Hivi karibuni Taifa letu la Tanzania limesherehekea sikukuu mbili muhimu na za kihistoria. Bara tulikuwa na sherehe za miaka 51 ya Uhuru wa Taifa letu Desemba 9, 2012 na Zanzibar tulikuwa na sherehe za miaka 49 ya Mapinduzi, Januari 12, 2013. Ni sikukuu za kihistoria maana bila kupata Uhuru toka kwa mkoloni na bila kumpindua Sultan sidhani kama tungekuwa na Jamhuri hii ya Muungano wa Tanzania .

Baada ya kuwa huru watu wa nchi hizi waliweza kujiamulia mambo yao wenyewe, wameweza kujipangia maendeleo yao wenyewe na ndiyo maana waliunganisha hata Jamhuri za nchi zetu mbili kupata nchi moja kubwa na yenye amani inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .

 

Kwa upande wa Tanganyika mimi ninakasumba ya kumnukuu mwalimu wangu wa historia darasani kule St. Mary’s Tabora – huyu kumbe ndiyo sote tumemwita Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere. Kwa kumbukumbu zangu ni kuwa Juni 28, 1962 akizungumzia kuhusu Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika, ilidhihirika hivi namnukuu, “…he argued that it was impossible to devise a foolproof constitution, and that the only real protection against tyranny is a national ethics…” Nyerere: (Uhuru na Umoja uk. 174).


Hapa Baba wa Taifa anatamka wazi kabisa kuwa Katiba hata iwe nzuri namna gani – bila kuwepo na Maadili ya Kitaifa ni kazi bure! Nchi yetu siku hizi imo katika mchakato wa kuandaa Katiba Mpaya yetu wenyewe. Je, hiyo Katiba kweli italeta Utawala Bora katika nchi yetu? Itaondoa kero zote tunazolalamikia siku hizi? Itajibu matakwa yetu yote? Nchi  hii ina watu wenye vionjo na mitazamo mbalimbali, kweli hiyo Katiba itakuwa “toolproof” ya matakwa ya Watanzania wote? Kwa nini nauliza yote hayo?


Hapa nanukukuu tangazo rasmi lililotolewa na Mwalimu Nyerere nalo lilikuwa hivi:-

Sentensi ya mwisho katika Tangazo hili inasema “Every Tanganyikan can now say’ I am a citizen of a sovereign independent state” kwa tafsiri yangu maana yake kila Mtanganyika anaweza kujigamba sasa kuwa yu raia wa Taifa huru. Tangazo hili maana yake kuonesha kuwa baada tu ya kupata Uhuru, hali ya Mtanganyika (status) imebadilika tangu saa ile ile usiku ule tukawa na heshima ya kiutu katika nchi yetu. Haki na uhuru wa raia inategemea Maadili ya Taifa lenyewe.

 

Haya maadili ya taifa ni yapi na nani anayatunga? Maadili ya Taifa ni tabia ya kila raia kuwa Mzalendo wa taifa lake na uzalendo wa Taifa unajengeka kuanzia katika kila familia kwa kuwa na tabia njema, utu, uvumilivu na uwajibikaji. Kujenga uzalendo kuna maanisha kila mwananchi kujua wajibu wake kama raia, kuheshimu Katiba kama sheria mama ya nchi na Taifa na kujali raia wenzake, kuheshimu mawazo na vionjo vyao (Kiingereza tunasema to be tolerant) na kustahiana kitaifa.


Mtu akisoma ule mwongozo uliotolewa na Mwalimu kwa tume ya kuandaa Katiba ile ya Chama kimoja 1963, humo anaweza kukuta baadhi ya hadidu za rejea kwa Tume ile ziliorodhesha Maadili ya Taifa hili. Baadhi ya yale ninayokumbuka ni kama hayo.

i. Kila binadamu huzaliwa huru na sawa katika Uhuru na haki – hivyo kila binadamu anastahili heshima (dignity and respect) na kujaliwa.

ii. Kila raia wa Tanganyika ni mtu muhimu katika taifa hili, hivyo ana haki ya kushiriki katika Serikali Kuu na Seriklai ya Mtaa, mikoani na wilayani.

iii. Kila raia ana haki ya uhuru wa kutembea na kukaa mahali popote ndani ya nchi hii, ana haki ya kufuata dini apendayo, kukutana na yeyote na kujieleza apendavyo mradi havunji sheria za nchi.

iv.  Kila raia ana haki ya kufanya kazi ya akili au ya mikono na kupata mshahara wa haki na mzuri utakaomwezesha kuishi na familia yake.

v. Raia wote wa nchi hii kwa umoja wao, wanamiliki utajiri wa maliasili ya nchi hii na hivyo kuwawekea urithi wazawa wao, utajiri wa maliasili za taifa hili.

vi.  Hakutakuwa na unyonyaji wa mtu kwa mtu au wa taifa moja kwa taifa jingine katika nchi hii.

