Dk. Rashid Tamatamah katika picha ya pamoja na wahariri waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
Dk. Rashid Tamatamah katika picha ya pamoja na wahariri waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya habari.

Wakati serikali ikiwa na takwimu za samaki kwenye maziwa, hali ni tofauti kwenye eneo la bahari kuu ambako sensa haijafanyika ili kutambua rasilimali hizo ambazo tangu Tanzania ipate uhuru hazijawahi kuvunwa wala kutambuliwa kwa idadi halisi.

Katika kikao kazi baina ya wahariri waandamizi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (anayeshughulikia sekta ya Uvuvi), Dk. Rashid Tamatamah, amesema serikali imeanza mikakati ya kufahamu samaki wanaopatikana katika eneo la bahari kuu iliyoko ndani ya himaya ya Tanzania.

“Tunayo hifadhi ya samaki wengi sana kule bahari kuu ila bado hatujawekeza katika kupata idadi sawasawa ya mazao ya bahari yaliyoko katika eneo la bahari kuu. Hivi karibuni kuna meli moja ya nje ilijaribu kufanya zoezi hilo, hatukuridhika na takwimu zao,” amesema Dk. Tamatamah.

Dk. Tamatamah amesema sekta ya uvuvi nchini imekuwa chanzo muhimu cha upatikanaji wa samaki na mazao yake kwa ajili ya lishe, kipato na ajira. Huku akisisitiza kwamba miaka ya hivi karibuni samaki hawaongezeki kukidhi mahitaji kulingana na ongezeko la watu.

“Kiasi cha samaki wavuliwao kuanzia miaka ya 1990 hadi sasa kimebaki kuwa ni kati ya tani 350,000 na 400,000 kwa mwaka. Lakini katika kipindi hicho idadi ya watu imeongezeka kutoka watu milioni 25 hadi watu milioni 55, hali hiyo imesababisha kushuka kwa kiasi cha samaki kiliwacho kwa kila mtu kwa mwaka kutoka kilogramu 14 mwanzoni mwa miaka ya 90 hadi kilogramu 8 mwaka 2019.

“Hali hii inatishia ustawi wa taifa kwa vile samaki huchangia asilimia 30 ya protini itokanayo na wanyama na asilimia 1.7 ya pato la taifa. Vilevile inachangia katika ajira na kipato ambapo zaidi ya watu milioni 4 wameajiriwa katika shughuli zinazotegemea uwepo wa samaki,” amesema Dk. Tamatamah.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (sekta ya Uvuvi), ukanda wa Pwani wenye  urefu wa kilomita 1,424, eneo linalojumisha maji ya kitaifa kilomita za mraba  64,000 na ukanda wa uchumi (EEZ) kilomita za mraba 223,000.

Akizungumza na wahariri waandamizi hivi karibuni, Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Magesse Bulayi, amesema lengo kuu la sera ya taifa ya uvuvi ni kukuza uhifadhi, maendeleo na usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

 Bulayi amesema sekta ya uvuvi inatoa ajira kwa wavuvi waliosajiliwa 202,053 mwaka 2017/18; na watu wengine zaidi ya milioni 4.5 wameajiriwa kupitia sekta ya uvuvi.

 “Kiwango cha rasilimali kinachoweza kuvuliwa bila kuathiri uwepo wa rasilimali hiyo ni tani za kimetriki 750,000. Hata hivyo wastani wa kiwango cha samaki kinachozalishwa nchini kwa mwaka kwa sasa ni tani 350,000 ambacho kinazalishwa na wavuvi zaidi ya 230,000 walioandikishwa kisheria,” amesema Bulayi.

Katika miaka ya hivi karibuni hali ya uzalishaji wa rasilimali katika maji ya nchi yetu imekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa nguvu ya uvuvi  (wavuvi) 156,544 (2006) – 203,529 (2017), kuongezeka kwa vyombo vya uvuvi kutoka 51,552 mwaka 2006, vyombo 59,338 mwaka 2017 na kuongezeka kwa zana za uvuvi 7,628,432 mwaka 2010 hadi zana 8,386,561 mwaka 2017.

Samaki hawatoshelezi

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema kuwa idadi ya samaki waliopo nchini haitoshelezi kulingana na idadi ya Watanzania ambayo inazidi kuongezeka kila mwaka na kushindwa kila mtu kula wastani wa kilogramu 14 kwa mwaka.

Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na  Katibu Mkuu wa Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Rashid Tamatamah wakati akifungua kikao kazi cha wataalamu wa sekta ya uvuvi na wahariri wa vyombo vya habari nchini ikiwa ni kutoa mwelekeo  wa sekta ya uvuvi nchini.

Dk. Tamatamah amesema kiasi cha samaki wavuliwao kuanzia miaka ya 90 hadi sasa, kimebakia kuwa ni kati ya tani 350,000 na 400,000 kwa mwaka, huku idadi ya watu ikiongezeka kutoka takriban watu milioni 25 hadi kufikia milioni 55.

 “Hali hii inatishia ustawi wa taifa kwa vile samaki huchangia asilimia 30 ya protini itokanayo na wanyama na asilimia 1.7 ya pato la taifa. Vilevile inachangia katika ajira na kipato ambapo zaidi ya watu milioni 4 wameajiriwa au kujiajiri katika shughuli zinazotegemea uwepo wa samaki,” alisema.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa taarifa za utafiti zilizofanyika katika vipindi tofauti, kiasi cha samaki kilichopo katika maji yetu ni tani 2,803,000 ambapo mchanganuo wa kiasi unajumuisha tani 2,210,000 katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika tani 295,000 na Ziwa Nyasa tani 168,000.

