Ninachokipenda sana katika ujasiriamali (katika mifumo rasmi), ni ile hali ya mtu kuwa na uwezo wa kutengeneza kipato kikubwa pasipo kufanya kazi zaidi na zaidi.

Ukiajiriwa unalazimika kuitumikia fedha (utalazimika kuendelea kuuza muda wako kwa malipo ya mshahara), lakini ujasiriamali unatoa fursa ya fedha kukutumikia wewe.


Ukijipanga vizuri kijasiriamali unaweza kufika katika hatua ambayo hutahitaji kufanya kazi tena ili kupata fedha. Fedha inakuwa ikijizalisha.


Hivyo basi, utagundua kuwa suala la kusoma ama kusomesha huku kukiwa na mawazo ya kuajiriwa ni sawa na kujiandalia utumwa.


Hali iliyopo sasa haimtambui mtu aliyeshikilia vyeti vyenye maksi nyingi, ila mazingira yatambeba yule tu mwenye uwezo wa kupambana na kutatua changamoto za maisha zinazomzunguka (bila kujali elimu yake).


Tanzania ya leo lazima tuanze kujiokoa na kuokoa kizazi kijacho, tujenge mazoea ya kutengeneza ajira badala ya kulalamika kila kukicha kuhusu ukosefu wa ajira.


Kama nilivyosema awali, ujasiriamali ndiyo eneo pekee linaloweza kutoa mamilioni ya ajira pamoja na kuwapa watu wengi uhuru wa kweli wa kiuchumi na kifedha.


Kwa nini kuwepo na fikra hasi kuona kuwa ujasiriamali si ajira kamili wakati ujasiriamali ndiyo unaoweza kuwapa watu uhuru wa kweli wa kiuchumi na kimaisha?


Dhana ya ujasiriamali kuchukuliwa ‘poa’ kumechangiwa na mwenendo na utamaduni wa makundi kadhaa katika jamii nyingi. Kundi mojawapo ni la baadhi ya wafanyakazi wa kuajiriwa ambao wamekuwa na vimiradi vidogo vidogo vya ujasiriamali. Lengo lao kubwa huwa ni kupata faida fulani ambayo itasaidia kukabiliana na kutotosheleza kwa mishahara yao.

 

Kwao hawa ujasiriamali si kazi inayoweza kusimama peke yake na kumpa mtu uhuru wa kiuchumi na kimaisha.

 

Kundi hilo lina madhara makubwa kwa taifa kwa sasa na wakati ujao. Hebu chukulia watoto wa mfanyakazi ambaye anaendesha vijimradi vya kijasiriamali ama kwa kuajiri watu ama baada ya kutoka kazini kwake ili kukabiliana na mshahara usiotosheleza.


Picha inayojengeka katika fikra za watoto wake ni kuona ujasiriamali ni harakati za ‘kuganga njaa’.


Watoto hawa wanapokua, moja kwa moja hawatakuwa na imani na ujasiriamali hata kidogo.

Lakini ninaomba kuwatambua wafanyakazi ambao hufanya ujasiriamali wakiwa ‘serious’.


Kwa kawaida hawa huwa na malengo ya kufikisha mtaji ama hatua fulani kabla ya kuachana na ajira na baadaye kuwa mabosi katika shughuli zao wenyewe.


Hata inapotokea wameendelea kufanya kazi (walikoajiriwa) ni kwa sababu wanapenda na kufurahia kufanya kazi hizo na si kwa ajili ya uhitaji wa fedha.


Wengine wanaopanda mbegu hasi za ujasiriamali kutoaminika ni wajasiriamali ambao licha ya kwamba wanafanya biashara na ujasiriamali kwa mafanikio makubwa lakini wanashawishi familia, watoto na jamii zao kuamini kuwa ujasiriamali na biashara si kazi za kufanya.

Hawa utawasikia wakiwaambia watoto wao kauli kama hizi:


“Usiangalie mali za mimi baba yako, urithi pekee ninaokupa wewe ni kukusomesha ili uje uwe na kazi yako”.


Kauli hii kwa haraka haraka inaonekana ni yenye busara kubwa lakini kutokana na mabadiliko yanayotokea sasa duniani, hii ni imani ya kufisha. Siku huyu mtoto akikosa ajira, utamkuta ameshika bango na anaandamana barabarani kudai ajira (sijui nani atakuwa akidaiwa hiyo ajira)!

 

Kwa upande mwingine, wajasiriamali wenyewe kuna kauli ambazo huwa tunazitumia ambazo zinatuondolea heshima mbele ya fikra za jamii na kutujazia hisia hasi. Hebu fuatilia tofauti ya mfanyakazi wa kuajiriwa na mjasiriamali kauli wanazotoa kabla ya kuondoka asubuhi kuelekea kazini.


Mfanyakazi ambaye huenda analipwa mshahara wa chini ya laki tano kwa mwezi anaaga kwa kusema, “Ninaenda kazini, tutaonana jioni”.


Lakini mjasiriamali ambaye ana uhakika wa kuzalisha wastani wa faida ya shilingi milioni mbili kwa mwezi anaaga kwa kusema hivi; “Ninaelekea kuhangaika, ninaenda kuchakarika, tutaonana jioni!”


Kabla hujaingia katika kufanya biashara zako tayari umeutangazia ubongo wako kuwa kuna mahangaiko siku hiyo! Ndiyo maana si ajabu kuona kuwa wafanyabiashara wengi licha ya kuwa wanatengeneza mamilioni ya faida kwa mwezi zaidi ya wafanyakazi wa kuajiriwa; lakini bado hawajiamini ukilinganisha na wafanyakazi wa kuajiriwa.

 

Binafsi katika ujasiriamali nimeizoeza akili yangu kujitambua kuwa mimi ndiye bosi hata kama niwe katika biashara yenye mtaji mdogo kiasi gani.


‘Im my own boss’. Shida ya wajasiriamali wengi huwa hawathamini hata maeneo wanayofanyia kazi.


Kama ni dukani, ni vema ukaweka hata meza fulani ya kisasa na kiti cha ‘kujiachia’ ili akili yako inavyoingia kazini iwe inapata uhuru wa kufikiri na kufurahia mazingira ya biashara.

 

Unapojitambulisha kwa watu usijitambulishe kinyonge, ongea kwa kujiamini.


‘Mimi ni mkurugenzi wa Massawe Kiosk’ ama ‘Mimi ndiye mmiliki wa magari yaendayo sehemu fulani’ au ‘Naitwa Albert Sanga, mmiliki na ofisa mtendaji mkuu wa Anesa Company Limited; badala ya kujiweka mnyonge na kusema, Naitwa Albert Sanga, nahangaikahangaika na biashara hizi na zile’. Kwa hivi hutakuwa na fikra zinazojiamini.


Wajasiriamali tunawajibika kujitoa asilimia zote kufanya biashara pasipo manung’uniko.

Haina tija kuwa katika ujasiriamali huku tukitamani tena kuajiriwa.


Unapochukua hatua ya kuufurahia ujasiriamali uufanyao ndipo utakapogundua kuwa ujasiriamali ni ajira kamili na kazi pekee inayoweza kukupa fedha za kutosha na muda wa kutosha kufurahia maisha.

0719 127 901, [email protected]


By Jamhuri