Naikumbuka vyema Jumamosi ya Mei 30,1969 nilipohudhuria Sherehe za Vijana wa Tanzania zilizofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Upanga, Dar es Salaam na kuhutubiwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Sababu kuu zinazonifanya nikumbuke siku hiyo ni kwanza; kwa  ukereketwa wangu, nilivyokuwa kijana wa TANU ilinibidi kuhudhuria, pili, kumsikiliza Mwalimu Nyerere atawafunda nini walimu kutoka mikoa yote ya Tanzania kuhusu Azimio la Arusha na siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea. Sababu ya tatu ni lile somo lililotolewa na Mwalimu Nyerere kwa walimu wenzake kuhusu “Unyonge wa Mwafrika”.

Na hili ndilo hasa ninalokusudia kulizungumza kwa uchache wake, nikilinganisha na vijana wetu hapa nchini, wako vipi!

Katika sherehe zile, Mwalimu Nyerere, kama kawaida yake, hakuacha kuonesha tabasamu, kutoa maneno ya mzaha na hatimaye kusema kusudio lake la kuzungumza na walimu wenzake, vijana wake na wazee wake wa Dar es Salaam.

Hotuba ile ilikuwa ndefu lakini haikuwachosha watu kuisikiliza kutokana na utani, vijembe na vidokezo kwa wananchi, viongozi, wakoloni, walimu na vijana — vilivyotolewa na Mwalimu Nyerere. Ukweli vilitia mashamushamu na hisia.

Nakumbuka vijana wa TANU na nyimbo zao za kuhamasisha watu — Ee vijana, vijana, vijana vijana tayari. Kulitumikia Taifa Taifa Taifa, kulitumikia Taifa Taifa Tanzania. Naye Mzee Rashidi Siso, (marehemu sasa) na vicheko vyake  Hohohooi Pasua mzee.

Unyonge wa Mwafrika ni somo makini na pana katika uwanda wake kwa mtu yeyote anayetaka kulijua. Katika somo hilo, Mwalimu Nyerere alisema kuwa unyonge wetu ni wa aina mbili ambao unawasumbua Waafrika. Mwalimu alisema;

“Unyonge wa kwanza ulio mkubwa ni unyonge wa moyo; unyonge wa roho. Huu ni unyonge wetu sisi; babu zetu hawakuwa nao, na wala hawakuwa na sababu ya kuwa nao unyonge huo wa moyo.

“Huu ni unyonge wetu sisi vizazi vilivyokuja baada ya kukabiliana na mataifa mengine, na kuona jinsi mataifa hayo yalivyotutangulia. Babu zetu wakajitahiditahidi, lakini wakashindwa. Vizazi vilivyofuata vikapata maradhi ya unyonge mbaya sana wa roho; wa moyo.”

Uthibitisho wa kauli hiyo: Angalia wasanii wetu, waimbaji na waigizaji baadhi yao wanavyohusudu kuimba katika staili ya Kizungu, kucheza na kunengua Kizungu, na hata mavazi yao kwenye majukwaa ni ya Kizungu. Je, hatuoni na kusikia?

Hebu watazame waigizaji;  wacheza sinema miondoko yao, vitendo vyao, mavazi yao hata sehemu zao za kuigizia ni zile zenye sura na mazingira ya Kizungu, ingawa hadithi au stori ya mchezo wenyewe ina uhalisia wa nje ya Uzungu.

Watazame vijana wa kike wanavyopigana vikumbo madukani kununua nywele bandia zinazofanana na za Kizungu. Makopo ya dawa yenye kemikali kali zinapakwa miilini kuondoa rangi nyeusi ya Mwafrika na kuweka rangi nyeupe/nyekundu za Mzungu.

Usiishie hapo. Angalia utamaduni wa Uzunguni wa kijana wa kiume kuvaa hereni sikio moja; kuvaa suruali chini kabisa ya kiuno. Zaidi, vijana wa kike na kiume wanavyobusiana barabarani hadharani. Hizo picha na mapenzi mitandaoni ndiyo usiseme.

Unyonge huo hauishii kwa vijana tu; hata kwa watu wazima.  Hapa ndiyo unatia kichefuchefu. Mama mtu mzima ana watoto na wajukuu, kioo hakimtoki na makemikali hayamwishi kujisinga mwilini ili aendane na wakati katika kuponda maisha.

Mashavu yanachuma kunde na ngozi ya mwili inasinyaa, lakini bado anataka jina la Kizungu la “Sugar mammy” hataki kuitwa bibi au Bint Shomvi” Looh! Unyonge huo!  Hizi ni dhambi za duniani, sijui kwa Mungu zitakuwaje.

Unyonge wa moyo, unyonge wa roho una somo pana, haliishii kwa vijana na akina mama pekee, bali unagusa na akina baba na viongozi mbalimbali kwa kuangalia kauli na vitendo vyao ndani ya jamii yetu hii. Nitaeleza.

Hebu angalia Waafrika watumwa kutoka Afrika wanavyokataa kuitwa Waafrika bali waitwe Wanegro, lau kama wanakubali wana damu ya Uafrika.  Wajapani wanaotaka kuitwa Wazungu lau kama asili yao ni Uasia.

Ndugu zangu Wangazija, Wamatumbi hata Wandengereko baadhi yao wanapokataa kutambulika kama walivyo, watambulike ni Waarabu.

 

Itaendelea

 

0717/ 0787 – 113 542

1552 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!