Kwa muda wa miaka mitatu nchi yetu imeshuhudia mnyukano wa mchakato wa kupata Katiba mpya. Mnyukano huu ulianza rasmi mwaka 2011 Rais Jakaya Kikwete alipotangaza kuandikwa kwa Katiba mpya. Tangazo la Rais Kikwete lilianzisha mchakato wa kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo hatimaye imelifikisha taifa katika kupata rasimu.
Rasimu ya Katiba ya kwanza ilitolewa June 3, mwaka 2013 na Desemba 31, mwaka 2013 ikatolewa rasimu ya pili ya Katiba. Ni kweli rasimu hii inatajwa na wengi kuwa ina upungufu mkubwa. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wao wanasema imependekeza mfumo wa Serikali tatu bila kupata ridhaa ya wananchi.
Inatumia idadi ya watu waliotoa maoni ya Serikali tatu kuwa ni 17,000 tu kati ya 340,000 ya watu waliotoa maoni, na kwamba maoni haya hayakutolewa katika mazingira mahususi ya kuwahoji Watanzania iwapo wanautaka Muungano au la na iwapo wanautaka uwe wa Serikali ngapi.
Kwa wenye kumbukumbu, wanawasuta CCM kuwa wao ndio walitumia nguvu kubwa kupinda sheria isiruhusu kuhoji Muungano iwapo wananchi wanautaka au la, ambapo iwapo swali hilo lingeruhusiwa na sheria mwaka 2011 mgogoro ulipo sasa kamwe usingejitokeza. Wapo wanaosema Katiba inavunja Muungano kijanja kwa kurejesha mamlaka yote kwa nchi za Zanzibar na Tanganyika.
Kwa upande wa wapinzani, wanaongozwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi, wenyewe wanasema rasimu ya Katiba inapaswa kupitishwa kama ilivyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba. Wanasema kupinda misingi ya Serikali tatu iliyopendekezwa na Jaji Warioba itakuwa ni kuvunja Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Wapo wanaohoji kuwa ikiwa UKAWA wanataka rasimu ya Katiba ipitishwe kama ilivyopendekezwa kuna sababu gani ya kuwapo Bunge Maalum la Katiba. Profesa Patrick Otieno Lumumba kutoka Kenya, amewataka UKAWA kurejea bungeni kwa masilahi ya taifa na usitawi wa Tanzania.
Amesema Kenya na nchi nyingine za Afrika wanaiona Tanzania kama nchi ya kupigiwa mfano iliyoamua kuruhusu mfumo wa vyama vingi na ikaendelea kuwa na amani, ila kupitia msimamo wa UKAWA anaona malaika wa vita wanaiita Tanzania kwa kasi itumbukie katika vita.
Anaonya kuwa hatua iliyofikiwa na Kenya mwaka 2007, ambapo walikufa watu zaidi ya 1,500 na zaidi ya 10,000 kukimbia makazi yao si ya kuruhusu ikaingia Tanzania kutokana na ubishi wa kisiasa. Amesema Tanzania imevuka maziwa, iweje leo itumbukie katika vidimbwi? Akawasihi ukawa kuwa si kila wanachokitaka wanaweza kukipata chote siku moja.
Maneno haya ya Profesa Lumumba na wengine waliotoa wito wa UKAWA kurejea bungeni yametugusa. Tunaamini UKAWA hawatamani kuona nchi hii inatumbukia katika vita na kukanyaga maiti kama daraja la wao kwenda Ikulu. Kuna kila dalili kuwa kama taifa tunaelekea huko.
CCM nao tunasema hali ilikofika sasa wasisahau usemi kuwa asiyesikia la mkuu, huvunjika guu. UKAWA na CCM mnayo dhamana ya kuwaenzi Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume kwa kuiepusha nchi hii isitumbukie katika vita. Tunasema ikibidi CCM wasitishe mchakato wa Katiba.
Mgogoro ulipofikia nchi ijipange upya, Katiba iandaliwe mazingira mazuri ya kuijadili na asiwepo wa kujiona ameshindwa katika harakati hizi, bali sote tujione tu washindi kwa heshima ya kuliepusha taifa letu na vita. Tukae chini, tujipange upya nchi yetu isonge mbele izidi kudumisha amani na utulivu, kisha tupate Katiba mpya muda mwafaka bila kumwaga damu. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri