Kwa hivi sasa mashine za kielektroniki za EFD za TRA, imekuwa ndiyo habari ya ‘mjini’ kwa wafanyabiashara karibu kila kona nchini. Hii imekuja baada ya awamu nyingine ya TRA kujumuisha wafanyabiashara wengi zaidi tofauti na ilivyokuwa mwanzo wakati zikiingia.

Awamu ya kwanza ya TRA katika uhamasishaji wa matumizi ya mashine hizi iliwalenga wafanyabiashara wenye mitaji mikubwa, na hawa wafanyabiashara wengine wadogo walidhani kuwa mfumo wa mashine hauwahusu. Baada ya awamu ya sasa kuonekana kuwa inatakiwa hata hawa wafanyabiashara wadogo watumie mashine hizi, ndiyo maana kumekuwa na kuhamaki, woga na mshikemshike wa kutosha.

 

Siku chache zilizopita nilipata wasaa wa kuzungumza na mfanyabiashara anayemiliki duka dogo la kuuza bidhaa za nyumbani. Yeye alinieleza kuwa TRA wameshawaelekeza kuwa wanunue mashine hizo na waanze kuzitumia.

 

Malalamiko yake yalikuwa katika gharama za mashine hizo na uharaka wa TRA pasipo kuzingatia uwezo wa mfanyabiashara husika katika kununua mashine hizo. Kwa maelezo yake alisema gharama za mashine hizo ni mzigo hasa kwa wafanyabiashara wadogo kama yeye.

 

“TRA wangefanya kama wanavyofanya Tanesco ama idara ya maji kwa kukodisha mashine hizo. Badala ya kusema tununue kwa shilingi laki sita ama laki nane ama zadi; wangekuwa wanatupatia hizo mashine bure halafu sisi tuwe tunaendelea kulipa kidogo kidogo ama tuwe tunalipia pango ya mashine hizo,”

 

Mfanyabiashara huyu aliendelea kunieleza hisia zake:  “Wao TRA wanasema kuwa fedha tunazonunulia mashine tutarudishiwa kupitia kodi tunazolipa kwa maana kuwa kutakuwa na hela wanayoirejesha kupitia makadirio wanayotufanyia.

 

“Hilo ni jema lakini mzigo unaoendelea kuja ni huo wa kuinunua mashine hii kwa mkupuo. Mimi na biashara kama hii unaniambia ninunue mashine ya laki nane si unataka niue kabisa mtaji?

 

“Hatukatai hizi mashine lakini TRA ingejaribu kuangalia uwezekano wa kutusaidia kuzimiliki pasipo maumivu makubwa hasa sisi wenye vimitaji vidogo.”

 

Ninachokiona katika suala hili la mashine za kielektroniki ni ule utamaduni wa kuona kama kulipa kodi ni adhabu. Ukiwasikiliza wafanyabiashara wengi utagundua kuwa hofu yao kubwa ni kuwa huenda mashine hizi zikawafanya wawe wanalipa kodi kubwa kupindukia.

 

Nafahamu kuwa kila kitu kipya huwa hakipokewi haraka haraka kwa mikono miwili; lakini suala la hizi mashine na ulipaji kodi kwa ujumla yafaa tulitazame kwa jicho la tatu.  Kimsingi kumekuwa na changamoto kubwa katika eneo la ulipaji kodi kwa nchi yetu. Kama ambavyo mara kwa mara TRA imekuwa ikiwabaini na kuwakamata baadhi ya wafanyabiashara wanaokwepa kodi; inaonesha dhahiri kabisa kuwa ipo shida.

 

Katika utafiti wangu nimebaini kuwa katika Taifa letu tuna makundi manne yenye hulka tofauti tofauti katika ulipaji kodi. Kundi la kwanza ni lile la wafanyabiashara wanaokwepa kabisa kodi.  Kundi la pili wanalipa kodi lakini hawalipi kiuaminifu. Kundi la tatu ni wale wanaolipa kodi halali na kwa uaminifu lakini wanafanya hivyo kwa manung’uniko na malalamiko mengi. Kundi la mwisho ni la wafanyabiashara wanaolipa kodi halali, kwa uaminifu na kwa furaha kabisa.

