Unaweza kuwa wewe, ndugu yako, rafiki au  jamaa yako ameunganishwa katika kesi ya mauaji. Aghalabu, daktari anasubiriwa kutoa ushahidi mahakamani kuhusu sababu za kifo cha marehemu. Na ni ushahidi huo wa daktari utakaokuondoa katika kesi hiyo ya mauaji au utakuingiza katika kesi hiyo, hivyo kutiwa hatiani na kuadhibiwa.

Lakini si daktari tu, bali wenye kesi wote ambao ushahidi wake unahitaji mtaalamu (expert) kuthibitisha; mfano, mkemia, mtaalamu wa mwandiko na sahihi, mtaalamu wa biashara au mtaalamu wa DNA.

Ushahidi wa daktari

Kifungu chac 47 cha Sheria ya Ushahidi kinaruhusu kutumika na kukubalika kwa Ushahidi wa Mtaalamu (Expert). Mtaalamu ni pamoja na daktari.

Mambo 6 muhimu unayotakiwa kujua

(A) Kabla daktari au mtaalamu mwingine yeyote hajaanza kutoa ushahidi wake ni muhimu sana athibitishe kwa ushahidi kuwa yeye ni mtaalamu kweli (expert) kwa hicho anachotaka kutolea ushahidi. Usikubali akaanza kueleza kabla ya kuthibitisha utaalamu. Mtake athibitishe hilo kwanza.

Utaalamu unathibitishwa kwa taaluma (professional). Kama ni daktari na mtaalamu wa eneo fulani la tiba, mfano mifupa, moyo, nk, aonyeshe cheti cha taaluma katika eneo hilo. Halikadhalika kwa wataalamu wengine nao wanatakiwa kufanya hivyo. Kama hawezi kuthibitisha hilo, basi hiyo ni faida kwako, kwa kuwa ushahidi wake ni wa kutia shaka.

Na hapo haijalishi mtaalamu (expert) huyo ameletwa na nani. Awe ameletwa na polisi, PCCB, au idara nyingine yoyote. Msimamo huu ulitolewa na mahakama katika kesi ya MUHAMMED AHMED V REPUBLIC (1957) E.A. C.A 523.

(B) Daktari au shahidi yeyote mtaalamu, asiwe tu mtaalamu wa vyeti, bali awe mwenye ujuzi na uzoefu wa kazi husika. Kwa mfano, daktari au mtaalamu ambaye amemaliza chuo, ana cheti lakini hajaajiriwa wala kuwahi kuifanyia kazi taaluma yake popote, hawezi kuitwa mtaalamu mwenye uwezo (competence) wa kutoa ushahidi wa kitaalamu.

Hakikisha unahoji uzoefu katika taaluma husika (practice). Kama hana sifa hiyo, basi ni faida kwako, kwani ushahidi wake ni wa mashaka. Lakini ni baada yako kulihoji hili, ili liingie katika kumbukumbu za mahakama. Huu ni msimamo wa mahakama katika kesi ya GATHERU s/o NJAGWARA v R (1954) E.A.C.A 384.

(C) Hata kama kinachotolewa ushahidi kinajulikana kwa kila mtu, bado anayetakiwa kukitolea ushahidi ni mtaalamu.

Kwa mfano, katika kesi ya SALUM HARUNA v R (1968) HCD 37, askari alitoa ushahidi kuwa alichomkamata nacho mtuhumiwa ni bangi. Mahakama ya wilaya ilikubali ushahidi huo na kumtia hatiani. Kwenye rufaa mahakama ilibatilisha hatia hiyo na kusema kuwa askari ambaye si mtaalamu wa dawa za kulevya hawezi kuijua bangi.

Hivyo hakikisha si tu shahidi anakijua kitu hicho, bali pia ni mtaalamu wake (expert). Kama si mtaalamu, hata kama anakijua kitu hicho, bado hakijui mbele ya sheria. Ndiyo maana utaona polisi wanasema: “Kitu chenye ncha kali”, “kitu kigumu” nk. Wanajua ni panga au jiwe lakini hawasemi, kwa kuwa si wataalamu (expert) wa kusema hivyo.

(D) Mtaalamu asiseme kwa akili yake mwenyewe (personal knowledge),  bali aseme taaluma au sayansi inavyosema kuhusu jambo husika. Kwa mfano, asitumie maneno kama “mimi ninavyojua”, “ nionavyo mimi”, “ushauri wangu”, “nafikiri”, bali aseme “sayansi inasema hivi”, “ kitaalamu jambo hili liko hivi” nk. Huu ni msimamo katika kesi ya LONGINUS KOMBA v R (1973) LRT 39.

(E) Pia aeleze amefikiaje jibu lake (conclusion). Ni kama ilivyo kwenye hesabu ambapo si tu unatakiwa kuonyesha jibu, bali njia uliyotumia kufikia hilo jibu. Lengo ni hiyo njia ihojiwe kuona kama inaweza kuzaa jibu sahihi au la.

(F) Mahakama hailazimiki kukubaliana na ushahidi wa mtaalamu hata kama jaji au hakimu si mtaalamu wa hicho kitu kilichotolewa ushahidi.  Kwa hakimu au jaji, ushahidi wa mtaalamu (expert) ni maoni tu, si hukumu. Ataamua kuyabeba au kuyatupa. Ni msimamo wa mahakama katika kesi ya HASSAN SALUM v R (1964) E.A 126.

By Jamhuri