Utata waliofia mgodini TanzaniteOne

Usiri mkubwa unaendelea kufanywa na wamiliki wa mgodi wa TanzaniteOne mkoani Manyara, baada ya kubainika kufukiwa kwa watu watatu; watumishi wa mgodi huo.

Watu hao walifukiwa kwa kile kinachoelezwa kwamba walishukiwa kuwa ni wavamizi walioingia mgodini kujitwalia madini ya tanzanite.

Miili ya watu wawili waliofukiwa imshaopolewa. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Massawe, ameunda timu kuchunguza tukio hilo ambalo linatajwa kufanywa kwa makusudi.

Mkuu wa Ulinzi wa TanzaniteOne, George Kisambe, amehojiwa kuhusu tukio hilo.

Kamishina wa Madini katika Wilaya ya Simanjiro, Henry Mditi, anasema maiti hao waliopolewa kwa nyakati tofauti wiki iliyopita.

Mwili mmoja umetambuliwa kuwa ni wa mtu aliyetajwa kwa jina moja la Halid. Kazi ya kuuopoa inatajwa kwamba ilikuwa ngumu kutokana na kubanwa na kifusi.

Mwingine aliyeopolewa naye ametajwa kwa jina la Dominic.

Mditi amesema miili hiyo ilipelekwa katika Hosptali ya Bomang’ombe kwa uchunguzi kabla ya kuchukuliwa na ndugu zao kwa mazishi.

Mwili wa Said Mgosi ulioplewa Machi12, mwaka huu na kupelekwa katika Hosptali ya Bomang’ombe ambako ndugu zake waliuzika siku iliyofuata hapo hapo Bomang’ombe.

Kisambe anazungumzia uopoaji miili na kusema: “Eneo walilokuwa marehemu hawa lilikuwa baya sana mchanga wa mgodi huu ni tofauti na migodi mingine, lakini tunashukuru Mungu kwa siku nne mfululizo tumeweza kuipata maiti wote.”

Katika ajali hiyo, mchimbaji Gidishi Benedict (32) mkazi wa Babati alinusurika katika tukio hilo.

 

Mapya yaibuka

Familia ya Said Mgosi ambaye ni moja kati ya wachimbaji wadogo wa madini ya tanzanite waliokufa mgodini na mwili wake kuopolewa, inasema ndugu yao huyo alikuwa mfanyakazi wa kampuni ya Sky Associate/TanzaniteOne.

Mkanganyiko huo umekuja siku moja baada ya kampuni hiyo kutoa taarifa kuwa Mgosi alikuwa mchimbaji haramu aliyeingia katika eneo la mgodi kwa lengo la kuiba madini.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake eneo la Bomang’ombe wilayani Hai, mke wa Mgosi, Maisara Said Mgosi alidai kuwa mume wake aliajiriwa katika kampuni hiyo wiki moja kabla ya kufariki dunia.

“Ninapata uchungu sana kutokana na kifo cha ghafla cha mume wangu, aliniaga mimi na watoto wetu wanne kuwa anakwenda kazini TanzaniteOne anakofanyia kazi, leo nashangaa kusikia taarifa kuwa hakuwa mfanyakazi- inauma sana,” alisema Maisara.

Maisara anasema kuwa hata taarifa za kifo cha mumewe alizisikia kwa mlinzi wa kampuni hiyo, Josephat Kasara ambaye alitumia namba ya mume wake kumfikishia taarifa hizo.

“Mume wangu ana kawaida ya kunipigia simu ili apate salamu za familia, nilipoona simu yake nikajua anataka kutusalimia, lakini ilikuwa sauti tofauti ambayo ilipasua moyo wangu baada ya mtu aliyekuwa akiongea kunipa taarifa kuwa mume wangu amefukiwa na kifusi na amefariki,” alisema,

Anataja namba ya mume wake iliyotumika kumjulisha taarifa ya kifo kuwa ni 0755 486603 na baadaye mlinzi huyo akitumia namba 0757 545875 kumpa taarifa za kila hatua hadi mwili ulipopatikana.

Ndugu mwingine, Said Mwambashi, anaeleza kushangazwa na taarifa ya TanzaniteOne ya kumkana ndugu yao kuwa si mfanyakazi wa kampuni hiyo.

“Kama alikuwa mvamizi simu yake ilitoka wapi hadi ikamfikia mlinzi, lakini pia eneo hilo linao ulinzi mkali na taa zenye mwanga ambao mtu hawezi kuingia bila kuonekana,” anasema Mwambashi.

Kwa maoni yake, anasema haiwezekani kwa Mgosi na wenzake wawe na vifaa vya uchimbaji na vyakula kama hakuwa wafanyakazi wa TanzaniteOne.

Anahoji kuwa kama walikuwa wavamizi, waliwezaje kupenya kwenye matundu madogo mno wakiwa na vifaa kama jenereta na mashine za kuchimbia madini.

Mkurugenzi Mwenza wa TanzaniteOne/Sky Associate, Faisal Shahbhay, anasema madai hayo ni ya kutungwa. Anasisitiza kuwa Mgosi na wenzake hawajawahi kuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Mwili wa Mgosi ulipelekwa Bomang’ombe kwa kutumia gari la kampuni ya Tanzanite One, Toyota Land Cruiser lenye nambari T636AEK.