John Stephen AkhwariKatika michezo ya Olimpiki iliyofanyika nchini Mexico katika Mji wa Mexico City mwaka 1968 Tanzania iliwakilishwa na mwanariadha aliyefahamika kwa jina la John Stephen Akhwari kwa upande wa mbio za marathon.

Kwa wale wasiomfahamu huyu ni mwanamichezo hodari wa kipindi hicho aliyekuwa na roho ya chuma na uzalendo uliotukuka kwa taifa lake.

Katika mashindano hayo aliacha kumbukumbu ambayo hadi leo ingali katika kumbukumbu za wapenzi na wanamichezo wote wa kipindi hicho.

Duru za michezo za wakati huo zinaeleza kuwa saa moja kabla ya waandaji kuhitimisha utoaji wa zawadi kwa washindi Akhwari aliingia uwanjani huku akiwa amesahaulika.

Taarifa zinaeleza kuwa aliingia uwanjani huku akiwa ameumia mguu ukiwa umeteguka akiwa amekataa kupanda gari la wagonjwa akilazimisha kumaliza mbio.

Huku akiwa anatokwa na damu kwenye jeraha lake akiwa amezingirwa na wanahabari  waliotaka kujua kilichomsibu mpaka akatae kupanda gari la wagonjwa, aliwajibu kuwa alitumwa na Watanzania kumaliza mbio na si vingine.

Katika mbio hizo Akhwari hakushinda medali, lakini uwakilishi wake katika mashindano hayo ulijawa na uzalendo uliotukuka kwa nchi yake.

Hata kama hakushinda medali, lakini aliamini katika utanzania wake na aliweka maslahi ya Tanzania na Watanzania wote kwa ujumla.

Hii ilikuwa ni kauli yenye chembechembe ya uzalendo na ushujaa uliotoweka miongoni mwa wachezaji wetu wa zama hizi ambao licha ya kukosa uzalendo, lakini wamefeli hata kitika michezo yenyewe.

Hebu jaribu kuweka kando uzalendo huo kwa nchi aliokuwa nao mwanariadha huyo wa wakati huo unaelewa sababu zinazotufanya tusiwe na mtu kama Maria Mtola, Hussein Bolt, Juma Ikangaa  na wengi wanaotamba katika anga za kimataifa miongoni mwa wanamichezo wetu wa kileo?

Jibu la swali hili haliwagusi wanamichezo pekee ndani ya nchi yetu, ni jibu linalowagusa wanamichezo, wanasiasa na jamii yote ya Kitanzania.

Ukimtazama Mtanzania wa leo utagundua kuwa kuna sehemu kubwa ya uzalendo na ushujaa fulani uliopotea miongoni mwa jamii nzima.

Wanamichezo wengi wa zama hizi hawana moyo wa chuma wa kupambana na kujitoa mhanga kwa ajili ya nchi na maslahi yao binafsi kama ilivyo kwa wenzao wa miaka ya nyuma.

Wengi wao ni wale waliojawa na maono ya kitaifa badala ya ile ya kimataifa na hawapo tayari kujifunza kutoka kwa wenzao wanaotoka katika mataifa yaliyopiga hatua.

Nyakati za usajili wengi wa wachezaji hawa wamekuwa wakilipwa mamilioni ya fedha kuliko wenzao, lakini bado hawana moyo wa chuma kupambana.

Ni dhahiri kuwa endapo wanamichezo wengi wa zamani kama ndio tungekuwa nao katika kipindi hiki ni hakika tungekuwa mbali.

Wana michezo kama Filbet Bayi, Juma Ikangaa, Akhwari, Peter Tino, Makumbi Juma, Sundey Manara na wengine wengi wangekuwa ndio za zama hizi hakika tungekuwa katika anga nyingine katika michezo.

Hawa ni baadhi tu ya wanamichezo waliofanya vizuri katika enzi zao licha ya kucheza nyakati za giza ambapo soka halikuwa katika kiwango ikilingashwa na hali ilivyo leo.

Kama hiyo haitoshi ukiwangalia wengi wa wachezaji wa leo ni watu wasiokuwa na hasira ya maisha ukilinganisha na wanamichezo wengine kutoka mataifa kama ya magaribi.

Wachezaji wengi kutoka nchi za Afrika Magaribi ni watu wenye roho za chuma mithili ya akina John Stephen Akhwari, ni watu wenye tabia ya kujitoa mhanga anapokuwa katika harakati za kutafuta maisha.

Mara nyingi tumekuwa tukiwashuhudia wanamichezo wetu wa kileo wakienda nje ya nchi kucheza soka mara anaweza akakaa huko kwa muda mchache baadaye utasikia tayari karudi bila hata ya kuwa na sababu maalum.

Hata kwa viongozi bado kuna matatizo makubwa linapokuja suala la uzalendo achana na mchezo wa soka ambao tayari tumeishakubali kushindwa. Hebu angalia vituko hata kwenye michezo mingine.

Kwa mfano Tanzania inatarajiwa kutuma wawakilishi katika mashindano ya Olimpiki yanayotarajiwa kufanyika nchini Brazil, Agosti mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wahusika Tanzania inatarajiwa kuwakilishwa na wachezaji saba, idadi hii haina tofauti na ile ya walioshiriki katika mashindano kama hayo yaliyofanyika nchini Uingereza.

Hakika hiki ni kichekesho, halafu tutarajie watu hawa warudi na medali hizi ni ndoto za alinacha, wakati sisi tutawakilishwa na wanamichezo wapatao saba jirani zetu Kenya watakuwa na watu 50.

Kinachojionyesha leo ndani ya michezo yetu ni ukosefu wa viongozi wenye mioyo ya kizalendo kwa nchi kama walivyokuwa akina Akhwari na wenzake wa enzi hizo.

Michezo ndani ya nchi imegeuka kuwa vitega uchumi vya watu. Angalia hata yanayoendelea ndani ya vyama vya mchezo wa masumbwi nako ni vituko.

Hakuna mipango thabiti yenye malengo ya kuendeleza mchezo, kila kukicha ni malumbano yasiyokuwa na manufaa kwa wanamichezo na mchezo wenyewe.

Ni aibu kwa taifa kama Tanzania ambalo miaka ya nyuma lilisifika kwa kutoa wanamichezo mahiri, leo kugeuka kuwa kichwa cha mwendawazimu katika ukanda huu.

Kama tunahitaji kurudi katika ushindani wa kweli ni lazima tuanze kwanza na somo la uzalendo na kujitambua kwa wanamichezo wetu kuanzia ngazi ya chini.

1542 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!