Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amesema, tofauti na wanasiasa wengine, yeye akiutaka urais hatasubiri kuoteshwa. Amesema wakati wa kugombea urais ukiwadia, na kama akitaka kuwania nafasi hiyo, hakuna kizuizi kwake.

Sumaye ametoa msimamo huo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akieleza sababu zilizomfanya aangushwe kwenye uchaguzi wa ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara. Katika uchaguzi huo, Sumaye aliangushwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu.


Sumaye ambaye mwaka 2005 alikosa ridhaa ya CCM ya kuiwakisha katika uchaguzi wa rais, amesema kuangushwa kwake kwenye uchaguzi huo kulitokana na rushwa kubwa aliyoiita “rushwa ya mtandao”.


Amesema pamoja na kuukosa ujumbe wa NEC, hana kinyongo na wala hakusudii kukata rufaa katika ngazi za juu za chama. Badala yake, amesema hali hiyo imempa nguvu zaidi.


“Kuangushwa Hanang’ kumenipa nguvu zaidi. Nikitaka kugombea urais sipiti kwingine, nikitaka urais napita CCM. Nikitaka urais sasa ndiyo vizuri zaidi kwa sababu kama ningeingia humo (kwenye NEC) ingekuwa tabu. Huku nje ndiyo nzuri zaidi,” amesema.


Kuhusu msimamo wake wa kugombea urais, amesema, “Sijatangaza bado wala sitasubiri kuoteshwa kama wanavyosema wengine, nikiamua naendelea.” Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia ni Mbunge wa Mtama, Bernard Membe, ndiye amekuwa akitumia neno la “sijaoteshwa” kila anapoulizwa na waandishi wa habari endapo atawania urais mwaka 2015.


Kuhusu tatizo la rushwa, Sumaye amesema ni kubwa mno, si kwa Hanang’ pekee, bali nchi kote, hasa kwenye uchaguzi unaoendelea ndani ya CCM.


“Tujirekebishe kabla hawajasema basi…tusidhani tutafanya haya (kutoa rushwa) miaka nenda miaka rudi…wananchi watafika mahali watasema hapana,” ameonya.


Alipoulizwa mmiliki wa mtandao wa fedha uliomwangusha kwenye uchaguzi Hanang’, Sumaye amesema hajui nani aliyetoa fedha hizo, na akakanusha taarifa na miong’ono iliyosambaa kwamba zilitolewa na Waziri Mkuu wa zamani ambaye ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.


“Kama Lowassa alishirikiana hilo mimi sina uthibitisho alishiriki au hakushiriki, hilo mwulizeni mwenyewe,” amesema, lakini akasisitiza kuwa wanasiasa wenye mitandao nchi nzima kwa sasa ni wengi mno.


Pamoja na kukiri kuwa hali ya rushwa ndani ya CCM ni mbaya, amesisitiza kuwa hana mpango wa kukihama chama hicho, kwani kama suala ni kuhama, atakuwa anahama kila anakokwenda kwa sababu hakuna mahali au chama ambacho hakijaathiriwa na rushwa.


Alisema kama CCM ingezingatia dhana ya uvuaji gamba, bila shaka hatua hiyo ingeisaidia kuondokana na mitandao ya rushwa.


Alipoulizwa nafasi na utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika uchaguzi wa Hanang’ , na kama taasisi hiyo ilifanya kazi yake, Sumaye akajibu kwa swali, “Ninyi hapa (waandishi) wa magazeti, wa televisheni kama mnachukua habari, lakini kesho hakuna kitakachotangazwa au kuandikwa kwenye magazeti, mtakuwa mmetekeleza wajibu wanu?”

TAARIFA KAMILI YA SUMAYE

Kabla ya kuzungumza uchaguzi wenyewe ningependa nizingumzie mambo mawili, matatu.

Kwanza, ni baadhi ya taarifa zenu katika magazeti na labda hata katika vyombo vingine vya habari. Kuna gazeti limeandika, “Sumaye kupasua jipu Dar es Salaam”.

 

Na Gazeti jingine likaandika, “Sumaye…nitalipua bomu Jumapili”. Mimi sina jipu wala bomu la kupasua. Kama kulikuwa na bomu au jipu limeshapasuka na ninyi mnalijua. Gazeti jingine la Oktoba 3, 2012 limeandika, “Sumaye amtangazia vita Edward Lowassa”.

 

Tena ikaendelea kusema, “Ikiwa Lowassa atawania urais, Sumaye ataingia katika mpambano huo kukabiliana naye kwa njia yoyote ile. Hataki kusema ataingia kwa CCM au kwa chama gani, au mgombea binafsi”.


Taarifa hii yasemekana imepatikana kwa chanzo kilicho karibu sana na mimi na bahati nzuri hicho chanzo sikifahamu.