Haya ni yale ninayoyakumbuka hadi leo ila kwa wasomaji wangu ninaloweza kuwathibitishia kwa uhakika ni kuwa misingi ya maadili ya kitaifa yameainishwa katika zile ahadi 10 za mwana TANU miaka ile kabla ya ujio wa vyama vingi katika nchi yetu mwaka ule 1992. Aidha mtu anaweza kupata ufafanuzi mzuri katika kitabu kile cha ndugu yangu mheshimiwa Ibrahimu Mohamed Kaduma kiitwacho “Maadili ya Taifa na Hatima ya Tanzania” kilichochapwa na Vuga Press 2004.

 

Lakini ninapenda kuwashauri wasomaji wa makala zangu kurejea Hotuba ya Mwalimu Nyerere ya 1963 katika kitabu kile cha Uhuru na Umoja sura ya 55 uk . ule wa 262 alipoelezea kwa maoni yake kanuni za maadili ya kitaifa nambari 1 – 8 ambavyo kwa mtazamo wangu ameunganisha na haki za binadamu zilizotangazwa na Umoja wa Mataifa tangu Desemba 10 mwaka ule wa 1948. Vifungu kadhaa amevichota kutoka kule na kuvielezea katika maelezo yake. Rejea Universal Declaration of Human Rights – kilichapishwa na The Tanganyika Standard – Dar es Salam.


Makala yangu inataka tu kuelezea licha ya bidii zote za Baba wa Taifa kujenga Taifa la Tanzania lenye hadhi na mwonekano wa kuwa na Serikali yenye utawala bora sasa yaelekea Taifa letu linakwenda mrama. Utawala bora wenyewe hatuuoni, matatizo ya kitawala ni mengi sana , kila mtu analalamika kwani kimetokea nini? Hapo ndipo ninapotaka kuelezea mtazamo wangu. Uhuru ni jambo zuri sana . Miaka 10 ya kwanza 1961 – 1971 kila raia wa nchi hii alikiri kuwa tumepiga hatua kimaendeleo katika nyanja karibu zote, elimu, afya, mawasiliano, kilimo, viwanda, wataalamu wetu wenyewe hata ulifika wakati mataifa makubwa ya ulimwengu yalituogopa na kutusifia.

 

Tulisimama kidete kusaidia ukombozi wa nchi za kusini mwa Bara letu la Afrika kama vile Msumbiji , Angola , Zimbabwe , Afrika ya Kusini na Namibia . Tulidiriki hata kumtikisa Mwingereza enzi za Udi, 1965, kule Zimbabwe pale mkoloni Ian Smith alipojitangazia Uhuru wa nchi ile. Tulithubutu hata kutishia kuondoka katika Jumuia ya Madola (Tazama Hanour of Africa by Mwalimu Julius Nyerere Hotuba kwa Bunge tarehe 14 Desemba 1965 uk. 1) pale Serikali ya Tanzania ilikuwa na msimamo na tuliheshimika, tuliogopwa na tulijaliwa na mataifa makubwa. Sasa leo hii kweli tunaweza kuwa na ubavu wa kumtikisa mzungu kama Mwingereza?

 

Ndipo ninajiuliza tuliteleza wapi hata tunajikuta tunabandikiwa maneno ya ufisadi, rushwa, usimamiaji mbovu wa rasilimali za nchi – watu wanapora tu na kadhalika. Mimi ningependa nianzie toka mwaka 1963 au hata nyuma kidogo 1962. Mara baada ya Uhuru baadhi ya wageni kwa dharau za makusudi kabisa walijaribu kuchezea uwezo wa Serikali ya taifa letu huru. Nitoe mifano ya dharau za namna hizo. Siku chache baada ya uhuru kule Mkoa wa Lindi alitokea mzungu fulani alimvalisha mbwa wake beji ya taifa kama alama ya kukejeli uhuru wa nchi hii. Serikali ilipopata habari ile kutoka wananchi wazalendo ikamfukuza mzungu yule katika muda wa saa 24 asionekane katika ardhi ya Tanganyika . Na kweli alikwenda kwao huko Ulaya! Huko Korogwe nako 1963, nafikiri, mkuu mmoja wa Mkoa (Jacob Namfua) alikataliwa huduma za chakula pale Korogwe Twavellers Inn, Hoteli ya wazungu walima mkonge kule mkoani Tanga. Serikali iliifunga hoteli ile na mwenye hoteli alifukuzwa nchini katika muda wa saa 24.

» Itaendelea wiki ijayo


Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).


By Jamhuri