Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) liko tayari wakati wowote kuchangia uboreshaji wa shughuli za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), amesema Mkurugenzi wa mpango huo, Helen Clark.

Shughuli zinazolengwa na UNDP kwa upande wa NEC na ZEC ni matumizi ya teknolojia na mashine za kisasa wakati wa Uchaguzi Mkuu mwakani, na katika TANAPA ni mapambano dhidi ya ujangili unaohusisha mauaji ya tembo.

“Uamuzi umeshachukuliwa kuhusu mfumo huo wa NEC na ZEC [mashine za kisasa zitakazohusisha uchukuaji wa alama za vidole], kinachotakiwa sasa ni utekelezaji,” amesema Clark aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa New Zealand.

Kiongozi huyo wa UNDP alikuwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita.

“Tuko tayari kuisaidia Tanzania teknolojia inayoitaka,” alisema Clark na kuongeza kuwa washirika wa UNDP watatoa dola milioni 22 za Marekani (sawa na Sh bilioni 35 za Tanzania) kuchangia gharama za mchakato wa Uchaguzi Mkuu ujao.

Katika hotuba yake ya mapitio na mwelekeo wa shughuli za Serikali, aliyoiwasilisha bungeni hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda, alisema NEC inajiandaa kupata vifaa vya kisasa vitakavyotumiwa katika uchaguzi huo.

Kuhusu uhifadhi wa wanyamapori na utalii Tanzania, Clark amesema jitihada zaidi zinahitajika kuwezesha ulinzi na uboreshaji wa sekta hiyo kwani ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.

“Lazima tuelewe kwamba uhai wa wanyamapori maana yake ni uhai wa utalii Tanzania,” alisema Clark.

Kwa mujibu wa Clark, UNDP inaendelea kufanya kazi kwa karibu na TANAPA kuhakikisha kwamba changamoto zote zinazolikabili shirika hilo la umma zinapatiwa ufumbuzi.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi huyo wa UNDP alitumia nafasi hiyo pia kuwashauri wanachama wa unaoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kukubali kurejea kushirikiana na wajumbe wengine wa Bunge Maalum la Katiba kujadili upatikanaji wa Katiba mpya.

UKAWA unaundwa na wanachama wa vyama vya siasa vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi. Kiongozi wa umoja huo, Profesa Ibrahim Lipumba, alitaja sababu za kususia vikao vya bunge hilo kuwa ni pamoja na kuchoka kudharauliwa na kusikiliza hoja za wajumbe wanaotaka muundo wa serikali mbili kinyume cha mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji (mstaafu) Joseph Warioba.

Katika ziara ya hapa nchini, Clark aliyefuatana na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Philippe Poisont, Naibu Mkurugenzi, Titus Osundina, na Mkurugenzi wa Utawala wa mpango huo, Steve Lee, alipata fursa ya mazungumzo maalum na Rais Jakaya Kikwete na kuzuru Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (RUNAPA).

1287 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!