Utaratibu wa kisheria katika kununua ardhi

Tunazo aina kuu mbili za ardhi. Tunayo ardhi iliyosajiliwa na ardhi ambayo haikusajiliwa. Ardhi ambayo imesajiliwa ni ardhi iliyopimwa au maarufu ardhi yenye hatimiliki, wakati ardhi ambayo haikusajiliwa ni kinyume cha hiyo.

Na ardhi tunamaanisha viwanja, nyumba au mashamba.

Pamoja na hayo, makala ya leo itamulika ardhi iliyosajiliwa/iliyopimwa/yenye hatimiliki, wakati makala katika toleo lijalo itamulika utaratibu wa kununua ardhi ambayo haikusajiliwa/isiyo na hatimiliki/ambayo haijapimwa.

Marejeo yetu ni  Sheria ya Ardhi, Sura ya 113 na kanuni zake za mwaka 2001, Sheria ya Mikataba Sura ya 345 na Sheria ya Usajili wa Ardhi, Sura ya 334.

Kununua ardhi iliyosajiliwa

Kwanza, mjue mtu anayekuuzia. Na si lazima kumjua sana kutokana na ugumu katika kumjua mtu. Kumjua tu kuwa ni fulani kunatosha, ama kama unaweza kwenda mbali zaidi katika kumjua nayo si mbaya. 

Pili, ukishamjua muulize maswali (interview) kuhusu umiliki wake, alipataje eneo hilo (kwa njia ya kununua, alirithi au alipewa zawadi). Muulize ikiwa kuna mgogoro wowote. Muulize kama ameweka rehani popote. Muulize kama ana mke au mume. Muulize mara ya mwisho kulipia kodi za ardhi, ikiwezekana akuonyeshe risiti za mwisho, muulize historia ya jiografia ya eneo hilo (mafuriko au vimbunga). Muulize na kingine chochote ambacho unahisi ni muhimu kukijua. 

Hapa wengi hawasemi ukweli, na kimsingi hatutarajii ukweli hapa, lakini ukweli tunautarajia hapa chini.

Tatu, baada ya majadiliano sasa ni wakati wa kumuomba akupatie kivuli cha hati (nakala) ili uipeleke ardhi kujiridhisha na baadhi ya hayo uliyomuuliza hapo juu (official search). Huko ardhi utajiridhisha na uhalisi wa jina la mmiliki, kujua ikiwa ardhi imewekwa rehani ya mkopo, kujua ikiwa ardhi ina zuio la mahakama, kujua ikiwa kuna zuio la mtu mwingine mwenye masilahi kama mke au mume, kujua ikiwa maeneo hayo watu watalipwa au walishalipwa fidia ili kupisha mradi fulani. Kujua ikiwa kuna mgogoro au jambo jingine lolote lisilo sawa.

Nne, baada ya kujiridhisha na mambo kuwa sawa, sasa ni wakati wa kujiridhisha juu ya uhalisi wa hatimiliki (genuineness of certificate of title). Wakati mwingine taarifa zilizo kwenye hati zinaweza kuwa sahihi lakini hati yenyewe ikawa si halisi (si genuine, wengine husema si original). Hivyo kuna ulazima wa kujua uhalisi wa hati.

Kwa kuwa si rahisi muuzaji kukupatia hati yake halisi uende nayo kujiridhisha uhalisi wake, basi muombe muambatane hadi ofisi husika ya masuala ya ardhi akiwa ameishika, ambako mtaonyesha hati ile kwa msajili wa hati (Registrar of Titles) ambaye atasema kama hati ile ni halisi ama hapana.  

Tano, baada ya kuridhika na uhalisi wa hati, sasa mnaweza kuanza kujadili masharti ya mauziano. Bei mnatakiwa muwe mmeijadili kabla kwa sababu si vema sana kufanya yote hayo ya awali wakati hamjafikia muafaka wa bei. Hapa mtajadiliana masharti mengine.

Sita, baada ya kuafikiana kwenye masharti ya mauziano, sasa ni wakati wa kuandika mikataba kwa mujibu wa Kifungu cha 64(1) cha Sheria ya Ardhi, kusainishana na wakili kugonga mihuri. 

Hapa hakikisha nyote, muuzaji na mnunuzi, mnasaini mkataba wa mauziano (sale agreement). Hakikisha muuzaji anasaini fomu namba 29 na 30, na hakikisha nyote tena mnasaini fomu namba 35, kanuni za ardhi za mwaka 2001. 

Aidha, ikiwa muuzaji ni mwanandoa hakikisha huyo mwanandoa mwingine ambaye hajasaini kama muuzaji anaandaliwa na kusaini nyaraka iitwayo ridhaa ya mwanandoa (spouses consent). 

Na kama muuzaji ni msimamizi wa mirathi, hakikisha warithi wote wanasaini ridhaa ya warithi.

Saba, baada ya kusaini mikataba, sasa ni wakati wa kulipana, ambapo inashauriwa fedha zilipwe benki ili karatasi za muamala ziwe ushahidi wa malipo (consideration), Kifungu cha 10, Sheria ya Mikataba. 

Mnaweza kuanza kusaini mikataba halafu mkaenda benki kuhamisha fedha huku mikataba ikiwa mikononi mwa wakili au fedha ikaingizwa kwenye akaunti ya muuzaji, halafu hapo hapo benki bila kutoka nje mkasaini nyaraka za mauziano.

Nane, baada  ya hayo yote ununuzi halali, salama na wa kisheria utakuwa umefanyika. Aidha, unashauriwa kumtumia wakili katika hatua zote hizi.

Kuhusu  sheria  za  ardhi, mirathi, kampuni na ndoa, tembelea ‘Sheria Yakub Blog.’