Huwa kila jamii yenye kujiheshimu hujiwekea vigezo vya watu wanaotakiwa kuwa ndani yake. Mataifa nayo – kwa kuwa yana mipaka yake yana watu ambao ruksa kuwa ndani – na wengine wote haruhusiwa kuingia, kukaa kwa muda mfupi au mrefu hadi kwa ruhusa maalumu (viza).

Katiba za nchi mbalimbali zimeweka vipengele tofauti kuhusu hili, na sheria zitokanazo na Katiba hizo zimeainisha barabara nani anafaa kuruhusiwa kukaa nchini au kuwa raia.

 

Katika miaka yangu zaidi ya 20 hapa Uingereza, nimekuwa naifananisha nchi hii na Marekani, ambao pamoja na utajiri wao mkubwa, imekuwa mstari wa mbele kupokea watu wa mataifa mengine na hata kuwapa uraia au ukaazi wa kudumu.

 

Marekani ni nchi kubwa kwa kila namna na ukubwa wa eneo unaipa jeuri ya kukaribisha watu wengi. Lakini Uingereza ni kanchi kadogo kijiografia, Tanzania inaiacha kwa mbali, lakini pia ina wageni wengi.

 

Kwa vile sasa wanataka watu wenye viwango vya juu kuwa raia wao, wameweka kigezo muhimu cha kuupata, nacho ni majaribio au mtihani, wala si kutangaza magazetini sijui mara mbili au nne kama zifanyavyo baadhi ya nchi.

 

Tena wao mtihani wao wala hauhusu wewe kujua mambo ya dunia nyingine, bali kuijua kwa undani Uingereza, historia yake na kwa kuzama sana utamaduni wake.

 

Kwa hiyo unaweza ukawa unapenda mno kuwa mtu wa Uingereza, lakini mstari wa mwisho kukuruhusu ni kuijua UK kama sala ya Baba Yetu kwa Wakatoliki au ‘on call’ kwa matabibu kama sisi. Ukiingia kwenye chumba cha mtihani unakutana na maswali kama ya Cheggers ni nani na kwa sababu gani anachekesha hivyo?

 

Nimemsikia mwenyewe kwenye kantini ya wabunge pale Westminster, Theresa May, huyu mama ambaye ni waziri wa mambo ya ndani, akisema wamenuia kuweka uzalendo kama kiini cha utambulisho wa Mwingereza yeyote.

 

Kwa hiyo mambo muhimu wanayotakiwa kujua wanafunzi wa uraia wa Uingereza ni historia ya kisiwa hiki kikubwa chenye nchi nne, kilitoka wapi, kikapitia wapi na akina nani kabla ya kufika hapa kilipo sasa.

 

Uwe mweusi, mwekundu au rangi yoyote na kutoka eneo lolote la dunia hii, lazima ‘ukimanye’ Kiingereza vya kutosha, kwa sababu ni nguzo moja ya Uingereza.

 

Si tunapiga kelele kila siku kwa wanafunzi wetu kwenye somo la Siasa, hapana siku hizi wanaita ‘Uraia’ na kule sekondari ‘Civics’, kwamba Mwalimu Nyerere aliwaunganisha Watanzania kupigania uhuru kwa kutumia lugha moja – Kiswahili?

 

Sasa Waingereza wanasema wanataka kusonga mbele kutoka hapa walipo kwa kutumia Kiingereza. Labda kimbelembele cha baadhi ya watu kupigia debe Kiswahili na lugha nyingine mpaka zikapokewa Umoja wa Mataifa (UN) kimewaudhi akina May.

 

Kwa hiyo Mhindi anayetoka Kashmir au Jammu; Mkenya wa Kakamega; Mzambia wa Ndola na Mmisri wa Alexandria wote watatarajiwa kueleza kwa kina na Kiingereza kizuri Brut au Brutus wa Toy ni nani.

 

Wewe unamjua? Kama humjui rudi darasani hata kama huutaki uraia wa Uingereza, maana itafika mahali Tanzania tukakutaka umjue.

 

Hii ni kwa sababu Uingereza wametutawala na hivyo lazima uwajue mababa wa Uingereza. Umemjua sasa? Kama hujamjua kapumzike kidogo ndipo urudi kusoma makala haya, japo yanaishia.

 

Yale maswali yaliyokuwa ya kawaida siku zilizopita yamefutwa. Ulikuwa ukiutaka uraia wa UK (si Ukerewe kwa shemeji zangu), unaulizwa maswali kuhusu haki za binadamu (ambazo ni universal of course!)

 

Ungeulizwa pia na utarajiwe ueleze kwa mapana na marefu yake juu ya masurufu na mafao anayopata mtu mwenye haki ya ukazi au uraia wa Uingereza. Anzia nyumba, kazi au mshahara wa kumtosha kwa matumizi ya msingi, matibabu na kadhalika.

 

Waziri May ameyakata na kutupa kwenye jalala, labda kwa vile masurufu yenyewe yanapunguzwa kila siku na labda hadi mwaka huu uishe nayo yakawa kama yameisha.

 

Mbavu ziliniuma nilipomwona amepita kwenye kijia fulani sijui alikuwa akiwaza mambo hayo ya mitihani hati kiatu kikamvuka mama wa watu, nikabaki kusema kweli uzalendo una kazi.

[email protected]

By Jamhuri