* Ni aina ya vibambara, wapakwa mafuta kuvutia wateja

*  Wakaushaji wanatumia nguo chakavu, pumba, plastiki

Ukaushaji wa samaki kwa njia ya moshi (kubanika) katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza na vitongoji vyake sasa unaanza kuwatia shaka walaji wa samaki hao na wataalamu wa afya.

Walaji wa samaki, hasa wa aina ya sangara (Nile Perch) na sato (Tilapia) ambao wanakaushwa kwa moshi katika Kanda ya Ziwa Victoria maarufu kama vibambara hawatayarishwi katika mazingira salama ya kiafya na mamlaka husika zinaelekea kutokuwa makini katika jukumu la kuhakikisha usafi na usalama wa chakula kwa walaji.

Samaki waliotayarishwa katika mazingira machafu wanadaiwa kuwa kisababishi cha maradhi kutokana na mazingira na vifaa vinavyotumika, ama kuwahifadhi, au kukaushia samaki hao.

Jiji la Mwanza, vitongoji vyake na baadhi ya visiwa vilivyo ndani ya Ziwa Viktoria ni maarufu kwa ukaushaji wa samaki. Kwa Jiji la Mwanza samaki wengi wanakaushwa katika Wilaya ya Ilemela, hasa majumbani na katika baadhi ya fukwe za wavuvi.

Zipo taarifa kwamba utayarishaji wa samaki wa kukausha kwa moshi unaweza kusababisha maradhi kwa watumiaji kama mambo kadha hayakuzingatiwa. Mambo haya ni kama vyombo vinavyotumika, kuwaosha samaki kabla ya kuwasha moto, mahali wanapohifadhiwa tayari kwa kukaushwa, aina ya kuni zinazotumika, muda wa ukaushaji, n.k.

Labda ukaushaji huo ungezingatia utaalamu huenda hatari hiyo ingeweza kuepukika kwa kiasi fulani, lakini uchunguzi wa gazeti hili umethibitisha ukaushaji wa samaki hao unaofanywa na baadhi ya wauza samaki kwa kiasi kikubwa unafanyika bila kujali afya za walaji.

Kwa kawaida, miaka ya nyuma kuni zilitumika kukaushia samaki hao, lakini kutokana na uhaba wa miti na uchu wa kupata faida kubwa kwa baadhi ya waandaaji wa samaki hao, wamegundua njia nyingine za kukausha samaki hao.

Miti imekuwa michache katika maeneo ya wavuvi hali ambayo imelazimu kubuni mbinu mbalimbali za ukaushaji samaki. Katika Wilaya ya Ukerewe, sehemu kubwa ya miti katika visiwa hivyo imetoweka kutokana na kutumika kwa kukaushia samaki na shughuli nyingine za kibinadamu.   Wilaya ya Ukerewe ina visiwa 39, lakini kutokana na shughuli za kibinadamu ukiwemo uvuvi, miti imepungua.

Kwa maeneo ya Jiji la Mwanza uhaba wa kuni umewafanya baadhi ya wakausha samaki hao kutumia nguo kuukuu, karatasi, mifuko ya plastiki kwa nia ya kupata moshi mwingi ambao ndio hukausha samaki hao. Wengi hutumia uchafu utokanao na mbao katika viwanda pamoja na pumba zitokanazo na mazao mablimbali.

Nyamtondo Elias (46), mmoja wa wakausha samaki katika eneo la Ilemela jijini Mwanza, anasema ingawa yeye hutumia kuni na pumba ni kweli wapo wenzao “wachache” wanatumia vitu visivyofaa katika kukaushia samaki.

“Mimi nakausha kwa kuni, nikikosa kuni natumia pumba ama maranda, lakini wapo wenzetu wachache ambao ni kweli hutumia nguo kuukuu na mifuko ya plastiki katika ukaushaji, bila shaka samaki wa aina hiyo ni hatari,” alisema na kuongeza kwamba tabia hiyo imeenea zaidi katika baadhi ya maeneo ya jiji hilo.

“Hapa Mwanza utapata wapi kuni za kukaushia samaki wakati hata mkaa tu bei yake ni kubwa? Mkausha samaki yeyote anaangalia kama anaweza kupata faida, hii imesababisha baadhi yetu kubuni njia mbalimbali za ukaushaji usio na gharama kubwa zikiwemo hizo za kutumia nguo kuukuu na mifuko ya plastiki,” alisema.

