Vyombo vya dola nchini, kwa mara nyingine vimeiaibisha nchi yetu kimataifa kwa kushindwa kudhibiti uvushaji wa shehena haramu ya meno ya tembo (ndovu) kwenda Dubai na hatimaye Hong Kong.

Tukio hilo limefichuliwa wiki iliyopita na maofisa wasimamizi wa Bandari ya Hong Kong waliokamata vipande zaidi ya 500 vya meno hayo vyenye thamani ya Sh bilioni 2.24, vilivyoingizwa visiwani humo kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

 

Meno haayo yalikutwa yakiwa yamechanganywa na mbegu za alizeti kwenye magunia 400 ndani ya kontena lililosafirishwa na meli kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Dubai kabla ya kuhamishiwa kwenye meli nyingine iliyolisafirisha kwenda Hong Kong.

 

Hili ni tukio la pili la shehena haramu za pembe za ndovu kukamatwa nje ya nchi zikitokea Bandari ya Dar es Salaam katika kipindi cha mwezi mmoja.

 

Itakumbukwa kwamba mwezi uliopita, maofisa wa Idara ya Forodha ya China walikamata shehena ya vipande 1,209 vya meno hayo vyenye thamani ya dola milioni 3.4 za Marekani kutoka Kenya na Tanzania.

 

Kama ilivyoelezwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, inasikitisha kuona nyara za Serikali zinakamatwa ughaibuni tena na maofisa wa mataifa mengine, hali inayoitia doa nchi yetu kutokana na udhaifu wa maofisa wa Bandari ya Dar es Salaam katika udhibiti wa shehena haramu.

 

Sisi JAMHURI tunasema hujuma hii ya maofisa wa TPA, Usalama wa Taifa, TRA na Polisi haivumiliki kwani inatia doa nchi yetu katika medani ya kimataifa.

 

Inashangaza kuona utoroshaji wa nyara za Serikali kwenda nje ya nchi kupitia Bandari ya Dar es Salaam unafanyika mbele ya maofisa usalama waliokabidhiwa dhamana ya kukagua na kudhibiti uovu wa aina hiyo kwa kutumia mashine za kisasa.

 

Tunaamini kuwa dawa thabiti ya kukomesha tatizo la kupitisha shehena haramu katika Bandari ya Dar es Salaam ni uongozi wa juu wa Serikali kufanya uamuzi mgumu wa kuwawajibisha kwa kuwafukuza kazi maofisa na watumishi wote walioruhusu hujuma hiyo.

 

Wahusika wanastahili kabisa adhabu ya kufukuzwa kazi na kushitakiwa mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi.

 

Tunatambua kuwa Tanzania haiwezi kufuta aibu na doa la udhaifu uliodhihirika bandarini hapo, lakini kitendo cha kuwawajibisha maofisa waliosababisha taswira hiyo kitasaidia kuimarisha udhibiti katika bandari zetu.

 

Wakati wa kulindana na kuoneana aibu katika masuala nyeti yanayobeba heshima ya nchi yetu hauna nafasi katika zama hizi za ukweli na uwazi, ushindani wa sayansi na teknolojia.

Kama adhabu kali halizitatolewa kwa wahujumu hawa, tembo na wanyamapori watamalizwa katika mbunga na hifadhi zetu nchini.

 

Tuna mambo mawili tunayopendekeza. Mosi, elimu ya uhifadhi lazima iendelee kutolewa kwa wananchi wote. Elimu hiyo iende pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii kutoa tuzo nono kwa watu wote wanaofanikisha kukamatwa kwa nyara.

 

Pili, Serikali itumie jukwaa la kimataifa kuhakikisha kuwa biashara ya nyara za aina hii zinakomeshwa. Kama soko la meno ya tembo na faru litakufa, ni wazi kwamba uuzaji wanyamapori wetu utakomeshwa. Kubwa zaidi, ni zawadi kwa wanaoumbua hujuma hizo hapa nchini, na adhabu kali kwa wote wanaobainika kujihusisha na uhujumu huo.

 

Mtandao wa uhalifu huu lazima usakwe na uteketezwe.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

1056 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!