Kwa sasa taifa limekuza vipaji vya usanii, hasa wa muziki. Vijana wamebuni muziki unaojulikana kama muziki wa kizazi kipya. Huu ni aina ya muziki ninaoweza kusema una mambo tofauti na muziki tuliokuwa nao miaka ya nyuma. Ni muziki unaokwenda kwa waimbaji kuimba tu bila ya kuwa na zana za muziki!

Wanatunga tu mashairi na kwenda kwa watu wanaoitwa “mapromota” hao ndio wanawatafutia midundo toka kwenye compyuta na kuichanganya na hayo mashairi, basi wao wanapanda kwenye majukwaa na kuonekana wanaimba.

Wakati zamani muziki uliopigwa ulikuwa unalenga zaidi kuburudisha tu wapenzi wa muziki ilhali wasanii wenyewe wakiwa hawaambulii chochote cha maana, kwa sasa wasanii wa muziki wanaonekana wanavyotengeneza pesa wakiwa hawaendani tofauti zaidi na wanamuziki wa nje.

Mfano tulikuwa tunamsikia mwanamuziki Michael Jackson wa Marekani alivyokuwa na pesa nyingi, tuseme alikuwa mwamuziki ghali kuliko wanamuziki wengi duniani. Lakini kikubwa ni kwamba alifikia mafanikio hayo kwa jitihada zake binafsi zilizotokana na ubunifu wake wenyewe.

Aliyoyafanya yanawashinda wengi hasa hapa kwetu. Yeye alikuwa ni muimbaji mwenye kipaji cha aina yake, aliyebuni namna ya kuimba na kucheza akiwa na sauti iliyomtambulisha mara moja kwamba huyo ni Michael Jackson. Pamoja na hayo akiongeza vituko vingine vingi vilivyomjengea utambulisho wa haraka na wa aina yake.

Sio kwamba kwetu hapa hawapo vijana wanaoweza kufikia kiwango chake, wapo ila wanachokikosa ni kitu kimoja tu, ubunifu wa cha kufanya ili waweze kujitambulisha kama wao.

Kwa mfano tunaye mwanamuziki kijana ambaye mafanikio yake ni makubwa sana kwa kiwango cha hapa nchini kwetu, Nasibu Abdul maarufu kama Diamond Platnumz. Ni kijana aliyetengeneza kipaji chake na kukikuza sana kiasi cha kuanza kutambuliwa kimataifa.

Ila kitu pekee ninachoona anakikosa ni uwezo wa kujitambulisha kama yeye linapokuja suala la kiwango alichokifikia. Anafikiri kwamba kuwa maarufu kwa ngazi ya kimataifa ni kuiga ambayo wengine waliofikia kiwango kama alichokifikia yeye waliyafanya!

Naona anajaribu kumuiga Michael Jackson kwa karibu kila kitu! Mfano mfalme yule wa Pop alipendelea kuvaa kofia ya pama, tayari Diamond anaivaa kofia ya aina hiyo, kuimba kwa kubanabana pua na madoido mengine jukwaani ni kama ya Michael Jackson!

Kibaya zaidi naona hata uvaaji kajaribu kuiga wa Jackson. Tuliona alipoitwa kutumbuiza kwenye tuzo ya mchezaji bora wa kandanda barani Afrika nchini Misri, vituko vingi jukwaani alikuwa akiiga vya Jackon. Shati alilovaa, hata kama kwa thamani halikufikia la Michael Jackon, lakini kimuonekano lilikuwa kama la Wako Jacko!

Naona wakati mwingine anavaa miwani ya jua kama alivyokuwa akifanya nguri huyo wa muziki duniani. Ila cha kumshauri Diamond ni kwamba alipaswa kuelewa kuwa Michael Jackson alikuwa kajiharibu sana maumbile yake kiasi ambacho hata yeye asingemshauri mtu mwingine amuige, sababu alikuwa amejiharibu sana. Kujihatarisha.

Si ajabu macho yake ambayo yalishafanyiwa upasuaji mara kadhaa kwa kutafuta urembo zaidi yalikuwa hayawezi kuhimili mwanga wa kawaida, ndiyo maana pengine akawa anavaa miwani ya giza hata kwenye giza!

Natumia nafasi hii kumshauri mdogo wangu Diamond asije akajaribu kufanya upasuaji wa sura yake akidhani ile nayo ni sehemu ya umaarufu wakati ilikuwa ni sehemu ya kujimaliza. Shida alizozipata Michael Jackson mpaka kufikia kifo chake ni kubwa sana, alijuta!

Kwa mfano pua yake ilikuwa ‘inanyofokanyofoka’ ovyo kutokana na upasuaji aliokuwa akifanyiwa mara kwa mara. Sidhani kama hilo ni jambo la heri ambalo mtu angetamani kuliiga.

Wapo wanamuziki wengi wa Afrika wanaopenda kuonekana kwa mitindo waliyoibuni wao wenyewe, mfano Joseph Mayanja wa Uganda, maarufu kama Chameleon. Nilipokutana naye mjini Mwanza mwaka 2015, nikapata nafasi ya kuongea naye kama robo saa alinieleza mambo mbalimbali zikiwemo changamoto anazokumbana nazo katika fani yake ya muziki.

Pamoja na kumpongeza kwa kutumia staili yake inayomtambulisha bila kupendelea kuiga staili za wengine, nilimuuliza kwa nini mtu kama yeye kwa kiwango alichofikia bado anapendelea kutumia kitu kinachoitwa “play back” yaani kuweka CD na kufuatisha kama anaimba kumbe inayoimba ni CD, yaani muziki ambao umerekodiwa.

Alinijibu kwamba inategemea aliyempa mwaliko anatakaje, sababu eti inakuwa sio rahisi mtu amuite kwa gharama ya kucheza ‘play back’ yeye abebe vyombo vya muziki na kuja navyo. Kwamba kwa namna hiyo ni kama atakuwa amekuja kuburudisha tu bila mategemeo ya faida yoyote. Niliona hoja, lakini kiukweli sijawahi kuona kama ana vyombo vyake mwenyewe.

Maana kuna kipindi nilimuona Kampala akitumbuiza kwa njia hiyo ya kufuatiliza CD wakati kule ndio kwao.

Hayo tuyaache, cha muhimu ni kwamba anapiga muziki unaojitambulisha kwamba ni wa nani. Akiwa jukwaani anatambulika wazi kuanzia uvaaji miondoko yake na kadhalika.

Hicho ndicho kitu ambacho ningependa kumhimiza Diamond kukifanya, kuwa yeye kama yeye bila kuigiliza miondoko ya wengine. Hilo ni jambo la kuzingatia. Hatutaki kumuona Diamond wa kubumba, tunataka kumuona Diamond mwenyewe akifanya vitu vyake visivyo na dalili zozote za kuiga. Na kwa namna hiyo ndipo tunaweza kumpata mbadala wa Michael Jackson kwa maana halisi.

[email protected]

0654031701

By Jamhuri