Naye Michael Malimi (41) ambaye ni mfanyabiashara ya samaki wa kukaushwa kwa moshi alikiri kwamba hali hiyo ipo kwa baadhi ya wakaushaji.

“Ukaushaji wa sangara kwa kutumia nguo kuukuu, nailoni na kandambili upo ingawa sasa umepungua baada ya walaji wengi wa samaki wa aina hiyo jijini Mwanza kuwasusa wakitaka samaki kutoka visiwani ambao hukaushwa kwa kuni,” alisema.

Malimi anasema kwa sasa (Februari, 2014) wakaushaji wa samaki kwa kutumia nguo kuukuu wamepungua jijini Mwanza. Lakini wakati wa kipindi cha mvua wanaongezeka kutokana na “malighafi” kubwa wanazotumia wakati huo kunyeshewa, hivyo kushindwa kutoa moshi unaohitajika kukausha samaki.

Alizitaja malighafi zinazotumika kukaushia samaki kwamba ni pamoja na mabaki ya mbao baada ya kupigwa randa na pumba zitokanazo na mazao mbalimbali. “Siyo wote wanatumia hizo nguo kuukuu ama nailoni, lakini wachache wetu wanatumia hadi sasa,” alisema Malimi.

Afisa Afya wa Jiji la Mwanza, Danford Kamenya, alikiri kuwa taarifa hizo zipo. “Nimesikia habari hizo, nipo Shinyanga nikirudi Mwanza tuwasiliane,” alisema na kuahidi kufuatilia suala hilo na kutoa majibu. Hata hivyo, pamoja na mwandishi kufika ofisini kwa Kamenya, mwezi mmoja baadaye, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.

Lakini akizungumza kwa simu baadaye hivi karibuni, Kamenya alisema baada ya kupata taarifa hiyo vyombo husika vilifuatilia. Hata hivyo, majibu ya ufuatiliaji huo hakuyatoa kwa madai kwamba mpaka kibali kipatikane kutoka kwa Mkurugenzi wa Jiji ambaye angemruhusu kuzungumzia suala hilo linalogusa maisha ya watu wengi kibiashara, kiafya na ajira.

“Nenda kwa Mkurugenzi wa Jiji akupe kibali, ila najua hayupo,” alisema Kamenya kwa njia ya simu. Mwandishi wa habari hizi amefuatilia kwa muda sasa na hajafanikiwa kumpata Mkurugenzi wa Jiji, Alfa Hassan Hida.

Gazeti hili limewasiliana na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Mwanza na kupitia ofisa wake, Moses Mbambe alielezea jinsi samaki wanavyokaushwa na kwamba ofisi yake italifuatilia suala hilo kwa kushirikiana na Idara ya Uvuvi, Udhibiti na Ubora.

Mbambe ambaye hakukataa ama kukubaliana na habari hizo alitoa maelezo machache juu ya ukaushaji samaki kwa njia ya moshi. “Kabla sijaeleza hatua zitakazochukuliwa ni vema kwanza ukafahamu teknolojia inayotumika katika ukaushaji wa samaki. Samaki wanakaushwa kwa moshi ambao unakuwa na joto lengo likiwa kukausha maji maji ambayo ndiyo yanayosababisha samaki kuharibiwa na bakteria.”

Akaendelea, “Lakini la pili ni kupata ile harufu ya moshi (smoked flavour) ambayo wateja huwa wanaipenda kwani inasemekana inaongeza ladha ya samaki ndiyo maana hata sausages huwa zinafukizwa moshi ili kupata ile harufu nzuri ya moshi.”

“Katika hili uchaguzi wa kuni zinazotumika kupata ile harufu ya moshi ni la muhimu sana,” alisema Mbambe.

Mbambe aliongeza kwamba iwapo samaki watakaushwa kwa kutumia nguo chakavu, maplastiki na matairi basi samaki hao watanuka moshi wa matairi, kwani vyakula aina ya protini vina tabia ya kuchukua harufu nyingine kwa haraka, hivyo kufanya chakula hicho kutolika kutokana na kuwa na harufu mbaya.

“Pamoja na maelezo haya taarifa hii bado itafanyiwa kazi kwa kushirikiana na ofisi ya Uvuvi Idara ya Udhibiti Ubora (Fish Quality Control) na kukupa majibu mapema iwezekanavyo,” alisema, lakini hadi sasa majibu hayo hayajatolewa.