 

Lipo tatizo la kimtazamo na kifikra miongoni mwa wafanyabiashara wengi. Upande wa mtazamo ni vile wanavyotazama kodi zinakwenda wapi wakishazilipa; wakati upande wa kifikra ni namna wafanyabiashara wanavyolitazama suala la kodi katika maendeleo yao ya kibiashara.

 

Nianze na hili la kifikra. Kumekuwa na utamaduni uliozoeleka na unaoaminika miongoni mwa wafanyabiashara wengi kudhani kuwa kutakiwa kulipa kodi ni suala la uonevu. Fikra hizi zinaamini kuwa kodi si jambo la lazima kwao na kwa wengine na kulazimishwa kulipa kodi ni kama kulazimishwa utumwa.

 

Imani ya namna hii husababisha wafanyabiashara wengi kuanza kutafuta mianya ya kukwepa kodi kiasi kuwa wapo ambao hudiriki hata kutengeneza mitandao ya kufanikisha ukwepaji huu. Fikra hizi zinachagizwa zaidi na tetesi, taarifa, fununu ambazo huwa zinazagaa mitaani kuwa mfanyabiashara fulani anafanikiwa kwa sababu ya kukwepa kodi.

 

Kimsingi, kunaweza kusiwe na ukweli ama ushahidi kuwa fulani na fulani wanakwepa kodi, lakini kuwapo kwa tetesi hizo ni sumu kwa wafanyabiashara wengine wanaosikia fununu hizo. Huu huwa ndiyo mwanzo wa wafanyabiashara kuidanganya TRA kuhusu mauzo na mapato yao wakati wa kukadiriwa kodi.

 

Upande mwingine unaosababisha wafanyabiashara wengi kudiriki kukwepa ama kudhulumu kodi ni mtazamo wanaokuwa nao kuhusu zinakokwenda kodi zao. Kutokana na taarifa za mara kwa mara za ufisadi na ufujaji wa fedha kodi unaofanywa na viongozi serikalini; wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao wameweka nadhiri za ama kutolipa kodi kabisa, au kulipa kodi kiupungufu.

 

Mioyoni mwao wanajisemea, “Hakuna sababu ya kulipa kodi wakati nikilipa kodi hiyo kuna watu wanakwapua na kwenda kujijengea mahekalu yao.

 

“Siwezi kulipa kodi kwa sababu nikilipa kodi wapo wajanja wengi wanaikwapua na kuifanyia anasa mtaani mbele ya macho yangu.”

 

Wengine wanajisemea, “Sitakaa nilipe kodi kwa uaminifu mpaka serikali itakapokomesha ufisadi uliokithiri.”

 

Kutokana na mtazamo huo nimepata kumuuliza mfanyabiashara anayemiliki kampuni swali hili: “Kuna umuhimu gani wa kulipa kodi, ikiwa kodi tunazolipa zinaishia mifukoni mwa wajanja wachache?”

 

Mfanyabiashara huyu alinijibu swali langu kwa kuniuliza swali jingine lifuatalo: “Kuna umuhimu gani wa kuendelea kutoa sadaka kanisani wakati tunasikia kila siku habari za wachungaji ambao wanazitumia sadaka zetu kuishi maisha ya kifahari na kujineemesha wakati waumini wengi wanaishi maisha ya umaskini uliokithiri?”

 

Wakati nikiwa bado naweweseka kutoa jibu kwa swali lake, ‘akanitwanga’ swali jingine, “Katika hali kama hiyo unaweza kuendelea kutoa sadaka kanisani?” Nikamjibu “ndiyo” Baada ya kumpa jibu hilo akaendelea kunipa somo kuhusu kodi ambalo lilinifanya tangu wakati ule mpaka leo niendelee kutazama ulipaji wa kodi katika mtazamo chanya.

 

Ufisadi, wizi na ukwapuaji wa kodi unaofanywa na viongozi na watawala wetu serikalini haufuti umuhimu na uhalali wa kodi kwa nchi na Serikali. Wewe kusikia habari za wanaofuja kodi zetu hakukupi haki ya kujitoa katika wajibu wa kulipa kodi. Hii ni kwa sababu ufisadi serikalini ni uovu na ukwepaji kodi ni uovu pia. Huwezi kumaliza uovu kwa kutumia uovu. Huwezi kumaliza suala la ufisadi serikalini kwa wewe kukwepa kodi.

