu tuliopo katika Muungano wa Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Mshindo huu, ni wazi kuwa hata Trump Wamarekani watajifunza kwa Uingereza alichowafanya Johnson hivyo hawatamchagua.

Sitanii, mara nyingi sikubaliani na aina ya uchaguzi ulivyoendeshwa Zanzibar, ila nikisikiliza hoja za akina Maalim Seif Sharif Hamad za kujiondoa kwenye Muungano, nikaangalia alichokifanya Boris Johnson kwa Waingereza, japo siungi mkono, ila nashawishika kwa masilahi mapana ya nchi “kufunika kombe mwanaharamu apite.” Tumejifunza nini kwa Uingereza? Nijibu.

1566 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!