Katika eneo la Igombe ambalo ni maarufu kwa ukaushaji huo ilibainika kwamba wengi wa wakaushaji samaki kwa njia ya moshi hutumia pumba na mabaki ya mbao ingawa mwandishi alifanikiwa kukuta kandambili kuukuu na mifuko ya nailoni ambayo baadhi ya wakaushaji walidai inatumika kwa kuwashia moto.

Moshi utokao katika tanuru la kukaushia samaki hao ni mkubwa na kwa baadhi ya wakaushaji hawaruhusu mtu wasiyemjua kufika karibu na tanuru.

Mama Agness Yuda, mmoja wa wakaushaji hao, alisema, “Ni kweli huko nyuma baadhi ya wakaushaji walitumia hizo nguo chakavu, plastiki, nailoni, viatu vikuukuu kukaushia sangara, lakini sasa wengi wetu tumeacha,” alisema na kuongeza kwamba hali ya kukausha kwa nguo kuukuu na vitu vingine inasababishwa na bei kubwa ya kuni.

“Faida ni ndogo sana na pengine usipate faida kabisa kama utatumia mkaa ama kuni, ndiyo sababu tunatumia pumba na mabaki ya mbao wakati wa kuranda,” alisema na kuongeza, “Hizi nailoni unazoona ni kwa ajili ya kuwashia moto tu.”

Kwa mujibu wa Mama Agness, kupungua kwa ukaushaji wa sangara kwa kutumia nguo kuukuu na plastiki kunatokana na ukweli kwamba jijini Mwanza baadhi ya walaji wanawaona wakaushaji hao, wanaishi nao na pia baadhi huwagundua samaki wa aina hiyo ambao huwa weusi ama kijivu kupitiliza na hutoa harufu.

Mama Agness anaongeza, “Kwa baadhi ya walaji wakubwa wa samaki wa aina hiyo hupendelea wale wanaotoka visiwani katika wilaya za Muleba (iliyopo mkoani Kagera) na Ukerewe maana wenzetu hawa wanatumia kuni.”

Alivitaja baadhi ya visiwa ambavyo hutumia kuni kuwa ni Goziba, Kerebe, Ghana, Bulubi, Kamasi, Irugwa, Ukara, Buluza, Lyegoba, Kulazu, Kweru Muto, Bumbile na Galinzila. “Hawa hutumia kuni na ni rahisi kuwagundua wasiotumia kuni kwa vile wapo kwenye makambi, kwa hapa Mwanza ni vigumu maana wengi wanakaushia majumbani mwao,” alisema.

Anasema, “Mazingira ya kibiashara yamelazimisha baadhi yetu kuachana na ukaushaji wa kutumia matambara hayo, lakini siyo kwamba tumeacha wote, bado kuna wanaotumia haya matambara na plastiki.”

Anasema matambara na plastiki zinatumika kwa vile yana moshi mwingi ambao unahitajika sana katika ukaushaji wa samaki.

Akiwa katika kisiwa cha Ghana, mwandishi wa habari hizi alishuhudia jinsi sangara wanavyokaushwa kwa moshi. Pia mwandishi wa habari hizi alifanikiwa kufika Bulubi na Lyegoba, Ukerewe na kukuta hali ni ileile, yaani ukaushaji kwa kutumia kuni.

Matanuru yote yalikuwa yakitumia kuni ingawa baada ya kuwakausha kwa moshi wahusika walikuwa wanawapaka mafuta ya nazi, pamba na kwa baadhi mafuta ya sangara kwa lengo la kuwafanya samaki hao kumeremeta na kuvutia wateja.

Kwa mnunuzi wa samaki aliyepakwa mafuta ni rahisi kuhadaika maana samaki wa aina hiyo hugeuka na kuwa na rangi kama ya njano inayovutia macho ya mlaji ambaye hudhani ni mafuta ya samaki husika.

Afisa Afya wa Jiji la Mwanza ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa madai ya kutokuwa msemaji na kwamba suala linalozungumziwa ni nyeti, alikiri kwamba naye amekuwa akisikia habari hizo.

“Nimekuwa nasikia habari hizi, sijazithibitisha bado, lakini nijuavyo plastiki ikitumika kukaushia samaki ni sawa na kuwakausha samaki kwa kutumia sumu, maana unapochoma plastiki ni sawa na kutengeneza sumu,” alisema na kuahidi kufuatilia.

Makala hii imetafitiwa na kuandikwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Waandishi wa Habari Tanzania (TMF).

2404 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!