Wengi tumemsikia Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, akiwaambia wanachama waliokatwa majina kwenye vikao vya mchujo kwamba anayetaka kukihama chama hicho, ahame haraka. Amesema CCM haiwezi kufa, na akaongeza kwamba wanaodhani kuwa CCM itakufa, watatangulia kufa wao.

Inavyoonekana ni kwamba Rais wetu bado hajasahau vionjo vya misemo ya kipwani pwani! Tunakumbuka wakati fulani alipata kusema “kelele za chura hazimzuii ng’ombe kunywa maji.” Akaongeza msemo mwingine wa “kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala.” Misemo hii ilikuwa ni ujumbe wake kwa wapinzani.


Sijasahau pale aliposema kwamba “wasichana wanapata mimba kutokana na kiherehere chao!” Wakati mwingine misemo ya aina hii ni mitamu, hasa tunapokuwa tumechoka kusikiliza hotuba ndefu za viongozi, na wakati mwingine hotuba fupi zisizokuwa na mantiki. Ukiwa umechoka, ukasikia misemo ya aina hii, unaweza kurejea kwenye hali ya “kuwapo kwenye eneo la tukio”.


Mara kadhaa nimesema kwamba CCM wana ada ya kujidanganya kwa kudhani kwamba kuwaambia wanachama kwamba “wanaotaka kwenda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waende sasa,” ni jambo jepesi.

 

Tena basi, Mwenyekiti amejipa matumaini kwa kusema wanachama waliojitokeza kuomba ridhaa ya kukiwakilisha chama kwenye uchaguzi ni zaidi ya 5,000; lakini waliotakiwa ni zaidi kidogo ya 2,000.


Kwake yeye, hii ni idadi kubwa mno! Sijui kama ameshapata kuona ni wanachama wangapi wanaojitokeza kuwania uongozi ndani ya vyama vya upinzani kama vile Chadema!

 

Nimepata kusema kwamba wananchi kadhaa, wakiwamo wana-CCM wanakichukia chama hicho, si kwa sababu kina sera mbovu au kimepoteza mwelekeo moja kwa moja, bali ni kutokana na tabia ya binadamu ya kutaka mabadiliko.


Mathalani, kuna familia zenye wazazi wanaohakikisha watoto wao wanakula nyama na samaki siku zote saba za wiki. Imetokea mara kadhaa watoto au wanafamilia wakawachukia baba/mama kwa sababu tu ya kulishwa nyama, samaki na wali kila siku kwa wiki nzima! Wapo watoto waliogoma kula nyama kwa sababu wanafanya hivyo kila siku.

 

Wanagoma kula samaki si kwa sababu samaki hawafai, bali wamewachoka! Wanagoma kula wali na kutaka ugali au makande, si kwa sababu wali ni mbaya, bali wanataka kubadili mlo. Wana hamu ya kula chakula tofauti.


Vivyo hivyo, watu wanaichukia CCM si kwa sababu haiwaongozi vizuri, bali ni kwa sababu watu wamechoka kusikia chama tawala kimoja tu.

 

Watoto wanazaliwa, waanza shule, wanahitimu, wanafanya kazi, wanaoa au kuolewa, masikioni mwao ni CCM tu. Hili hawalitaki.


Kama kilivyo chakula kizuri, Serikali ya CCM imejitahidi kujenga barabara zinazoonekana. Imejenga Chuo Kikuu Dodoma cha mfano katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Inajitahidi kusambaza huduma za jamii na kadhalika, lakini pamoja na yote hayo, wananchi – kama walivyo wanafamilia waliolishwa chakula cha aina moja kwa muda mrefu – nao wamechoka! Wanataka wabadilishiwe chakula.


Ukiweka sababu hiyo ya kuwapo madarakani kwa muda mrefu, ukachanganya na hii sanaa ya uendeshaji chama ilivyo, mwangwi wa mabadiliko unasambaa kila kona.

Mwangwi huu, hata kama hauwanyimi raha Mwenyekiti Rais Kikwete na wenzake – inawezekana, si leo wala kesho – lakini keshokutwa athari zake zikaonekana.

 

CCM inajimaliza yenyewe. Wakati mwingine inakuwa vigumu kujua ni sababu gani hasa inayoifanya CCM ichungulie kaburi haraka namna hii! Hapo awali nimesema kwamba wananchi, kama walivyo watoto au wanafamilia, wanahitaji kubadilishiwa chakula. Shida yao ni kubadilishiwa chakula hata kama mpishi au wapishi watabaki wale wale.


Kwenye wapishi wale wale ndipo hapo tunapoona kile kilichotokea muda mfupi baada ya Rais Kikwete kuvunja Baraza la Mawaziri na kuliunda upya. Baraza jipya lililoundwa ni la wafuasi wa CCM. Je, mambo gani yamejitokeza baada ya Baraza jipya kuanza kazi?