 

Kama ambavyo huwezi kuacha kutoa sadaka kanisani kwa sababu mchungaji anakula hizo sadaka, ndivyo ambavyo huwezi kuacha kulipa kodi kwa sababu zinaibwa! Hata kama sadaka zinaliwa kanisani lakini tunatoa sadaka huku imani yetu ikiwa kwa Mungu na si kwa mchungaji.

 

Kinachofanya tulipe kodi ni ile kutambua kuwa ni wajibu wetu, kutambua kuwa msingi wa kodi ni kwa ajili ya maendeleo yetu na ya taifa letu. Vile vile tunalipa kodi tunapotambua kuwa kufanya hivyo ni kama kutoa shukurani kwa mazingira yaliyoandaliwa hata yakatuwezesha kupata faida tuliyoipata.

 

Tuiase Serikali ijichunguze na kujisaili namna inavyotumia kodi zetu na ikibidi tuiwajibishe.  Pamoja na hayo, kamwe tusijivue wajibu wa kulipa kodi kwa uaminifu. Kama ilivyo kanisani tunaweza kumuhoji, kumhamisha ama kumfuta kazi mchungaji wetu kwa kufuja mapato ya kanisa lakini kamwe sisi waumini hatuwezi kuthubutu kuzira kutoa zaka na sadaka!

 

Hakuna sababu ya kulipa kodi kwa shingo upande, timiza wajibu wako kwa furaha. Kukwepa kabisa kulipa kodi hakuwezi kukufanya uwe na furaha, ni kama kufuga joka ambalo kila siku litabaki likikutisha. Unahofu muda wote, “Itakuwaje nikikamatwa?” Na kimsingi siku unapokuja kubainika itakuharibia sifa na jina lako kibiashara. Yote hii ni ya nini?

 

Na tena usidhani kuwa kukwepa kabisa kodi kutakusababisha uwe tajiri zaidi, la hasha! Hapo ni kama kujitafutia tu matatizo rohoni mwako na kwenye biashara zako.

 

Hata zama za Yesu Kristo kwenye nchi aliyokuwapo kulikuwa na dhuluma nyingi, kulikuwa na ufisadi wa kutisha na kulikuwa na uonevu uliokithiri. Pamoja na hayo yote hata siku moja Yesu hakuwahi kuendesha mgomo wa kutolipa ama wa kukwepa kodi. Tena la kusikitisha ni kuwa kodi alizokuwa akilipa ndizo hizo hizo zilizowalipa posho na mishahara askari waliomsulubisha hadi kumuua. Ni kodi hizo hizo zilizotumika kuchongea msalaba uliotumika kumnyongea.

 

Pamoja na hayo ni yeye Yesu ambaye wakati wote alisisitiza watu walipe kodi kwa uaminifu na kwa wakati na ndio maana akasema, “Ya Mungu mpeni Mungu na ya Kaisari mpeni Kaisari.”

 

Mafanikio ya kweli kibiashara ni yale yanayothamini ustawi wa Taifa lako na ya watu wengine. Biashara yako inapolipa kodi, kodi yako inakwenda katika ujenzi wa miundombinu, inakwenda katika kutoa maarifa na elimu kwa watoto wetu, inakwenda hospitalini kuokoa maisha na uhai wa wanadamu wenzetu. Achana na hawa wezi, mafisadi na wadokoaji kadhaa serikalini, bali itazame kodi kwa ujumla wa umuhimu na uzuri wake.

 

Kiufupi tunaweza kusema kodi inaongeza thamani katika maisha ya raia wenzetu. Kufanya biashara pasipo kulipa kodi ni udhulumaji, ni unyonyaji na ni wizi wa maisha ya wengine. Ni udhoofishaji wa afya za wanadamu wenzako, ni uuaji wa maisha ya wenzio na hata uwe na mabilioni mengi kiasi gani, hayo hayawezi kuwa mafanikio halisi na ya kweli.

 

[email protected]

+255 719 127 901

By Jamhuri