Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Timu ya Soka ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, Hans Van Der Pluijm, ametema nasaha nzito kwa timu hiyo, ambazo zinastahili kuzingatiwa pia na klabu nyingine za soka hapa Tanzania.

Akizungumza katika hafla ya kumuaga iliyofanyika jijini Dar es Salaam wiki iliyopita baada ya kuifundisha Yanga kwa kipindi cha miezi minne, Pluijm aliwaasa viongozi wa timu hiyo kuzingatia mambo yafuatayo:

Kuimarisha ushirikiano kuanzia kwa wachezaji, benchi la ufundi, kamati ya usajili, viongozi, wanachama na mashabiki kwa jumla.

Kwa mujibu wa Plujm, mambo hayo yakizingatiwa kwa vitendo, yataisaidia timu ya Yanga kustawi na kutamba katika tasnia ya soka.

Akasisitiza kuwa ushirikiano huo utawezesha kujua matatizo yaliyopo baina yao na kuyatafutia ufumbuzi, hivyo kuijenga timu hiyo na kuiwezesha kufanya vizuri katika mashindano ndani na nje ya nchi.

Pluijm alikwenda mbali kwa kuwataka viongozi wa Timu ya Yanga kuwa na maono ya mbali zaidi ya kupata ubingwa wa ligi ya ndani, badala yake wajikite pia katika kuandaa kikosi imara kitakachoweza kutwaa ubingwa wa Afrika.

Alikiri kwamba Timu ya Yanga ina wachezaji wenye vipaji vya soka ambavyo vinastahili kuendelezwa ili hatimaye viweze kucheza katika klabu kubwa vya soka duniani, vikiwamo vya Ulaya, hivyo kuijengea Tanzania hadhi ya kimataifa katika tasnia ya soka.

“Jambo hilo linawezekana, kikubwa ni kuwa na misingi mizuri ambayo itasaidia kuwaandaa wachezaji wanaojitambua na kutambua kuwa soka ni kazi inayofanya maisha yao yasonge mbele, pia kujiona wao ni mabalozi wa Taifa,” alisema Pluijm ambaye aliahidi kuwa mshauri wa Yanga katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusaka wachezaji bora wa kigeni.

Nasaha zilizotolewa na Pluijm kwa viongozi wa Timu ya Yanga zinastahili kuzingatiwa pia na timu nyingi za soka hapa nchini, kwani zimejaa mbinu za kusaidia kufikia mafanikio makubwa katika tasnia ya mpira wa miguu.

Kama alivyosema Pluijm, dhana ya ushirikiano unaogusa muundo mzima wa klabu ya soka ndiyo njia pekee ya kufikia mafanikio. Ushirikiano mpana unasaidia kutatua matatizo yanayokwaza maendeleo ya soka.

Kukosekana kwa dhana ya ushirikishwaji wa wadau wote siku zote ni chanzo cha matatizo na migogoro isiyokoma katika klabu za soka hapa nchini.

Matumaini ya wengi ni kwamba uongozi wa Timu ya Yanga umeupokea na utauzingatia kwa vitendo ujumbe mzito uliotolewa na Pluijm, lakini na timu nyingine za soka hapa nchini zikiwamo Simba, Azam na  Mbeya City nazo zinapaswa kuufanyia kazi ili ziweze kufikia mafanikio makubwa.

Kwa upande mwingine, klabu za soka Tanzania zinapaswa kuwa makini kwa kuhakikisha zinakuwa na viongozi bora watakaozisaidia kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya soka na uchumi.

Ushirikiano imara utasaidia kupata wachezaji wenye vipaji mahiri vya soka, ambao licha ya kuziwezesha timu zao kutwaa ubingwa katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi, watakuwa chachu ya kuziinua kiuchumi.

Pluijm ameanika mbinu ya mafanikio ya klabu za soka. Kazi imebaki kwenu viongozi wa klabu za soka Tanzania.

871 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!