 

Hivyo kama chanzo hicho kipo, hizo ni hisia zake, siyo zangu. Mimi sijaongea na mtu yeyote mambo hayo wala nisingeweza kuyasema hayo kwa sababu kwanza sina uhasama na Mheshimiwa Lowassa, na pili nikiamua kugombea urais sitagombea kwa sababu ya mtu fulani, bali nitagombea kwa sababu ya NCHI NA WANANCHI WA TANZANIA.


Pili, kuna gazeti moja la Ijumaa Oktoba 5, 2012 likisema, “Sumaye ateta na Chadema”. Tatizo hapa siyo mtu kukutana na viongozi wa Chadema, bali kuwa habari hiyo siyo ya kweli maana mimi sijakutana na kiongozi yeyote wa Chadema wala chama chochote cha upinzani. Lakini nadhani tufikie kwenye ustaarabu kuwa vyama vya upinzani siyo maadui wala viongozi wao siyo maadui wa viongozi wa CCM.


Mimi ningekuwa nimekutana nao ningesema tu, mbona hata hao wengine wanaotafuta urais kwa udi na uvumba huwa wanakutana nao? Nasikitika sana kusema kuwa habari hii iliyotengenezwa kwa kusudi maalumu na picha yangu kuwekwa pamoja na Mheshimiwa Mbowe kana kwamba kweli tulikuwa kwenye mazungumzo, imebeba uvumi mzito kuwa kama nitaingia Chadema ikibidi nitashughulikiwa itakavyoonekana inafaa ili nisivuruge mipango ya watu fulani kuingia Ikulu.


Dawa siyo kushughulika na watu wanaokihama chama, bali tushughulikie yale yanayowahamisha kwenye chama chetu. Mimi ninamwomba Mwenyezi Mungu kuwa huu uwe ni uvumi usio na msingi tusije tukaiingiza nchi kwenye matatizo makubwa kuliko tunavyofikiri.

 

Mimi ni mwanachama mwaminifu wa CCM na nilishawahi kusema mimi siko CCM kwa ajili ya cheo na wala kukosa NEC na hasa kwa njia iliyotumika hakuninyimi usingizi wala hakunizuii kugombea urais kwa tiketi ya CCM endapo nitaamua kufanya hivyo.

 

Lakini nataka kukumbusha kuwa hata Baba wa Taifa na mwanzilishi wa chama hiki aliwahi kusema kama chama kikiacha misingi yake atakiacha. Chama si mama yake. Kilichomuudhi Mwalimu wakati huo, pamoja na mambo mengine ni hali ya rushwa katika uchaguzi wetu hivyo tusiandame watu, bali tuandame maovu.

Septemba 6, 2012 wakati nilipokuwa nafunga mafunzo ya waandishi wa habari viongozi nilitahadharisha sana juu ya waandishi kutumika vibaya hasa nyakati hizi za uchaguzi kwa masilahi ya watu binafsi badala ya masilahi ya umma au ya taaluma yenyewe. Sina uhakika maana gonjwa hilo halijaanza kuwakumba baadhi ya waandishi wetu. Napenda kwa sasa niamini kuwa labda haya yaliyotokea ni utaratibu wa kawaida wa wanahabari kuchokonoa habari, lakini msivuke mipaka mkajioteshea ndoto za uchokozi.

Hali ya Uchaguzi kwa jumla

Mambo yaliyotokea Hangang’ yametokea katika maeneo mengi nchini, tofauti labda ni viwango vya hayo yaliyotokea na sura za watu waliohusika.

 

Mimi nataka nizungumzie mambo hayo katika sura ya kitaifa kuliko kujibana katika eneo dogo wakati tatizo ni kubwa sana. Uchaguzi huu ulighubikwa na matumizi makubwa ya fedha za rushwa. Suala la rushwa katika nchi yetu na katika chama chetu siyo geni lakini sasa nahisi tatizo hili limeota mizizi na linazidi kuwa kubwa.

 

Mimi binafsi nilizungumzia tatizo hili mara kadhaa; kwa mfano Oktoba 10, 2010 nikiwa Same kama mgeni ramsi kwenye sherehe za kuwekwa wakfu Askofu nilisema, “Rushwa ni tatizo kubwa katika bara letu na katika nchi yetu pia. Inaonekana sasa hapa kwetu kuwa huwezi kushinda uchaguzi bila kuhonga wapiga kura.

 

Kwa maana nyingine unakuwa kiongozi si kwa sababu watu wanakupenda bali kwa sababu umewanunua. Kiongozi anayepatikana kwa njia ya rushwa yeye mwenyewe lazima ni mwizi na fisadi maana vinginevyo hizo fedha za kuhonga angezipata wapi? Kiongozi mtoa rushwa ni mali ya watu fulani yaani wale waliompa hizo fedha maana “mlipa fedha ndiye huchagua wimbo”.

 

Aidha, hawezi kuwatendea haki anaowawakilisha kwa sababu haoni tena japo macho anayo, hana huruma na wananchi kwa sababu kwake wananchi ni sawa tu na bidhaa za sokoni na akiwa madarakani kazi yake kubwa ni kutafuta fedha kwa ajili ya kuja kuwahonga wapigakura tena kwa kipindi kijacho. Maoni ya rushwa ni mengi, hatuwezi kuyaorodesha hapa”.


