Vibarua wa kufunga maturubai mizigo ya makaa ya mawe kwenye malori wamevurugana na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga baada ya halmashauri hiyo kujitwalia mamlaka ya kutunza fedha zao katika akaunti ya halmashauri.

Kwa mujibu wa vibarua hao kutoka Kata ya Amanimakolo, wilayani Mbinga, ili kulipwa stahili zao ni lazima kwanza kipatikane kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na zaidi ya hapo, wamekuwa wakikatwa sehemu ya fedha hizo kibabe kwa ajili ya kuchangia shughuli mbalimbali za kijamii bila kuwapo kwa taarifa za matumizi ya fedha hizo kwa umma.

Akizungumza kwa niaba ya vibarua wenzake 60, Isaac Komba, amesema kazi zao hazina tofauti na makuli lakini wamekuwa wakishangazwa fedha zao kuwekwa kwenye akaunti ya pamoja ya Halmashauri ya Wilaya (Basket Fund) na kuwasababishia kuishi katika mazingira magumu mithili ya ombaomba.

Komba amesema kwa sasa kikundi chao chenye vijana 60 ambao kwa mwezi hufunga maturubai magari 1,500 hadi 2,000 ya makaa ya mawe, kiwango ambacho kimeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2013 walipoanza kazi hiyo wakiwa 46. Kwa wakati huo walikuwa wakifunga maturubai magari 500 hadi 1,200 kwa mwezi.

Amesema idadi yao imeongezeka hadi kufikia 60 Januari 2019 na katika mwezi huo ndipo walipoanza kukatwa asilimia tatu katika kila Sh 10,000.

Kufunga maturubai kunakozungumziwa hapa ni ile kazi inayofanywa ya kuyafunika makaa ya mawe mara baada ya kupakiwa kwenye lori ili yasipeperushwe kwa upepo, lengo likiwa ni kuhifadhi mazingira kwa sababu madini hayo yamechanganyika na madini mengine yenye kemikali kama vile ‘Pyrites’, ambayo yakichanganyika na maji hutengeneza ‘sulphuric acid’ ambayo ni sumu.

Amesema wanapomaliza kufunga turubai  kwa kila gari dereva hulipa Sh 10,000 papo hapo, kwa hiyo mwezi mzima hupata zaidi ya Sh milioni 18 lakini kinachowashangaza serikali ya kijiji imekuwa ikizichukua fedha hizo na kuzipeleka kwa mkurugenzi ambaye huziweka kwenye akaunti ya halmashauri kwa siku zaidi 40. Akitoa mfano, amesema Februari mwaka huu fedha hizo zilikaa kwenye akaunti hiyo kwa siku 51, na baada ya hapo ndipo wakalipwa.

Hata hivyo Komba amesema inapofika mwisho wa mwezi wamekuwa wakimkumbusha mtendaji wa kijiji kuhusu malipo yao na mara nyingi hupewa majibu tofauti, wakati mwingine hujibiwa kuwa mkurugenzi amesafiri, mtandao unasumbua, tatizo la umeme au dokezo lilichelewa kupelekwa. Wanahoji, iweje fedha zao ziingizwe kwenye mfumo wenye usumbufu dhidi yao?

Katika ufafanuzi wake kuhusu suala hilo, Komba amesema hata wanapolipwa fedha hizo wamekuwa wakikatwa Sh 10,000 kwa siku walizofanya kazi, yaani kama ni siku nne basi watakatwa Sh 40,000 kwa ajili ya mchango wa Sekondari ya Kata Amanimakolo bila kupewa risiti lakini pia kila mmoja hukatwa asilimia tatu ya kila Sh 10,000 sawa na Sh 3,000 ambazo hupelekwa halmashauri.

“Hivi kweli kwa serikali hii ya Rais John Magufuli mtu unamkata Sh 10,000 bila kutoa risiti … inaingia akilini? Kweli fedha ya kuli inapelekwa benki kwani sisi na kuli kuna tofauti gani?”amehoji Komba.

Kwa mwezi serikali ya kijiji kupitia makato ya asilimia tatu kwa kila Sh 10,000 hukusanya wastani wa Sh milioni 5.4 na makato ya Sh 10,000 mchango wa sekondari kwa mwezi kutoka kwa kila mmoja wao, kwa watu 60, serikali hiyo hukusanya zaidi ya Sh. 600,000 kwa sababu wakati mwingine wamekuwa wakikatwa hadi Sh 40,000 kwa kila mmoja hivyo kwa mwezi serikali ya kijiji hukusanya zaidi ya Sh milioni sita.

