Hayati-Baba-wa-Taifa-Julias-K.-NyerereUshirikiano kati ya TANU na ASP uliongezaka uchaguzi wa Juni 1961 ulipokaribia. ASP ilifungua ofisi kwenye makao makuu ya TANU mwaka 1961. Thabit Kombo alisafiri Dar es Salaam mara kadhaa Aprili kuhakikisha kwamba ofisi ya ASP inafanya kazi Dar es Salaam. Vile vile, Kombo alikutana na viongozi wa TANU na kuomba msaada wa pesa na mawazo.

TANU ikakubali kutoa khanga 11,000 zenye rangi walizotaka ziwe kwenye bendera ya Tanganyika baada ya Uhuru. ASP ilipokea khanga na kuziuza kwa Sh 12, waliipa TANU Sh 10 kwa kila khanga waliyouza na kuchukua Sh 2 zilizobaki. ASP ilipata Sh 22,000 kwa kuuza hizo khanga. Pesa hizo zilitumika kwa uchaguzi.

TANU ilituma viongozi wake wanawake kwenda kuhamasisha ASP na wafuasi wake. Lucy Lameck na Bibi Titi Mohammed walienda Zanzibar mwaka 1961 na kutoa hotuba kuhamasisha wafuasi wa ASP. Hotuba ya Bibi Titi ilikuja kuzua gumzo na Abdulrahman Babu aliyekuwa mwanachama wa ZNP kipindi hicho, alilaani TANU kwa kuingilia siasa za Zanzibar.

Viongozi wengine wa TANU waliotoa hotuba Zanzibar ilikuwa ni pamoja na Saadan Abdulkadir Kandoro. Hizo hotuba za viongozi wa Bara zililenga kuijenga ASP ili ishinde uchaguzi.

Msaada wa pesa kutoka TANU uliendelea muda tofauti kabla ya uchaguzi. Saleh Sadalla na Aboud Jumbe walipewa Sh 6,000 na TANU. Ali Haloua wa TANU alitumwa Zanzibar na Sh 5,000 za ASP. Misaada hii ilitolewa na TANU kwa nia ya kusaidia ASP ipate ushindi.

TANU haikutoa ushauri wa pesa tu, baadhi ya viongozi wa Bara walishirikishwa kutoa ushauri kwenye baadhi ya uamuzi muhimu wa kisiasa ya ASP. Bibi Pili Bint Khamif, mke wa Jaha Ubwa Jaha wa ASP, alipewa kazi ya kutuma ujumbe kati ya TANU na ASP mnamo Juni, 1961. Bibi Pili alipeleka ujumbe Zanzibar kutoka kwa Mwalimu Nyerere kwamba wasusie Legislative Council mpaka serikali itapoacha kuwaonea Waafrika. Katika kipindi hicho, Othman Shariff alirekodiwa na ujumbe ukapazwa Radio Tanganyika. Shariff alisema kwamba polisi walikuwa wanakamata Waafrika bila sababu na kuwanyanyasa. Machafuko ya kisiasa na kile walichoona kuwa ni unyanyasaji wa ASP na wafuasi wake hata kabla ya uchaguzi, uliwafanya viongozi wa Bara kuzidisha msaada kwa ASP.

Vurugu zilitokea mwanzoni wa Juni 1961.  Wafuasi wa ASP na ZNP walishambuliana. Zaidi ya watu 60 walipoteza maisha; wengi waliumia, na zaidi ya watu 700 walikamatwa. Ripoti nyingi zilisema fujo zilianzishwa na wafuasi wa ASP. Moja ya chanzo cha fujo hizo walisema ilikuwa ni matatizo wakati wa kupiga kura.

Othman Shariff alizungumza Radio Tanganyika mwezi Juni na kusema kwamba polisi walikuwa wanatumia sheria za dharura kukamata Waafrika. Pia kulikuwa na ripoti kwamba wafanyakazi wenye asili ya Bara walikuwa wananyanyaswa. Shariff aliomba msaada wa wanasheria kusaidia kutetea wafuasi wa ASP mahakamani.

Tanganyika haikuwa nchi peke iliyotoa msaada kwa ASP mwaka 1961. ASP ilianza kupata msaada kutoka Ghana. Ghana ilituma mwanasheria Bartholomeo Kwawswanzy kusaidia ASP baada ya vurugu za uchaguzi wa Juni 1961. Othman Shariff na Kwawswanzy walienda kuonana na Mwalimu Nyerere mnamo Septemba 1961 kuomba ushauri. Mwalimu Nyerere aliwashauri wasilazimishe uchaguzi na wajaribu kuunda serikali ya umoja na ZNP/ZPPP kama ASP watapewa nafasi mbili za uwaziri. Shariff akarudi Zanzibar na kutoa ushauri wa Mwalimu Nyerere kwa ASP. ASP ikafanya maongezi na Shamte na walifuata ushauri wa Mwalimu Nyerere kwenye madai yao. Maongezi hayo hayakufanikiwa.

ZNP na ZPPP wakaunda serikali ya pamoja ikiwa na Shamte kama Waziri Mkuu mwishoni mwa Juni 1961. ASP ilitaka kuhakikisha watashinda uchaguzi ujao wa mwaka 1963. Walifanya mikutano mingi kuanzia mwaka 1962 kupanga mikakati ya uchaguzi. Mkutano mmoja ulifanyika Juni 1962. Viongozi wa ASP walikutana kujadili mapendekezo kuhusu uchaguzi na wafanye nini kama wakishindwa. Walijadili suala la kuunda serikali ya umoja na ZNP/ZPP kama wakishindwa. Pia walizungumzia uwezekano wa kufanya mapinduzi kama wakishindwa uchaguzi.

