Nadhani kila anayesoma maneno haya hii leo, anaweza kuona jinsi Baba wa Taifa alivyodhamiria kujenga nchi ya watu wenye hali ya usawa katika kila nyanja.

Kwa upande wa wananchi nao walipokea mwito huo wa Baba wa Taifa nao wakachangamkia kusawazisha tofauti zilizorithiwa katika elimu, kwa nia ya sote kulelewa katika usawa kama Watanzania kwa namna mbalimbali.

 

Jumuiya za Waislamu katika mkutano wao wa kwanza (First Muslim Congress 1962) waliazimia kuanzisha Idara ya Elimu chini ya usimamizi wa East African Muslim Welfare Society na wakabuni mpango kabambe wa kujenga shule zao.


Tunasoma maneno kama haya; nanukuu, “Muslims did not wait for the Independent Government to start fulfilling its pre- independence promise of redressing educational disparity between them and Christians. Muslims initiated their own plans to complement government efforts (Mohamed Said – The Untold Story of the Muslim Struggle against British Colonialism in Tanganyika” uk. 26), na kweli shule zilianza kujengwa, mathalani shule za msingi kule Ilala, Kigogo na Kurasini – kwa Dar es Salaam. Ruvu na Maneromango – Pwani na shule za sekondari Kinondoni, Dar es Salaam na Kibohehe, Moshi.


Utekelezaji mwingine ni pale Serikali ilipotaifisha shule zote za misheni na za watu binafsi (Wahindi na za Wazungu) kuwa shule za Serikali mwaka 1970. Kwa hatua namna hizi, watoto wote wa nchi hii waliweza kupata fursa sawa katika elimu bila kujali rangi wala dini zao katika Taifa huru hili.


Watoto wa sekondari walitawanya katika shule zote za sekondari humu nchini. Wa Kagera wakasambazwa Sumbawanga, wa Kilimanjaro wakasambazwa kusini; wa Lindi/Mtwara walifika Kagera na Kilimanjaro. Hili kwanza liliwapanua upeo wao wa ukubwa wa nchi yetu na wakajionea mazingira tofauti katika mikoa, wakaanza kujengeka kizalendo kwa nchi yao bila kujali makabila na ndiyo chanzo cha utaifa.

 

Kwa hatua za namna hii, watoto wote wa nchi waliweza kupata fursa sawa katika elimu bila kuwapo kwa ubaguzi wa dini au wa rangi au wa mikoa au wa makabila katika Taifa huru la Tanzania.


Mimi ninajikita katika kuielezea elimu katika nchi hii nikiamini kuwa Mtanzania wa leo amekwishajikomboa kifikra, wala hana zile kasumba za Uzungu au Uarabu au za Uhaya, Uchagga, ukusini au ukaskazini, bali yuna uzalendo wa Tanzania tu. Kama fikra yangu hiyo si sahihi, ni kwa sababu ya malezi yale katika kambi za JKT nilikokuwa nalea vijana kutoka kwenye kasumba ya ukoloni, ukabila au usomi na ukihiyo na kuja kwenye uzalendo (patriotism).

 

Siku za kwanza elimu ya kawaida ilipokewa katika nchi yetu iliambatana na imani za kidini za wageni wale waliotuletea elimu yenyewe. Kwa hiyo Ukristu uliambatana na Uzungu wa Magharibi ambako Uislamu uliambatana na Uarabu wa Mashariki ya Kati!


Ni bahati mbaya ilioje imani hii ya kiroho ikaunganishwa na utaifa wa yule aliyeileta. Kutokana na utofauti wa imani, nasi wananchi tumejikuta tukigawanyika kwa misingi ile ile ya imani zetu. Elimu ya kawaida hii ya kusoma na kuandika haina dini kamwe. Wananchi sisi imani za dini tumekuwa nazo tangu kale enzi za mababu.


Kulikuwa na ukoo wenye watu wa imani tofauti huku kwa Wabantu wahusika hawakutengana kamwe. Ndiyo maana unaona Wabantu wa maeneo ya Tanga au Masasi wana majina ya Ukristo na Uislamu kama vile mtu anaitwa Albano Athumani au Silvester Hemedi, John Ramadhani au Francis Juma na kadhalika.