Komba amesema wamekuwa na shaka kuhusu matumizi ya fedha hizo za mchango ya sekondari kwa kuwa taarifa za mapato na matumizi hazisomwi kwa wananchi.

Pia amesema mwaka 2016/2017 serikali ya kijiji na kata kupitia afisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata waliwashauri watu 80 kutoa mchango wa Sh 10,000 kila mmoja na walitoa jumla ya Sh 800,000 kwa ajili ya kusajili kikundi chao lakini hadi leo kikundi hicho hakijasajiliwa, na wanapouliza kwa mtendaji na afisa maendeleo ya jamii wa kata hakuna majibu ya kuridhisha.

Ameeleza kutokana na kudai warudishiwe fedha hizo ndipo uongozi wa serikali ya kijiji na Kata ya Amanimakolo walipobadilisha utaratibu na kutaka kila mwananchi mwenye uwezo akafanye kazi hiyo ingawa vilevile amesema hawajui hatima ya Sh 800,000 zilizokwisha kukusanywa.

Komba amedai kuwa uongozi wa serikali ya kijiji umekuwa na mipango inayolenga kumwondoa kwenye kazi hiyo kutokana na kile wanachoamini kuwa ametoa siri na taarifa za ndani za shughuli yao kwa mwandishi wa Gazeti hili la JAMHURI.

Mmoja wa madereva wa malori yanayosafirisha  makaa ya mawe, Japhet Jeremier, kwa niaba ya wenzake amesema wamekuwa wakipata kero kutoka kwa wafungaji maturubai hao kwa kuwa licha ya kuwalipa Sh 10,000 bado wamekuwa wakiwaomba ‘posho’ ya chakula.

Mtendaji wa Kijiji, Michael Kiulu, amesema ni kweli vijana hao wanawakata mchango wa sekondari bila kuwapa risiti lakini suala lao linashughulikiwa, watapewa tu risiti zao pia fedha zao zinazokusanywa zinapelekwa kuhifadhiwa kwenye akaunti ya halmashauri na mwisho wa mwezi wanazichukua na kuwalipa baada ya kukata Sh 3,000 kwa kila Sh 10,000 na kukata mchango wa sekondari kwa kila mmoja Sh 10,000 kwa mwezi, ambapo kila mmoja kwa mwezi anakatwa Sh 13,000.

Mtendaji wa Kata, Joachim Ngaponda, amesema suala la usajili wa vikundi hufanywa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata lakini kwa wale wanaofunga maturubai hakuna kikundi kinachohusika bali kila mwananchi mwenye uwezo wa kufunga turubai anaandika barua na kuipeleka kwa mtendaji au mwenyekiti wa kijiji na kuna kamati inayohusika na uteuzi wa majina hayo kwa kuzingatia fursa kwa wote na si kikundi, kwani kuna wengine hawapo kwenye kikundi.

Kuhusu kuchelewesha malipo ya vibarua wa kufunga maturubai, amesema husababishwa na mfumo wa akaunti ya halmashauri. Amefafanua kuwa utaratibu wa kuzitoa fedha kwenye akaunti ya halmashauri na kuziingiza kwenye akaunti ya kijiji umekuwa na hatua ndefu na ndiyo maana wakati mwingine mchakato huo huchelewa, ikiwa ni pamoja na kuwasilishwa kwa dokezo kutoka kijijini.

Kuhusu kukatwa Sh 10,000, mtendaji huyo amesema uamuzi ulitolewa kwenye kikao cha maendeleo ya kata kilichofanyika Oktoba mwaka jana kwamba wanaofunga maturubai wachangie Sh 10,000 kwa mwezi na ikawa hivyo, kwa hiyo kudai kwamba wakifanya kazi siku nne wanakatwa Sh 10,000 si kweli.

Juu ya suala la kutotoa risiti, amesema wamekuwa wakitoa risiti moja na kuikabidhi kwa mtendaji wa kijiji ambaye huiwasilisha kwa kiongozi wa vibarua hao. Amesema suala la usajili wa kikundi cha wafunga maturubai atalifuatilia ili kubaini undani wake.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya kata, Michael Mapunda, amekiri ofisi yake kupokea Sh 800,000 kwa ajili ya kusajili na kuandika katiba ya vikundi vitatu ambavyo ni AMANIMAKOLO DRY PORT, JITEGEMEE WAFUNGA TURUBAI na JIKWAMUE WAFUNGA TURUBAI na kusisitiza kuwa fedha hizo zitatumika kama ilivyopangwa.