Mzee Karume na wengine walikubaliana kufanya serikali ya umoja kama wakishindwa; kundi hilo lilikuwa na watu wengi zaidi. Ilikuwa katika kipindi hiki, Ali Sultan aliwataarifu ASP kwamba yeye au Babu wapo tayari kupigania Jimbo la Darajani na kuungana na ASP.

Katika mkutano wa viongozi wa ASP, Othman alipendekeza kupindua serikali kama wakishindwa. Upande wa Karume ulikuwa na watu wengi zaidi nao walikataa pendekezo la mapinduzi. Shariff alikasirika na akaondoka Zanzibar kwenda kuzungumza na Mwalimu Nyerere. Alirudi na barua kutoka kwa Mwalimu Nyerere iliyoshauri ASP wasikubali kuunda serikali ya umoja na waweke nguvu zao zote kudai uchaguzi na kuushinda. Ushauri huu ulikubaliwa na uongozi wa ASP.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 1961, Ali Muhsin aliongeza mazungumzo ya sera za kupendelea “Zanzibari” zaidi ya watu wenye asili ya Bara. Katika mkutano mmoja baada ya uchaguzi na viongozi wa ZNP, Muhsin alisema mpango huo wa kupendelea “Wazanzibari” ni wa siri na hawakutakiwa kuuzungumza wazi. Sera za kubagua watu wenye asili ya Bara ilifanya viongozi wa Bara kuanza kufikiria njia nyingine za kusaidia ASP mwaka 1962.  Na kipindi hicho, Muhsin aliwaambia baadhi ya viongozi wa ZNP nia yake ya kudumisha uhusiano na Misri.

Serikali ya ZNP/ZPPP iliongeza uhusiano na serikali ya Misri mwanzoni wa mwaka 1961. Kama Tanganyika walikuwa wafadhili wakubwa wa ASP, Misri walikuwa mmoja wa wafadhili wakubwa wa ZNP/ZPPP. Mwanadiplomasia wa Misri, Abdulla el Chourbagni, alizuru Zanzibar Machi 1961. Alikutana na Ali Muhsin, Ahmed Seif Kharusi, na wanachama wengine wa ZNP. Chourbagni aliwaambia kwamba nia ya ziara yake ilikuwa kukipa nguvu chama cha ZNP. Alitangaza Misri itadhamini wanafunzi 24 kusoma nchini humo na kujenga Chuo cha Zanzibar. Na baadaye, Misri ikatoa pesa za kusaidia ZNP ishinde uchaguzi.

Ushirikiano kati ya TANU na ASP ulianza kuchukua picha mpya mwaka 1962. Kassim Hanga alianza kuwa karibu na viongozi wa Tanganyika aliporudi kutoka Urusi mnamo Desemba 1961. Hanga na Oscar Kambona walikuwa marafiki na walikaa pamoja walipokuwa wanafunzi Uingereza.

Hanga alisafiri Dar es Saalaam mwezi Machi 1962 na kukutana na viongozi wa TANU. Haikuchukua muda mrefu kwa Hanga kuungana na baadhi ya viongozi wa TANU, akiwemo Kambona. Hanga akapanda ndege baada ya mkutano na viongozi wa TANU akaenda Uingereza.

Mwaka 1962 ulikuwa ni wa viongozi wa ASP kwa ushirikiano na viongozi wa TANU waliongelea mipango mipya ya kuchukua serikali. Tanganyika tayari ilikuwa imepata uhuru na viongozi wa TANU walikuwa huru na tayari kutoa msaada wa aina yoyote uliohitajika. ASP ilianza kujitayarisha kwa uwezekano wa mapambano mwaka 1962.

 TANU ilikuwa mstari wa mbele kusaidia ASP katika kipindi hicho. Viongozi wa ASP- Karume, Thabit Kombo, Hasnu Makame, Mtoro Rehani -walikutana na Waziri Mkuu wa Tanganyika, Rashid Kawawa, Aprili 1962. Kawawa aliwashauri viongozi wa ASP waombe uchaguzi na kwamba TANU itawapa msaada wa pesa. Kawawa aliwashauri waingie kwenye uchaguzi na wakishinda wajiunge kwenye umoja wa Afrika Mashariki.

Karume, Kombo, Makame, na Rehani pia walikutana na Mwalimu Nyerere kwa ushauri zaidi. Mwalimu Nyerere, John Rupia, Karume na Kombo wakafanya mkutano mwingine wa pamoja baadaye.  Katika mkutano huo, Mwalimu Nyerere aliwaambia Kombo na Karume kwamba yupo tayari kuwasaidia kwa siri kama watajisaidia wenyewe. Kambona alionekana kushirikiana na viongozi wa ASP tangu mwaka 1962. 

 

>>ITAENDELEA…

 

Mwandishi wa makala hii, Azaria Mbughuni, ni Assistant Professor wa Historia katika Chuo Kikuu cha Lane, Tennessee, Marekani. Anapatikana kupitia barua pepe: azmbughuni@gmail.com

2603 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!