Maelekezo/Maagizo ya Nyalandu

 

Nyalandu aliwaambia Wakurugenzi -Profesa Songorwa na Profesa Kideghesho kuwa yeye anamfahamu mmliki wa FCF; na ni marafiki. Lakini kubwa ni historia ya kampuni zake katika tasnia ya uwindaji wa kitalii na mchango mkubwa katika uhifadhi na maendeleo ya jamii. Alishauri kuwa si vizuri kuwa ‘rigid’ pale wadau kama hao wanapohitaji msaada. Hivyo, alimtaka Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori atoe ‘user rights’ kwa Kampuni ya Mwiba Holdings haraka iwezekanavyo kama walivyoomba.

Nyalandu alielezwa wazi kuwa utekelezaji wa maelekezo yake ulikuwa mgumu kwa sababu zifuatazo:

*Maelekezo haya yalikuwa yanataka wakurugenzi wakiuke sheria. Alikumbushwa kwamba hamna Kampuni yenye kinga inapokuja kwenye suala la kufuata sheria;

*Kanuni tayari zilisharejeshwa wizarani kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hivyo, hapakuwa na sababu kwa nini wahusika wasifanye subira kwani zingesainiwa wakati wowote na Waziri wa Maliasili na Utalii na kuanza kutumika.

*Tayari wahusika waliwasilisha ombi kama hili kwa Waziri wa Maliasili na Utalii (Kaghasheki), na kujibiwa kuwa wasubiri Kanuni zitoke kwanza ili waweze kufikiriwa kwa mujibu wa taratibu zote za uanzishwaji wa Ranchi za Wanyamapori. Hivyo, hatua yoyote ya kuruhusu uwindaji na shughuli nyingine kwa kipindi hiki si kwamba tu ingekuwa kukiuka sheria, bali pia ingekuwa dharau kwa kutenda kinyume na maelekezo ya Waziri wa Maliasili na Utalii.

*Mwiba Holdings si Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii. Hivyo, kuwapa haki ya kuwinda kunafuata sheria ipi?

*FCF wana ugomvi na kampuni nyingine na tayari kesi kadhaa zilikuwa mahakamani. Kitendo chochote cha kutenda kinyume cha taratibu kingeleta hisia kuwa Idara/Wizara imenunuliwa na Kampuni hiyo na kuifanya Wizara/Idara ipoteze heshima (credibility) mbele ya jamii.

Nyalandu alionyesha kushinikiza kuwa hilo lifanyike badala ya kuendelea kuwachelewesha wadau hawa muhimu! Nyalandu alishauriwa, kwa kuwa Kanuni zilikuwa zinasubiri saini ya Waziri, basi ingekuwa busara endapo angemuona bosi wake halafu amuombe azisaini mapema. Aidha, Mkurugenzi alimuomba aweke maelekezo yake kwenye maandishi kwa ajili ya kumbukumbu. Baada ya hapo alisema kuwa angefuatilia suala hili na kuona namna nzuri ya kulitafutia ufumbuzi, japo alionyesha kutokufurahishwa na msimamo wa wakurugenzi Kideghesho na Songorwa.

 

Uharaka wa FCF/Mwiba Holdings kutaka ‘user rights’ ulitokana na nini?

Pamoja na shinikizo la kuhakikisha kuwa bosi wao anapata eneo la kuwinda kama ambavyo amezoea, menejimenti ya FCF ilishapata habari kuwa eneo lao halikidhi vigezo na wasingeweza kukidhi masharti yaliyoko katika Kanuni za Uanzishwaji wa Ranchi ya Wanyamapori.

Hii ni kutokana na uwezekano wa kuwapo watu wasio waadilifu ndani ya Idara/Wizara ambao wanawapatia FCF taarifa zote zinazoendelea ndani ya Wizara zikiwamo baadhi ya nyaraka.

