*Wasira,  Mwakyembe, January Makamba nao watajwa kundini

Mkutano Mkuu wa Nane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliomalizika mjini Dodoma wiki iliyopita, umetoa ishara ya baadhi ya wanachama wanaoweza kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kama mapokezi na kushangiliwa, ndani na nje ya ukumbi ni kigezo cha “mgombea urais mtarajiwa” kuanza kujulikana, basi miongoni mwa kundi hilo wamo wanasiasa Bernard Membe, Dk. John Magufuli, January Makamba, Edward Lowassa na Stephen Wasira.

 

Wakati wa uombaji kura nafasi za wajumbe 10 wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, wanasiasa walioshangiliwa zaidi walikuwa ni Wasira, Membe, January na Mwigulu Nchemba ambaye kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu CCM (Tanzania Bara).


Haikushangaza kuona kuwa kwenye matokeo, Wasira, January na Mwigulu wakipata kura nyingi, huku Membe naye akishika nafasi ya sita licha ya kupata upinzani mkali kutoka kwa kundi hasimu. Mashambulizi dhidi ya Membe yaliongozwa na Hussein Bashe ambaye ameshaweka hadharani msimamo wake kwamba yupo katika kambi ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.


Wakati Lowassa akiwa tayari ni mjumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Monduli, yeye alionekana kupokewa kwa shangwe na wana CCM wengi ndani na nje ya ukumbi wa mikutano. Kila alipokuwa, wanachama wengi walimfuata na kumshika mkono; ingawa hali hiyo pia inaweza kutafsiriwa kuwa ni kumpa pole kutokana na maradhi ya macho. Itakumbukwa kuwa siku chache kabla ya kuanza Mkutano Mkuu iliripotiwa kuwa mwanasiasa huyo alienda nchini Ujerumani kwa uchunguzi wa kawaida wa macho. Amekuwa akifanya hivyo kila baada ya miezi sita.


Lowassa anatajwa kuwa ndiye mwana CCM mwenye nguvu za kimtandao miongoni mwa wale wanaoutaka urais. Nguvu hizo zilithibitika wakati wa uchaguzi wa nafasi mbalimbali ndani ya CCM kwa wale wanaotajwa kuwa wafuasi wake kushinda kwa kishindo.


Tofauti na wana CCM wengine, Dk. Magufuli yeye si mjumbe wa NEC. Mara zote amebaki kuwa mwana CCM asiyetaka cheo chochote ndani ya chama, lakini akiwa anatumika kama “kiraka” kwenye Baraza la Mawaziri. Dk. Magufuli alionekana wazi kuwavuta wana CCM wengi kuanzia kwenye hotuba ya ufunguzi iliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete.


Rais Kikwete kila aliposema, “Dk. Magufuli atakuja kutoa maelezo”, ukumbi ulilipuka kwa shangwe.


Wakati wa uwasilishaji taarifa ya hali ya barabara na vivuko nchini ulipowadia, ukumbi ulizizima kwa shangwe na vifijo. Shangwe hizo zinaweza kuwa zinatokana na kukubalika kwake kama kiongozi makini na msimamizi wa sheria asiye na simile, au pia zilitokana na namna yake ya kukariri majina, urefu wa barabara na gharama za ujenzi wa miradi mbalimbali. Uwezo wake wa kukariri urefu, majina na gharama za ujenzi umekuwa ukiwaacha hoi, si wajumbe wa CCM pekee, bali hata wabunge na wananchi wengi wa kawaida.


Pamoja na kuwa na wafuasi wengi, Dk. Magufuli amekuwa akitajwa kama mmoja wa wana CCM wasiokuwa na makundi, sifa ambayo ilimsaidia Mzee Benjamin Mkapa kupitishwa na CCM kuwania urais mwaka 1995. Hata hivyo, yeye mwenyewe amekuwa msiri mno katika kuonesha msimamo wake kwenye suala la urais.


Aidha, Dk. Magufuli anatajwa kama kipenzi kikuu cha Mzee Mkapa, hata baada ya kustaafu. Mara zote Mkapa amemtambua Magufuli kama mwanawe. Sifa yake kuu ni kusimamia kazi anazopewa kwa ufanisi.


Waziri mwingine ambaye kama angekuwapo ukumbini Kizota angeweza kukonga nyoyo za wajumbe wengi ni Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe. Uamuzi wake wa kuvunja bodi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Kampuni ya Ndege (ATCL), pamoja na kusimamia na kuanzisha usafiri wa reli jijini Dar es Salaam, vinatajwa kama moja ya mitaji yake ya kisiasa. Mwakyembe amekuwa akitajwa kuwa miongoni mwa wana CCM wanaoweza kufaa kukiwakilisha chama hicho kwenyer Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hasa baada ya afya yake kuendelea kutengemaa kwa kasi.


Wasira ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), ni miongoni mwa wagombea wa u-NEC waliopokewa kwa shangwe mno na wajumbe. Shangwe na vifijo vya wajumbe vikatafsiriwa baadaye na kura za wajumbe wa Mkutano Mkuu kwani ndiye aliyeongoza kwa kupata kura zaidi ya 2,000.


Anajulikana kwa misimamo yake, na hasa pale anapoamua kwenda “mstari wa mbele” kukabiliana na hoja za vyama vya upinzani. Ana historia ya kuwa upande wa upinzani, kwani mwaka 1995 alishinda kiti cha ubunge Jimbo la Bunda mkoani Mara kupitia chama cha NCCR-Mageuzi.


Mahakama Kuu ilimvua ubunge baada ya kubainika dosari kwenye uchaguzi. Mlalamikaji alikuwa Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba. Baada ya kuukosa ubunge mambo yalimwendea kombo, na hakuchukua muda mrefu akaamua kurejea CCM.


Wasira anatajwa kama mmoja wa wana CCM wanaojiona kuwa na sifa za kuwania urais mwaka 2015 kupitia CCM. Mwenyewe amekuwa hakanushi. Mmoja wa wana CCM wanaotajwa kuwa karibu naye kuhakikisha anafanikiwa kuikwaa nafasi hiyo ni Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine. Nyangwine amekuwa akipinga hoja za baadhi ya wananchi wanaotaka Katiba iweke ukomo wa umri kwa wagombea urais. Kwa sasa Wasira ana umri wa miaka 67.


Nyota ya January inaendelea kung’ara. Akiwa na umri wa miaka 38, ameweza kuonekana kuwa ni tegemeo ndani ya chama hicho kwani kwenye kura za NEC alikuwa wa pili, nyuma ya Wasira.


1501 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!