Marekani imeishutumu Urusi kwa kukiuka hadharani mikataba iliyoafikiwa katika enzi za Vita
Baridi, kwa kuunda kile Rais wa Urusi, Vladimir Putin, alichokitaja kuwa kizazi kipya cha silaha
madhubuti.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeghadhabishwa na tamko la Putin na kusema
kuwa Rais huyo wa Urusi amethibitisha madai ambayo yamekuwako kwa muda mrefu kuhusu
mpango wake wa nyuklia.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Sarah Sanders, amesema kuwa Rais Putin amethibitisha kile
serikali ya Marekani imekuwa ikijua, ambacho Urusi imekuwa ikikana, na kuongeza kuwa Urusi
imekuwa ikiunda silaha za kuvuruga amani kwa muongo mmoja sasa.
Rais wa Marekani, Donald Trump, anafahamu kitisho kinachoikabili nchi yake na washirika
wake katika karne hii, hali ambayo imeendelea kuitisha nchi hiyo pamoja na washirika wake
ambao wamekuwa wakilalamikia hatua ya Urusi kuunda silaha hatari.
Katika siku za karibuni, Urusi imetangaza kuunda kombora jipya ambalo haliwezi
kushambuliwa kwa na silaha yoyote, au kutunguliwa na linaweza kufika pahala popote duniani
endapo pakihitajika kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa Rais Vladimir Putin alipokuwa akieleza sera zake muhimu za muhula wake
wa nne, taifa hilo linalotarajiwa kufanya uchaguzi mkuu katika siku 17 zijazo nchini humo,
amesema hiyo ni hatua kubwa na muhimu kwa taifa hilo.
Amesema kombora hilo halina uwezo wa kupaa juu sana, na ni vigumu kuonekana pia, lina
uwezo wa kubeba kichwa cha nyuklia na linaweza kufika mahala popote pale katika dunia hii
bila ya kizuizi.
Amesema njia linayofuata haiwezi kutabirika na adui na pia linaweza kukwepa vizuizi na
kimsingi haliwezi kuzuiwa na mifumo ya sasa ya kinga dhidi ya makombora na hata mifumo
inayotarajiwa kuundwa siku zijazo.
Wakati hayo yakiendelea, Rais Putin ameionya Marekani na washirika wake wa NATO kuwa
mipango na uamuzi wya kutaka kuivamia kijeshi nchi ya Korea Kaskazini yenye idadi ya watu
milioni 25 tu ni kuitia dunia nzima katika majanga ya kivita.
Korea Kaskazini ikiongozwa na Kim Jong Un, imekuwa ikitengeneza silaha za nyuklia kila
uchao kwa lengo la kujihami na wabaya wake ambao ni Marekani, Japan, Korea Kusini
zikiwamo na nchi za Ulaya kupitia umoja wao wa NATO.

By Jamhuri