Utapeli udhibitiwe Tanzania

Maoni ya Mhariri wa JAMHURI wiki iliyopita, yalipendekeza mtandao wa utapeli wa madini uliopo hapa nchini uvunjwe kwa sababu unaathiri uchumi, heshima na sifa ya Watanzania mbele ya uso wa Dunia. Kwamba watoto na wajukuu wao watakosa wa kufanya naye biashara, hivyo Taifa letu kuendelea kuwa tegemezi.

Maoni hayo si ya kupuuzwa na Watanzania wazalendo na hayana budi kutazamwa kwa mboni mbili zisizo na makengeza. Mboni hizo ziende mbali zaidi katika nyanja ya uchumi, siasa, ulinzi na utamaduni kwa sababu zimekwishaleta mitikisiko ndani yake na kuonesha mifarakano ya kijamii, kitaifa na kimataifa.

 

Mitikisiko hiyo imetokana na vitendo vya hujuma, ufisadi, wizi na utapeli unaofanywa na wafanyabiashara wakishirikiana na baadhi ya wanasiasa na maofisa watumishi wa umma katika sekta za madini, ardhi, kilimo, fedha, utalii, ujangili, michezo na burudani.

 

Vitendo hivyo vinafanywa chini ya uwezo mkubwa wa fedha ambao umevuruga taratibu za utendaji kazi kwenye vyombo vya kutoa haki, usalama, ulinzi, siasa na huduma za jamii. Kote huko kumejenga utamaduni wa kutoa na kupokea hongo na rushwa kama ndiyo mtindo halali wa kupata ajira, uongozi na huduma.

 

Maovu mengi yanatendwa na wenzetu wachache wasio na upendo, udugu na umoja. Hawana uzalendo wala uchungu wa kukosa maendeleo ya Taifa letu. Jambo wanalopenda ni ushirikina wa kujitajirisha, kuvuruga na kuua uchumi wa nchi na kuona Watanzania wengi wakiwa maskini. Ndiyo maana mitandao yao ya utapeli inatumia fedha kama mtaji na nyenzo ya maendeleo yao bila ya kujali Watanzania wenzao wanaumia kiasi gani.

 

Leo tunaarifiwa kuwa matapeli hawa wa madini wanatumia jeuri ya fedha na inasemekana wamefika mahala wameiweka Serikali mfukoni! Dhana ya kuiweka Serikali mfukoni isipuuzwe, ifanyiwe kazi. Hiyo ni jeuri na kiburi kwa Serikali na Watanzania. Lau kama Serikali imesema itapambana kuondoa kiburi hicho, bado narudia kusema mapambano hayo yawe na muono wa mboni mbili zisizo na makengeza, ama sivyo kauli ya Serikali itakuwa bure aghali. Itakuwa haina maana mbele ya jamii duniani.

 

Kauli kama hiyo kwamba tutapambana imepata kutolewa na Serikali katika dhamira ya kupambana na rushwa, wizi, ufisadi, biashara haramu na nyinginezo, lakini dhamira ya mapambano hayo huwa inaisha kiaina aina! Kulikoni Serikali? Wananchi na vyombo vya mawasiliano na umma vinajitahidi kufichua matendo maovu na wakati mwingine kutoa rai au ushauri wa kupambana na maovu hayo. Lakini matokeo yake watoa taarifa au ushauri huishia kufungiwa, mkong’oto au hata kuuawa!

 

Kutokana na maelezo hayo, nina mambo mawili ya kusema. Mosi, Serikali itimize kauli yake kwa dhati ya kufanya utaratibu wa kuwakamata matapeli na kuwafikisha mahakamani. Pili, Serikali iache tabia ya kuchukua hatua kwa matokeo badala ya chanzo au asili ya matokeo hayo.

 

Utapeli katika nchi yetu haukuanza katika karne hii au katika utawala huu wa Awamu ya Nne. Ulikuwapo tangu zamani na huu wa leo ni mwendelezo wenye teknolojia na falsafa ya kimaendeleo ndani ya mtandao wa mawasiliano duniani. Huko nyuma utapeli ulitumia sana lugha yenye maneno mazuri, matamu ya kulainisha na kupumbaza mawazo ya mtu kufikiri kwa makini. Hila zilitumika. Hivyo, utapeli haukuwa na nafasi na nguvu ya kutikisa jamii husika.

 

Leo, utapeli bado unatumia mbinu hizo hizo za zamani pamoja na mbinu mpya za fedha na miundombinu ya kiteknolojia kupitisha taarifa za maandishi katika mitandao ya mawasiliano. Mitandao hiyo imepanua aina anuwai za utapeli duniani, kama vile kupata elimu, kazi, matibabu, biashara, ngono na kadhalika kwa kuonesha picha, filamu au video. Kwa hali hii, nguvu na mbinu za kupambana na utapeli hazina budi kuwa na maarifa ya kiteknolojia.

 

Nadhani, nguvu ya dhana ya fedha na teknolojia ingeweza kuwa dhaifu kama watumiaji wa dhana hiyo hapa nchini wangelelewa katika malezi ya kufundishwa maadili, mila na desturi za jamii ya Watanzania.

 

Tumeelezwa katika tahariri ile ya JAMHURI kuwa wanaofanya utapeli wa madini wengi wao ni askari wastaafu, ambao ukweli wanaharibu heshima ya Taifa hili. Hapa sura mbili zimejichomoza.

 

Sura ya kwanza wastaafu hao huenda wameshindwa kuwa katika maadili mema na umri umekwenda ilhali wanataka utajiri. Sura ya pili, huenda hawakupata mafunzo ya kuwajengea fadhila na mwenendo mwema unaokubalika katika jamii. Kadhalika, hawakufunzwa itikadi na mambo ya siasa wanayopaswa kuyafahamu ili wawe raia wema wanaojua wajibu wao na hali zao katika jamii au Taifa.

 

Katika dhamira hiyo ya kupambana na utapeli hapa nchini, ni busara Serikali ikatumia pia njia ya malezi ya kupambana na mazingira ya mtu katika njia halali na jinsi ya kuyakabili, kudadisi na kupima mambo, kumuhimiza kuwa mwadilifu na muungwana.