Katika koo zetu jambo namna hili halitupi taabu. Lakini tatizo linaanza pale imani ya mtu inapounganishwa na utaifa wake – Mzungu huyo, basi lazima awe Mkristu au Mwarabu huyo, basi sharti awe Mwislamu. Tafsiri namna hizi si sahihi hata kidogo. Chukua nchi ya Misri ni nchi ya Kiarabu na wananchi wake wote ni Waarabu. Lakini kule Misri wapo Waarabu Wakristo wa Kanisa la Coptic!


Hivi karibuni vyombo vya habari vilitangaza Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo amefariki dunia. Si tulisikia? Hapo ukisema Waarabu wote wa Misri ni Waislamu si sahihi! Lebanon, Palestina, Algeria, Tunisia, Morocco katika historia walikuwapo Wakristu Waarabu huko. Aidha, kusema Wazungu wote ni Wakristu si sahihi pia maana wapo Wazungu hata Wachina Waislamu safi kweli katika ulimwengu wetu huu.


Nijitolee mfano wa umbumbumbu wangu. Nilipokuwa Mafinga JKT kuna sehemu inaitwa Matanana palikuwa na Mzungu (jina nalihifadhi) Mwislamu kabisa katikati ya Wahehe wale. Mimi kwa kasumba yangu ya kufikiria kila Mzungu ni Mkristu nikamuuliza “we! bwana hapa Kanisa la karibu unakokwenda kusali liko wapi?” Alinishangaa akacheka sana! Nakumbuka tu aliniambia msikiti tunaosali hapa ni ule pale! Nikabaki hoi!  Sikudiriki kuongeza swali lingalilotazamiwa kuwa, “Kwani wewe bwana u Mwislamu?” Kasumba mbaya sana kudhani utaifa na dini ni kitu kile kile. Sivyo  hata kidogo jamani! Wazungu waislamu wapo wengi Ulaya hata Marekani.


Sisi Watanzania wa leo tumeipokea elimu ya kawaida kutoka Arabuni na kutoka Ulaya. Hii ni elimu dunia yenye kutujaza ujuzi wa aina aina. Tuwe wazalendo wa Tanzania wala tusijiingize katika kishawishi cha kutafuta nani mchawi wetu katika elimu ya nchi hii.

 

Kulaumu wengine ni alama ya woga wa kupambana na hali halisi iliyoko mbele yetu. Mipango yote ya elimu na sera zote za elimu katika nchi yetu zinaandaliwa na sisi wananchi wenyewe. Kama kuna matabaka au fursa si sawa kwa watoto wote wa Tanzania, basi wa kujilaumu ni sisi wenyewe kwa kukosa ujasiri wa kudumisha uzalendo wetu!


Ipo methali ya zamani pale wahenga waliposema, “YALIYOPITA SI NDWELE, TUGANGE YAJAYO”, maana tusisumbuke na fikra za makosa ya kale – tuamke turekebishe ili tusonge mbele. Enzi zile za ukoloni wageni walituletea hii elimu ya kawaida wakilinganisha na ya kwao. Leo sisi vipi tuendeleze kuiga mambo ya kigeni?  Huku ndiko kuendeleza utumwa wa kifikra.


Mbona tumeshajikomboa na ukoloni sasa bado tunaendeleza majeraha ya ugomvi wa wamisheni Wazungu na mamwinyi Waarabu wa karne ya 19, kweli hiyo? Huyo mwanasiasa mmoja mchekeshaji sana na msanii akiitwa Kanali Moses Nnauye, akiita ulofa mtupu!


Serikali imefungua milango, mimi nasema imetoa ruksa kwa watu binafsi na taasisi za kidini na zisizokuwa za kidini kuwekeza katika elimu. Kwa kuangalia rekodi za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inaonekana wengi wamechangamkia fursa hii na wamewekeza kwenye elimu.

 

Hadi Juni 2011 shule binafsi na shule za madhehebu kwa pamoja zilikuwa 942 (Tazama National Data: Best 2007-2011 ya Juni 2011 uk. 90 tebo nambari 4.24). Katika jumla hiyo, shule za madhehebu yaani seminari za Wakristo na za Waislamu kwa pamoja zimefikia idadi ya shule 105. Shule hizi za binafsi na za madhehebu zinatoa elimu bora sana ukipima matokeo ya mitihani. Zote zinaelimisha watoto wa Taifa hili la Tanzania wala si Wazungu wala Waarabu.