FCF walijua kuwa kama wangepata haki ya matumizi kabla ya Kanuni kutoka, ingewasaidia kuendelea kulitumia eneo hilo kama walivyotaka kwa kuwa kanuni zisingewabana. Kanuni/masharti yaliyoonekana kuwa kikwazo ni pamoja na yale yanayotaka:

*Ranchi ya Wanyamapori iwe angalau umbali wa kilometa 20 kutoka kwenye maeneo kiini yaliyohifadhiwa (core protected areas). Eneo la Mwiba linapakana (kilometa sifuri) na Eneo la Hifadhi la Ngorongoro, Pori la Akiba la Maswa na Hifadhi ya Jamii ya Makao (WMA).

*Itolewe taarifa ya kila robo mwaka inayoonyesha idadi ya wanyama waliozaliwa na waliokufa/kuvunwa. Hili lisingewezekana kwani eneo hili ni ushoroba (mapitio ya wanyama) na eneo la mtawanyiko kwa wanyamapori. Kimsingi, hata ile dhana ya uzalishaji wa wanyamapori haipo na si rahisi kusema wanyama wangapi wamevunwa/kufa au kuongezeka.

*Wanyama wanaozaliwa kutokana na ‘parent stock’ wawekwe alama. Hili pia lisingewezekana kwa sababu hata kuwatambua hao parent stock si rahisi kutokana na eneo hili kuwa mapito na eneo la mapumziko kwa wanyamapori tu. Kimsingi, Mwiba walitaka kupewa ushoroba, lakini si kuanzisha ranchi!

 

 Hitimisho

 Kwa maelezo hayo hapo juu, ni wazi kuwa Mwiba Ranch imeanzishwa kimagumashi. Haikidhi vigezo vya kuwa ranchi ya wanyamapori, bali imesukumwa na nguvu za ufisadi. Tambo za kampuni za Friedkin kuwa wana uwezo wa kuamua nani awe Mkurugenzi au Waziri zilisadifu. Mara tu baada ya Nyalandu kupata uwaziri kutokana na kujiuzulu kwa Balozi Kagasheki, wakurugenzi wawili waliokuwa na ujasiri wa kugomea ukiukaji wa sheria kwa manufaa ya Kampuni hizo pamoja na Nyalandu mwenyewe waling’olewa kutoka katika nafasi zao huku Lembeli akimpongeza Nyalandu kupitia vyombo vya habari na kumtaka ahakikishe kuwa Katibu Mkuu, Mama Tarishi naye anafungasha virago!

Ugomvi wa Lembeli na Mama Tarishi ulitokana na msimamo wa kijasiri wa huyu mama kukataa shinikizo la Waziri juu ya pendekezo la kumteua Lembeli kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori (TWPF) na Bodi ya TANAPA. Huko Lembeli alijua atafaidi mamilioni ya fedha. Ikumbukwe anayeteua Mwenyekiti ni Rais, lakini mapendekezo ya majina hutoka wizarani.

Hoja ya Mama Tarishi ilikuwa kwamba kufanya hivyo kungesababisha mgongano wa maslahi kwa kuwa tayari Lembeli alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ambayo kisheria inatakiwa kusimamia taasisi hizo.

Naamini kuwa mpango wa Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa wa utumbuaji majipu hautaishia kwa wale waliobaki ofisini tu. Kuna watu kama kina Nyalandu na washirika wake ambao wameiumiza sana nchi hii, japo hawako wizarani leo.  Wametumia vibaya madaraka yao kujinufaisha na kufanya kila aina ya uchafu. Wamewadhulumu Watanzania wenzao kwa kutumia kofia zao za uwaziri, ukuu wa wilaya, uenyekiti wa kamati na uwaziri kivuli. Ni wakati sahihi majipu haya yatumbuliwe kwani yameiva. Ni lazima wawajibike kwa madhambi yao. Huu ndiyo ukweli kuhusu hawa Mwiba Holdings.

 

>>TAMATI>>

By Jamhuri