Desturi ya kuweka nadhiri mwanzoni mwa mwaka ni desturi yenye chimbuko la desturi za kale za jamii za magharibi, na hata zile za bara Asia.

Inasemekana Wababeli, wakazi wa kale wa eneo ambalo sasa ni Iraq, walikuwa na desturi mwanzoni mwa kila mwaka ya kuahidi kurudisha mali walizoazima na kulipa madeni. Hali kadhalika, Warumi waliweka nadhiri mwanzoni mwa kila mwaka. Ni Wamarekani wa karne iliyopita ndiyo walikuza desturi hii, na sasa imesambaa kwa watu wengi duniani.

Siyo rahisi kusema moja kwa moja kuwa Waafrika hatukuwa na desturi hii, kwa kuwa hata maisha ya kale ya mwanadamu ya uwindaji yalihitaji kiwango fulani cha kupanga, na wakati wowote inapotokea mipango ya kujirudia rudia basi yamkini pia hujitokeza haja ya kuweka nadhiri.

Nia ya kuweka nadhiri ni moja tu: ni kuboresha tabia zetu ili yale ambayo hatukuyafanya tuyafanye, na yale ambayo hatukuyafanya vyema tuyaboreshe. Vilevile, ingawa tunazungumzia zaidi mtu binafsi kuweka nadhiri, huwezi kutenganisha mtu na shughuli anazofanya na ni kwa sababu hii basi suala la kubadilisha tabia binafsi linaambatana na suala la yeye kubadilisha namna anavyofanya shughuli zake.

Kwa lugha ya usimamiaji wa kutekeleza mipango, kuweka nadhiri ni hatua ya mwisho ya kutathmini yaliyopita, kuibua kasoro, na kuweka uamuzi wa kuepuka hizo kasoro katika kipindi kijacho. Haina haja ya kusisitiza umuhimu mkubwa wa kufanya hivi kwa kila mtu. Ni sawa na dereva wa masafa marefu anayefahamu vyema njia aliyopita kupanga, pale anaporudi njia ile ile, kuweka tahadhari ya kuepuka maeneo ambayo yatakwamisha kukamilisha safari yake. Akifuata vizuri malengo anayoweka mwanzo wa safari, basi anajihakikishia kufika anakoenda bila matatizo makubwa.

Na kama ulivyo ukweli kuwa kila binadamu anaishi ndani ya jamii ya mamilioni ya watu ambao wanaweza kuathirika na mwenendo wake mzuri au mbaya, basi kuweka nadhiri zinazotuongoza kwenye matendo chanya ni suala ambalo linalinda ustawi wa jamii pana inayotuzunguka. Nadhiri zetu binafsi za mwaka mpya zinaleta manufaa siyo kwetu tu, bali pia kwa wengine wengi.

 Maneno, ili mradi yanatoka kwenye kinywa chako, hayakugharimu pesa. Hayanunuliwi dukani. Maana yangu ni kuwa ni rahisi kuweka nia ya kufanya kitu kuliko kutimiza hilo lengo.

Kwa sababu hiyo, ahadi nyingi tunazojiwekea au kuwatangazia watu, huwa hazitimizwi. Sababu ziko nyingi lakini wachambuzi wanazungumzia sababu tatu kuu: kuweka nadhiri ambazo siyo bayana; kuweka nadhiri ambazo hazitekelezeki; na kutoweka nadhiri zetu ndani ya mfumo.

Unaponuwia kupunguza kuvuta sigara bila kusema kwa kiasi gani, hujaweka dhamira ambayo unaweza kuipima kwa ubayana wake. Wapo wale ambao wamefanikiwa kuacha kuvuta sigara mara moja, lakini ni jambo ambalo siyo rahisi kutimiza. Anayenuwia kuacha kuvuta sigara anaweza kujaribu kwa kupunguza kuvuta sigara, lakini dhamira hiyo, kwa mujibu wa wachambuzi, inapaswa kuambatana na ratiba inayoweka malengo ya siku, juma, mwezi, na kadhalika. Hizi ni hatua bayana.

Kuweka tu nia ya kuacha kufanya jambo fulani bila ya kuwa na ratiba inayopima kufikiwa malengo haisaidii kufikia malengo tunayojiwekea.

Kudhamiria kufanya jambo ambalo halitekelezeki ni njia nyingine ya kushindwa kutimiza malengo hata kabla ya kuanza. Mtu aliyekaa mwaka mzima bila kufanya mazoezi ya aina yoyote, hawezi kutegemea kufanikiwa kuanza kutembea kilomita tano kwa siku kwa sababu tu ni Mwaka Mpya. Tarehe 1 Januari haimbadilishi mtu. Kinachoweza kumbadilisha ni kuweka malengo ambayo ataweza kuyatekeleza, hatua kwa hatua.

Tunasema watoto wanatambaa kwanza, kabla ya kutembea. Na kuweka nadhiri ambazo zinatakelezeka inahitaji kupitia hatua ya kutambaa kabla ya kutembea, na hatimaye kukimbia. La sivyo, utalazimisha kutembea hizo kilomita tano tarehe 1 Januari, na hatutakusikia tena mpaka mwishoni mwa mwaka ukiweka nadhiri nyingine isiyotekelezeka.

Kuweka nadhiri ndani ya mfumo ni mbinu ya kutotegemea nia binafsi pekee katika kutimiza jambo, ila kuifunga ile nia ndani ya mfumo ambao siyo rahisi kuuepuka.

Mathalani, kusudio la kuongeza mazoezi ya kutembea kwa mguu linaweza kufanikiwa zaidi siyo kwa kutaja tu idadi ya kilomita za ziada, bali kwa kuanza kuamua kuteremka vituo kadhaa kabla ya kituo cha kazini na kutembea mwendo uliobaki, pamoja na kufanya hivyo hivyo wakati wa kurudi nyumbani, yaani kupanda basi katika kituo kilekile unachoshukia ukienda kazini. Kwa namna hii unakuwa umejijengea mfumo wa kutekeleza nadhiri ndani ya safari ya kwenda kazini na kurudi.

Narudia kuwa maneno hayanunuliwi, kwa hiyo ni kweli kuwa yote haya yanahitaji msukumo fulani wa yule anayeweka nadhiri kuweza kuyatimiza. Hata kushuka vituo viwili kabla ya sehemu ya kazi inahitaji kuweka nia.

Mwaka umepita, na mwingine unaanza. Siyo wote tutaweka nadhiri mpya, lakini kwa wale watakaoamua kufanya hivyo na kufanikiwa, bila shaka wataboresha maisha yao na wakati mwingine hata ya wale wanaowazunguka.

By Jamhuri