Ndipo mimi natoa wito kwa Watanzania wenzangu tushauri Serikali, watu binafsi na madhehebu waboreshe shule zetu zote zitoe elimu bora na sawa kwa watoto wote wa nchi hii. Najua Serikali imetenga shule fulani fulani na kuziita shule za watoto wenye vipaji maalumu. Hapo sijaelewa vipaji maalumu maana yake watoto wenye akili “saaana” tu ndiyo wanaokwenda katika shule namna hiyo au vipi?


Nakumbuka shule kama Ilboru (Arusha), Mzumbe (Morogoro), Kibaha (Pwani), Tabora Wavulana (Tabora), Msalato (Dodoma), Tabora Wasichana (Tabora), labda zipo na nyingine zinapokea watoto wenye vipaji maalumu (genious). Hizi zote ni za Serikali zina walimu wa kutosha, vifaa kamili na mazingira yake kweli ni ya kutolea elimu bora. Wasiwasi wangu unaanza hapa pa kuwa na shule tofauti kwa watoto tofauti.


Ndipo tunapoanza kujenga matabaka. Utaratibu huu wa kutenga shule kimatabaka ni kama ule wa nchi za kibepari kama Uingereza, ambako unakuta shule maalumu tangu zamani za watoto wa mamwinyi tu. Shule namna hiyo kule Uingereza kama Eaton, Harrow na nyinginezo chache hivi zinaitwa gramma schools.


Kisha zipo shule za kawaida zinajulikana kama technical schools na zipo shule za sekondari kwa kila mtu zinaitwa secondary modern schools kwa huku kwetu hizi ndiyo za kila mtu kama sekondari za Kata.


Mtindo wa kusomesha watoto kimatabaka unajenga matabaka katika Taifa. Si vizuri kuufuata katika nchi ya kijamaa kama yetu hii. Ni kinyume cha ndoto ile ya Baba wa Taifa aliposema mwaka ule wa 1962 kwa maneno haya, “Those of you who are educated, make use of your education to help build a Tanganyika in which everybody will have the opportunity you have had to aquire a good  education” (Nyerere: Uhuru na Umoja uk. 182).


Maneno yale yalitolewa Desemba 1962, lakini bado yanamaanisha dhana ile ya Mwalimu kwa wasomi wote wa nchi hii kuwa watumie elimu waliyopata kujenga Tanganyika ambamo kila mtu ataweza kupata elimu bora kama ile waliyopata wale waliosoma enzi za mkoloni.


Hapa tujiulize kwa mtindo huu wa shule za Kata na shule za watoto wenye vipaji maalumu au shule za binafsi dhana hii itawezekana kweli? Mimi yangu macho!


Kama kila Mtanzania akiwa na uzalendo kweli, fikra au utamaduni uliozoeleka hapa nchini wa kunung’unikia kila dosari na kutafuta faraja katika kumlaumu mtu mwingine, basi hatutafika mbali katika kuulinda umoja wetu na amani tuliyoijenga kwa miaka 51 sasa itatoweka.


Tunapopanga mipango yote ya maendeleo ya Taifa, basi elimu ipewe nafasi maalumu kwa vile elimu ni ufunguo wa maisha. Basi, tuuchonge kwa ubora sana ndipo tutautumia kufungulia maisha bora kwa kila mwananchi hapa Tanzania.


Mwisho, Watanzania sasa tujivunie URAIA wetu ambao hauna dini yoyote. Ukiwa Mtanzania tu kwanza jivunie hiyo hali ya kutokuchanganya uraia wako na dini yako. Wewe sema kama yule Rais wa Marekani, John Kennedy. Kwanza ni Mtanzania, pili u-muumini wa madhehebu haya au yale, lakini kamwe tusiingie katika kishawishi cha kuwa eti mimi Myao basi ni Mwislamu na ukiwa Mhaya, basi wewe ni Mkristo. Si sahihi.


Hivyo basi, Watanzania tukumbuke kuwa URAIA WA NCHI HAUNA DINI. Kama hujapikwa katika kambi za JKT enzi zile za uhai wake, pita sasa mlango umefunguliwa UKAJENGWE KIZALENDO NA KIURAIA (patriotism and nationalism).

Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).


By Jamhuri