Home Kitaifa Unyayasaji kingono washika kasi Kilimanjaro

Unyayasaji kingono washika kasi Kilimanjaro

by Jamhuri

Matukio ya watoto  kunyanyaswa kingono katika mji wa Moshi, yameibuka kwa kasi ya kutisha  na kutishia usalama wa watoto, huku wengi wao wakiwa ni wanafunzi wa shule za msingi.

Udhalilishaji huo unatokea huku wazazi wakitupiwa lawama kwa kushindwa kutoa ushirikiano vya vyombo vya dola watoto wao wanapofanyiwa ukatili wa kijinsia, ikiwamo kubakwa na kulawitiwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya mashirika ya kupambana na unyanyasaji wa kijinsia mkoani Kilimanjaro, wanafunzi 67 kutoka shule 14 za Manispaa ya Moshi wamegundulika kufanyiwa ukatili ikiwamo kubakwa na kulawitiwa kati ya Januari hadi Oktoba, mwaka huu.

Akitoa taarifa katika uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wiki iliyopita, Ofisa haki za binadamu na jinsia kutoka shirika lisilo la kiserikali la KWIECO, Elizabert Mushi, anasema  bado  mtoto hapati haki ya kujisikia kama kiumbe chenye haki.

Ulevi wa pombe na utumiaji wa dawa za kulevya kama bangi na mirungi, na uelewa mdogo wa jamii katika kuchukua hatua  watoto wao wanapofanyiwa vitendo viovu, ni moja ya sababu za ongezeko la unyanyasaji wa watoto kingono katika mji wa Moshi.

Mushi, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya siku 126 zakupinga ukatili kanda ya kaskazini, anasema wapo  baadhi ya wazazi wamekuwa wakidiriki kupokea mahari kama njia ya kupambana na umaskini na kuoza watoto katika umri mdogo bila woga.

Anasema, Oktoba, watoto 50 wenye umri kati ya miaka minane na 12 walibainika kufanya mapenzi na watu wazima na baada ya kufanyiwa vipimo vya afya, 20 walibainika kuambukizwa magonjwa ya zinaa yakiwamo maambukizi ya Ukimwi.

Wengi wa watoto hao ni wanafunzi wa shule ya msingi Kaloleni na baadhi yao hasa wa kiume wamebainika kulawitiwa na watu wazima huku watoto wa kike wakinajisiwa   kwa kufanyishwa  mapenzi na watu wazima kwa ujira wa Sh. 500 hadi Sh. 1000.

Chimbuko la maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, ni mauaji ya wasichana wa Mirabelle nchini Dominica mwaka 1960 na mwaka 1991 Umoja wa Mataifa ukaichagua Novemba 25 kuwa siku ya kimataifa ya kupinga ukatili huo.

“Kwa makusudi hayo Umoja wa Mataifa ulitenga siku 16 ikiwa ni Novemba 25, ambayo ni siku ya ya tamko kupinga unyanyasaji dhidi ya wanawake na Desemba 10  ni siku ya tamko rasmi la haki za binadamu ikiwa ni ishara ya kuhusisha ukatili kama huu wa haki za binadamu,” anasema mratibu huyo.

Kwa kanda ya Kaskazini, maadhimisho hayo yanaratibiwa na shirika lisilo la kiserikali la haki za binadamu na jinsia mkoani Kilimanjaro (KWIECO) na wadau wengine wa masuala ya haki za binadamu, jinsia na maendeleo ambao ni pamoja na NAFGEM, AJISO, shule kuu ya Polisi Moshi (MPS), Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mawenzi.

Wadau wengine ni Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF Net), Kikundi cha Wanawake mkoani Kilimanjaro cha kupambana na Ukimwi (KIWAKKUKI), Jeshi la Polisi nchini, Ofisi ya Elimu Mkoa, WOLEA Tanga, sekta ya habari na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

Athari za unyanyasaji huo wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto zinatajwa kuathiri afya za wahanga wa matukio hayo kimwili na kisaikolojia, na hivyo kusababisha kudidimiza maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Maadhimisho hayo ambayo kwa kanda ya kaskazini yamefanyika katika viwanja vya stendi kuu ya mabasi mjini Moshi, yanatumika pia katika kuweka mikakati ya   kutoa taarifa na kufuatilia matukio na kuchukua hatua za kisheria kwa wote wanaohusika na ukatili huo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadick, aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, alionya tabia ya wazazi kutochukua hatua kwa watu wanaohusika kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji watoto wao.

Alisema kuwa wazazi hawana budi kushirikiana na vyombo vya dola kuwafichua wahusika wanaofanya vitendo hivyo badala ya kutumia majani aina ya masale kumalizana na wazazi wa watoto waliofanya unyama huo.

Alidai kuwa unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake umekuwa ukiwaathiri pia hata katika upatikanaji wa ajira, licha ya kuwa na sifa lakini mila kandamizi zimekuwa zikiwanyima fursa ya kupata kazi, na kupongeza hatua ya Rais John Magufuli kuwapa nafasi wanawake wengi katika utawala wake.

Akizungumzia mimba za utotoni, mkuu wa mkoa alisema kuwa zaidi ya wanafunzi 231 wa shule za sekondari katika Mkoa wa Kilimanjaro wameachishwa masomo baada ya kubainika kuwa na ujauzito huku akiwanyooshea kidole waendesha bodaboda kwa kuwapa mimba wanafunzi.

Alisema matukio hayo yametokea kati ya Januari na Oktoba mwaka huu, huku mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi zikiwa tisa na mimba 222 ni kwa wanafunzi wa shule za sekondari. Ameonya kuwa matukio hayo yanaathiri maisha ya wanafunzi hao.

“Katika matukio hayo, wapo waliopewa mimba na waendesha bodaboda ambao hata pikipiki si za kwao, na wengine wamepewa mimba na ndugu zao na baadhi wamepewa mimba na wazazi wao wa kuwazaa na mpaka sasa tuna kesi tatu za wazazi kuwapa mimba watoto wao,” anasema.

Alitoa mwito kwa wazazi kujenga utamaduni wa kuwafuatilia watoto wao mashuleni na kujua mienendo yao huku akilitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina juu ya matukio ya wanawake na watoto kunyanyaswa kingono bila kuacha mwanya kwa Mahakama kuwaachia huru wahusika kwa kukosa ushahidi.

Utafiti wa shirika la International Center for Research on Woman (ICRW- 2010) unaonesha kuwa Tanzania ni moja ya nchi 20 duniani zinazoongoza kwa ndoa za utotoni kwa kuwa na asilimia 41.2 huku nchi ya Niger ikiongoza kwa nchi za Afrika kwa aslimia 74.5.

Kwa hapa nchini, utafiti unaonesha kuwa msichana mmoja miongoni mwa wasichana 20 amezaa mtoto akiwa na umri wa miaka 15 na takwimu huongezeka kwa kasi na kufikia msichana mmoja kati ya wanne wenye umri wa miaka 17.

Takwimu za Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro zinaonesha kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu kulikuwa na makosa 214 ya ubakaji, 51 ya kulawiti, matukio mawili ya kunajisi huku Mkoa wa Tanga ukiwa na matukio 26 ya kubaka, manane ya kulawiti, 28 shambulio la kimwili, 22 kutelekeza familia na mimba za utotoni 23.

You may also like