 

Tumeshuhudia namna Wizara ya Nishati na Madini ilivyokuja na mikakati yake, tumeshuhudia namna Wizara ya Uchukuzi ilivyochukua hatua na Wizara ya Maliasili na Utalii ilivyofanya kazi iliyowavutia wengi nk. Mawaziri sasa wanaonekana walau kuchukua uamuzi mgumu. Wananchi wamejitokeza kuwapongeza kwa dhati kabisa viongozi hawa. Matumaini yao yamerejeshwa.


Tunachojifunza hapa ni kwamba pamoja na ukweli kwamba mpishi (CCM) ni yule yule, kumbe kiu ya wananchi hawa ni aina ya chakula.


Hawajali sana aina ya mpishi. Ndiyo maana nilidhani kwamba Mwenyekiti Kikwete angetumia busara zaidi ya kuwapata kina Deo Filikujombe, Nimrod Mkono na Kangi Lugola wengi.

 

Wabunge hawa ndiyo pekee kutoka CCM waliosaini karatasi maalumu yenye kusudio la kukusanya saini kwa ajili ya kumwajibisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Ushiriki wao uliwezesha Rais Kikwete “kusalimu amri” na kuamua kubadili Baraza la Mawaziri.

 

Tena basi, huu haukuwa uamuzi wa wabunge hao watatu tu, bali hata Kamati za Kudumu za Bunge nyingi zilitoa mapendekezo ya kuwang’oa mawaziri na watendaji walioshindwa kazi. Kweli, baada ya mabadiliko kufanywa sasa walau kuna mambo yanaonekana kwenda vizuri.


Msimamo wa wabunge hawa si wao tu, bali ni wa wabunge wengi. Kama Rais Kikwete angekuwa mbishi na kuruhusu kura ya maoni ipigwe bungeni, ni wazi kwamba Serikali ingeangushwa.


Ikumbukwe kuwa kura inayopigwa ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ni ya siri.

Sisi tulio karibu na wabunge wa CCM kutokana na kazi zetu, tulikuwa na imani isiyo shaka kuwa kama kura zingepigwa Serikali ingeangushwa. Hii ina maana kwamba wabunge wengi wa CCM nao ni kama wenzao wa upinzani – hawaridhishwi na mambo mengi yanavyoendeshwa ndani ya Serikali.

 

Kilichofanywa na Filikunjombe, Mkono na Lugola ni ujasiri tu. Hawa hawana mishipa ya unafiki au woga. Wanatekeleza kile wanachokiamini. Waliapa kuwatumikia wananchi na nchi yao. Kwao wao, nchi ni zaidi ya CCM.

 

Kwa imani hiyo, hawakuwa tayari kuwa wanafiki wa kulalamikia pembeni. Waliweka wazi msimamo wao ili wapigakura na Watanzania wajue. Dhamira yao ilikuwa kuona ile kauli ya “kuwatumikia wananchi”, inatekelezwa kwa vitendo. Hawa ni jasiri.

 

Kinyume cha matarajio ya wapenda maendeleo wengi, Filikunjombe, Mkono na watu kama kina Lembeli walioshupalia mabadiliko ndani ya Serikali ya chama chao, wameonekana wasaliti. Wameadhibiwa kwa kunyimwa fursa ya kugombea uongozi.


Kibaya zaidi, watu hawa wametoa kauli za kuendelea kuwa watiifu kwa CCM. Haya ni maneno tu ya kisiasa. Wamekataa kwenda Chadema kama walivyoaswa na Mwenyekiti wao.

Kwa anayejua masuala ya vita, hii ni hatari ndani ya CCM. Kuwa na watu ndani ya chama msiokubaliana kuhusu mwenendo na utendaji kazi wenu, ni hatari.


Hii ni sawa na “gorilla war”. Vita ya kumtambua adui ni nani na yupo wapi, ni nzuri na ushindi wake huwa dhahiri. Ndani ya CCM kuna “gorilla war” inaendelea na kwa kweli hawa walioamua kubaki humo watakuwa na kila sababu ya kuhakikisha wanaleta mabadiliko!

 

Tulichojifunza kwenye mchujo huu wa vikao vya CCM, ni kwamba kusema ukweli ndani ya chama hicho kwa sasa ni jambo lisilotakiwa. Mwanachama mzuri ni yule aliye tayari kuwa mwongo, mnafiki, mzandiki na anayemfurahisha Mwenyekiti hata kama ndani ya nafsi yake anajua anachokifanya ni usanii tu.


Kwa kuwa Mwenyekiti ametamka wale tunaosema CCM inakufa, tutakufa kabla ya CCM kufa, basi tusubiri. Lakini wanazuoni walihitimisha kwa kusema, “Hakuna kisichobadilika isipokuwa mabadiliko tu”.


Na kwamba, “Kama unajua uendako huwezi kupotea.” Kama unajua wapi unakokwenda utasemaje umepotea? Utakuwa umepotea pale tu utakapokuwa hujui wapi unakopaswa kwenda au kufika.


Kama CCM haijui kuwa inakufa sasa itasemaje kwamba inakaribia kukata roho? Ni suala la kusubiri na kuona!

1216 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!