Alisema maji madogo (maziwa madogo na ya kati, mito na mabwawa) tani 30,000 na Maji ya Kitaifa ya Bahari ya Hindi tani 100,000.

Amesema katika mwaka 2018/19 kulikuwa na jumla ya wavuvi 202,053 nchini walioshiriki moja kwa moja kwenye shughuli za uvuvi kwa kutumia vyombo vya uvuvi 58,930.

“Nguvu hii ya uvuvi iliwezesha kuvunwa kwa tani 448,468 zenye thamani ya Sh trilioni 2.11 sawa na ongezeko la asilimia 15.72 ya samaki (tani 387,543) zilivunwa mwaka 2017/18. Ongezeko hili limetokana na juhudi za wizara katika kudhibiti uvuvi haramu nchini,” alisema.

Vilevile, alisema katika mwaka 2018/19 jumla ya tani 51,718.83 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 81,373 wenye thamani ya Sh bilioni 691.88 waliuzwa nje ya nchi.

Aidha, alisema katika kukabiliana na upungufu huo, serikali iliamua kuhamasisha uwekezaji katika tasnia ya ukuzaji viumbe maji, pamoja na kuanzisha idara ya ukuzaji viumbe maji kwa ajili ya kusimamia na kuendeleza tasnia ili kuongeza uzalishaji wa samaki na viumbe maji wengine.

Pia wizara kupitia Wakala wa Elimu na Mafunzo (FETA) kwa kushirikiana na NORGES VEL (Asasi isiyo ya kiserikali ya nchini Norway) na Chama cha Wakuzaji Viumbe Maji nchini (AAT) ilipata ufadhili wa Sh bilioni 4.6 kutoka Shirika la Misaada la nchini Norway (NORAD) kutekeleza mradi wa uzalishaji wa samaki aina ya sato na kufundisha Stadi za Ufugaji na Biashara.

Aliongeza kuwa wizara inaendelea na juhudi za kufufua lililokuwa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ili kuimarisha uwekezaji katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari, na Bahari Kuu ambapo menejimenti ya kusimamia ufufuaji wa TAFICO ilizinduliwa Julai, 2018.

Uvuvi wa bahari kuu

Taarifa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi zinaonyesha kwamba ushiriki wa wazawa katika uvuvi wa bahari kuu ni mdogo ikilinganishwa na kampuni zinazofanya uvuvi kutoka nje ya nchi. Hatua hiyo inachangiwa na gharama kubwa katika uwekezaji wa uvuvi wa bahari kuu.

Hata hivyo alisema wanajaribu kuhamasisha wazawa kujiingiza katika uwekezaji huo ingawa kuna gharama kubwa, ikiwemo kuandaa sera nzuri hasa katika uwekezaji wa ndani.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Tamatamah amesema vyombo vya habari vina jukumu la kuwaelimisha wananchi kuhusu uchumi wa bahari (blue economy) kupitia rasilimali za bahari ukiwemo uvuvi wa bahari kuu pamoja na uhifadhi wa mazingira ya baharini.

Amesema pamoja na mafanikio yanayoendelea kupatikana kupitia uvuvi wa bahari kuu, bado sekta hiyo inakabiliwa na tatizo la upungufu wa vitendea kazi ikiwemo vyombo vya usafiri.

Hata hivyo Gazeti la JAMHURI linafahamu kwamba kuna mradi wa uvuvi wa bahari kuu ambao umeanza tangu mwaka 2015 chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia na unamalizika mwaka 2021.

Hali ya rasilimali nchini

Kiwango cha rasilimali kinachoweza kuvuliwa bila kuathiri uwepo wa rasilimali hiyo ni tani za kimetriki 750,000. Hata hivyo wastani wa kiwango cha samaki kinachozalishwa nchini kwa mwaka kwa sasa ni tani 350,000, ambacho kinazalishwa na wavuvi zaidi ya 230,000 walioandikishwa kisheria.

Uvunaji wa rasilimali ya uvuvi hapa nchini unafanyika kwa kuzingatia sheria za nchi zilizopo:-

Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003 na Kanuni za Mwaka 2009; Sheria ya Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004 na kanuni zake.

Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu na Sheria ya Bahari Kuu ya Mwaka 1998 na Marekebisho yake ya Mwaka 2007 na kanuni zake za Mwaka 2009 na Marekebisho yake ya Mwaka 2016.

Majukumu ya Idara ya Uvuvi

Sera ya Taifa ya Uvuvi ya Mwaka 2015 imeweka bayana umuhimu wa Sekta ya Uvuvi ili kuchangia kikamilifu kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo  wa Taifa 2025.

Lengo Kuu la  Sera ya Sekta ya Uvuvi ni  kuendeleza, kuhifadhi, kusimamia na kuvuna kwa uendelevu rasilimali za uvuvi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 2015, majukumu mahususi ya sekta ya uvuvi ni pamoja na kuandaa Sera, Sheria na Mipango ya Kuendeleza Sekta ya Uvuvi.

Kuhakikisha kuwa rasilimali za uvuvi pamoja na mazingira yake zinasimamiwa kikamilifu na kwa njia endelevu kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na taratibu mbalimbali zilizopo na kukuza uwekezaji katika Sekta ya Uvuvi hususan katika uvuvi wa Bahari Kuu.

By Jamhuri