“…Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika muda mchache, kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi na walio wengi watakuwa watwana.”

Haya yalisemwa na Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere,  wakati akitahadharisha wazawa kuepuka kuuza ardhi kwa matajiri na wageni.

 

Uongozi mbovu CCM

“Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa vyama vingi.  Nilitumaini kuwa tunaweza kupata chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha CCM kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao.

Mwalimu Julius Nyerere aliyasema hayo kuwaeleza wananchi umuhimu wa vyama vingi vya siasa.


Rushwa katika CCM

“Wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza si kwamba rushwa haikuwepo, ilikuwepo lakini tulikuwa wakali sana.. Ikithibitika mahakamani kuwa mtu ametoa au kupokea rushwa hatukumwachia hakimu nafasi ya kutoa hukumu peke yake.”

Haya yalinenwa na Mwalimu Nyerere kuhimiza wananchi kushirikiana katika kupiga vita vitendo vya rushwa.

 

Watawala wa nchi

“Amini nawambieni enyi Waswahili wachache mnaotawala; mnategemea kweli kuwa mtawaongoza Watanzania kwa lazima wakati wamepoteza matumaini, na mtegemee kuwa watasalia wamekaa kimya kwa amani na utulivu?”

Manano haya ya Mwalimu Nyerere yanawahimiza viongozi kuhakikisha wanatimiza matarajio ya wananchi kuepusha uvunjifu wa amani nchini.

 

 

Amani na utulivu

“Amani ni zao la matumaini, pindi matumaini yatakapotoweka kutakuwa na vurugu katika jamii.”

Mwalimu Nyerere aliyasema haya kusisitiza umuhimu wa kulinda amani kuepusha vurugu katika jamii.

Upigaji kura

 

“Mtu aliyejiandikisha kupiga kura, halafu siku ya uchaguzi haendi kupiga kura, huyo ni mpumbavu.”

Maneno haya ya Mwalimu Nyerere yanahimiza wananchi kuzingatia suala la kujitokeza kupiga kura kuchagua viongozi wanaowataka.


 

 

 

 

By Jamhuri