Diwani wa kata hiyo, Ambrose Mtalazaki, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga amesema suala la kusajiliwa vikundi vya vijana alielezwa kuwa limekwisha kufanyiwa kazi na kuhusu makato ya asilimia tatu kutoka kila Sh 10,000 amesema fedha hizo huingizwa kwenye akaunti ya halmashauri ya Kijiji cha Amanimakolo kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya kijiji chao.

“Vijana walikuwa wanachangishwa Sh 10,000 bila kupewa risiti, hivyo nilimwagiza mtendaji wa kata kama hatoi risiti mchango huo mimi naufuta kwa mamlaka yangu ya udiwani, ndipo alikwenda kununua kitabu cha risiti na kutoa kwa viongozi wao,” amesema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.

Amesema kabla ya utaratibu wa sasa, vijana hao walikuwa wakidhulumiana katika malipo kati yao lakini baada ya utaratibu wa sasa wamekuwa wakilipana kati ya Sh 260,000 hadi Sh 300,000 kwa mwezi wakati kabla ya utaratibu wa sasa walikuwa wakilipana Sh 50,000 hadi 60,000.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga, Pascal Ndunguru, amesema wanazichukua fedha hizo na kuziweka kwenye akaunti zao kwa lengo la kuwatunzia wahusika ili walipwe kiasi kikubwa mwisho wa mwezi pia kuwaepushia vurugu kwani awali walikuwa wakigombana walipokuwa wanachukua wenyewe na kuhifadhi.

Amesema hivi sasa kwa mwezi wamekuwa wakikusanya hadi Sh milioni 20 na mwisho wa mwezi wanawatolea na kuwalipa baada ya kukata asilimia tatu ya kila Sh 10,000, sawa na Sh 3,000, hivyo kwa mwezi halmashauri hukusanya Sh milioni sita na vijana hulipwa Sh milioni 14, na Februari mwaka huu walipoingiza Sh milioni 18 walikatwa Sh milioni 5.4 na kupelekewa Sh milioni 12.6.

Ndunguru amesema kutokana na utaratibu wa sasa fedha haziwezi kutolewa kwenye akaunti ya mfuko wa pamoja halmashauri (Basket Fund) bila idhini kutoka Benki Kuu, hivyo dokezo linapopelekwa na benki kuidhinisha matumizi ndipo na wao wanalipa, kwa hali hiyo dokezo kutoka kijijini likichelewa lazima fedha itachelewa kutoka.

“Hili la maturubai hata kwangu ni kero, haiwezekani fedha zitoke Amanimakolo ziende Mbinga na zirudi tena Amanimakolo, kwanini?”amehoji Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye.

Mkuu huyo wa wilaya amesema hatua hiyo ni kero, kwa sababu kama kazi inafanywa na vijana hao wa Amanimakolo na fedha hulipwa taslimu na madereva wa malori, fedha hizo zinakwenda halmashauri kufanya nini, tena zinawekwa benki ili iweje?

“Kama halmashauri ushuru wao ni Sh 3,000 kutoka katika kila Sh 10,000, kwa nini wasikate kiasi hicho na kuwaachia vijana fedha zao hapo hapo Amanimakolo? Hapo kinatengenezwa kitu gani kama si kuwepo kwa mazingira ya rushwa kutokana na adha wanayoipata madereva kutoka kwa wafunga maturubai?” amehoji DC Nshenye.

DC amemwagiza mkurugenzi kukaa pamoja na vijana hao wafunga maturubai, madereva wa malori na viongozi wa serikali ya kijiji na kata ili kurekebisha tatizo linalolalamikiwa na vijana hao na madereva.

Utaratibu wa kazi kama hizo hufanywa katika viwanda na mashirika mbalimbali hapa nchini, kama vile  Kiwanda cha Saruji Mbeya na hata Kitengo cha Hifadhi ya Chakula cha Taifa cha serikali kilichopo Songea ambapo vijana wenyewe au kila mtu anafanya kazi na kupata mgawo wake kwa siku au wiki hata mwezi na kupanga matumizi yake, ikiwa ni pamoja na kujiwekea akiba benki.

Sera ya Taifa ya Vijana iliyoandaliwa mwaka 1996 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2017 inalenga kusimamia masilahi ya vijana, ikiwa ni sambamba na kuwawezesha kiuchumi kwa lengo la kuhakikisha taifa linakuwa na vijana wenye uwezo, ari ya kutosha, wawajibikaji na wanaoshiriki kikamilifu katika nyanja zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa maendeleo ya jamii. Vilevile kuweka mazingira yanayowezesha kujenga uwezo wa vijana na kukuza nafasi za ajira, sambamba na kupata huduma ya hifadhi ya jamii.

By Jamhuri