Julai 7, 2011 nikiwa mgeni rasmi katika sherehe za kuadhimisha miaka 35 ya CCM na miaka …ya kuanzishwa TANU mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, nilisema, “Rushwa ni adui wa haki. Kama ilivyo kwa mataifa mengi, rushwa ni tatizo kubwa katika nchi yetu na katika chama chetu. Rushwa haikuanza leo, ni gonjwa la siku nyingi, lakini nalo pia linaonekana kuota mizizi sana ambayo kama hatutakuwa na ujasiri wa kuikata, basi itaua chama chetu na hata nchi yetu.

 

Wananchi wanalalamika kununua haki zao katika kupata huduma mbalimbali katika ofisi za Serikali, hospitalini, mahakamani, barabarani na kadhalika. Lakini kuna rushwa moja ambayo watu huifurahia ambayo ni mbaya hata kuliko hizo nyingine, nayo ni rushwa nyakati za uchaguzi. Watu wameonekana kuuza mali zao na kugawa fedha kuwahonga viongozi na wapigakura ili kushinda nafasi mbalimbali katika chama au katika dola.

 

Nasema hii ni mbaya zaidi kwa sababu kiongozi anayetumia njia hii hawezi kuwa bora, bali ni dhaifu. Hatajali masilahi ya umma kwa sababu kawanunua, atajali zaidi masilahi yake na lazima yeye awe mla rushwa ili apate fedha za kununua tena kura kipindi kijacho. CCM lazima tukatae ovu hili na kulipiga vita kwa dhati”.


Narejea haya ili isionekane leo nazungumzia rushwa kwa sababu nimeshindwa katika uchaguzi wa NEC. Mapambano dhidi ya rushwa ni ajenda ya kudumu kwangu na nitaendelea nayo popote nitakapokuwapo.


Hivi leo tunavyoongea, hali ya rushwa wakati huu wa uchaguzi imekuwa mbaya zaidi. Katika uchaguzi wa kidemokrasia wapigakura humchagua mwakilishi wanayemtaka kwa sababu ya uwezo wake, yaani humchagua mwakilishi wao kwa ajili yao. Katika demokrasia iliyopondeka kwa rushwa, fedha huwachaguliwa watu mwakilishi kwa ajili ya waliotoa fedha. Wapigakura ni wapiga mihuri tu!


Hivi sasa hali imetoka kwenye mtu kuhonga ili achaguliwe katika eneo lake na badala yake kuna rushwa za kimtandao ambapo mtu hutoa fedha katika maeneo mbalimbali nchini ili watakaochaguliwa wawe wafuasi wake mbele ya safari atakapowahitaji katika safari za ndoto zake.

 

Watu wanaochaguliwa kwa utaratibu huu, utumishi wao na uaminifu wao siyo kwa wale waliopiga mhuri kuidhinisha zile kura alizopata, bali kwa fedha zilizonunua zile kura na hasa hasa kwa aliyetoa au waliotoa fedha. Tunakuwa wawakilishi wa mtu au watu na siyo umma. Naomba Watanzania wote, tuwe CCM au kwenye vyama vingine vya siasa, tupige vita hali mbaya inayodhihaki na kudhalilisha demokrasia na inayodhalilisha hata utu wa wananchi wetu wanaopiga kura.

Kuhusu uchaguzi Hanang’

Uchaguzi huo ulighubikwa na matumizi makubwa ya rushwa, vitisho vingi, uharamia wa kuhamisha wapigakura usiku na maovu mengineyo mengi. La msingi ni kuwa mimi sijakata na wala sitakata rufaa ya kupinga matokeo wala kupeleka malalamiko katika chama changu kwa sababu yaliyokuwa yanatendeka yalikuwa yanafahamikana hata vyombo vya habari vilitolea taarifa mara kadhaa. Narudia tena, mimi nitabaki mwanachama mwaminifu wa CCM.

Mwisho

Nchi nyingi hasa zenye demokrasia changa kama yetu zimeingia katika vurugu na kuhatarisha amani na utulivu nyakati za uchaguzi. Naomba Tanzania tusichafue historia yetu nzuri ya amani na utulivu kwa ajili ya uroho wa madaraka. Madaraka yatakuja tu kama wananchi wapigakura wanaona wewe ndiye utakayewafaa na wala usiwarubuni kwa fedha jambo lolote kwa kutumia vibaya nafasi ya umasikini wao.


Napenda nitambue kuwa haya ninayoyasema si matamu masikioni mwa baadhi yetu, lakini ni vema tukayasikiliza kwa makini na kuchukua hatua chanya ili yasilete madhara zaidi katika jamii na wala tusidiriki kuwanyamazisha wanaoyazungumzia kwa uwazi. Hawa wanatuonyesha tahadhari iliyoko mbele yetu kama Taifa.

MUNGU IBARIKI TANZANIA


1102 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!