Vee Money: Aachana na Sheria, afanya muziki 

Inawezekana ukawa haufahamu historia ya msanii, Vanessa Mdee (Vee Money). Kupitia makala hii una nafasi ya kutambua alikozaliwa, alivyoanza muziki na hata mafanikio yake aliyoyapata kupitia tasnia hiyo ya muziki wa Bongo Fleva.

Vee Money alizaliwa Juni 7, 1988 jijini Arusha. Ni msanii wa muziki mwenye talanta nyingi zikiwemo za kuandika nyimbo, pia ujasiriamali.
Amekuwa akifahamu tamaduni mbalimbali baada ya kukua katika miji mbalimbali duniani kama vile Arusha, New York, Paris na Nairobi

Alipata elimu ya sekondari katika shule zilizopo jijini Arusha.

Vanessa alipata elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na kusoma Shahada ya Sheria. Baadaye akaanza kujishughulisha na masuala ya ubunifu na sanaa.

Kama walivyofanya wanamuziki wengi duniani, akaachana na taaluma aliyosomea akaamua kujikita katika masuala ya muziki.

Ikumbukwe kwamba huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), yupo mwanamuziki ajulikanaye kwa majina ya Koffi Olomide, ni msomi mwenye shahada ya umahiri/uzamili, aliyeamua kuziweka kando na kufanya muziki.

Mwanzoni mwa mwaka 2007, Vanessa alipata fursa ya ukaguzi katika MTV VJ Search jijini Dar es Salaam. Baadaye alijiunga na Carol na kuwa mwenyeji wa Coca-Cola Chart Express.

Mwaka 2008, Vanessa alifanya maonyesho nchini Nigeria, Afrika Kusini, Kenya, Msumbiji, Angola, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Umaarufu wake unajulikana zaidi nchini Marekani na Brazil. Mwaka 2008, Vanessa alifanya kazi na Shirika la Staying Alive kuhusu mradi wa karibu na moyo wake.

Vanessa alipaswa kutembelea Uwanja wa Fisi jijini Dar es Salaam akiambatana na Balozi maalumu wa Alive Foundation, Kelly Rowland.

Uwezo wake wa kuhamasisha ulisababisha kujiunga na kampeni ya Malaria No More katika kampeni yao ya ‘Zinduka’, iliyolenga kukomesha malaria.

Anafahamika kama mwanamke wa kwanza kutoka Tanzania kutangaza katika kituo maarufu cha runinga cha MTV VJ kuanzia mwaka 2007 na baadaye kutangaza katika shindano la Epic Bongo Star Search na kipindi cha ‘Dume’ katika kituo cha ITV.

Mwaka 2012 Vanessa alijiunga na kundi la B’Hits na kushirikishwa na msanii nguli, AY, pamoja na msanii Ommy Dimpoz katika wimbo.

Mwaka 2009 Vanessa alitangaza katika maonyesho ya Sauti za Busara International Music Festival, ambayo hufanyika visiwani Zanzibar.

Aidha,  mwaka 2011 alikuwa mtangazaji wa kituo cha redio nchini kijulikanacho kama Choice FM na kufanya mahojiano na wasanii kibao wakiwemo K’Naan, Kelly Rowland, Mac Miller, Rick Ross, Ludacris, Miguel, Donald, Naazizi, Xtatic, Stella Mwangi, Camp Mulla, Tay Grin, Teargas, Dk. Sid na wasanii wengine wengi  barani Afrika na kimataifa.

Vanessa aliwahi kupata tuzo na kushiriki katika kazi na matangazo mbalimbali yakiwemo ya Music Awards, Airtel, Coke Studio, Crown Paints, Music Tours mwaka 2014 na kufanya nyimbo kibao ikiwemo ‘Siri’, ‘Hawajui’ na ‘Closer’.

Baadhi ya nyimbo za msanii Vanessa ni ‘Wet’, ‘Juu’, ‘Kisela’, ‘Cash’, ‘Madame’, ‘Niroge’, ‘Banbino’ na ‘Nobody But Me’. Nyingine ni ‘Scratch My Back’, ‘Kwangu Njoo’, ‘Move’, ‘Reekado Banks’, ‘Bounce’, ‘Pumzi ya Mwisho’ na ‘Hawajui’.

Vanessa aliachia vibao vingine ‘matata’ vya ‘Come Over Shadee’, ‘Unfollow’, ‘Don’t  You Know’, ‘Never Ever’, ‘Tusimame’, ‘The Way You Are’ na ‘Closer’.

Vanessa ana dada yake aitwaye Nancy ‘Namtero’ Mdee a.k.a Tero, aliyekuwa mtangazaji maarufu wa kipindi cha Str8 Up cha KTN ya Kenya. Hata hivyo Tero ameachana na fani hiyo kwa sasa na kuanzisha familia.

Vanessa kama walivyo binadamu wengine, yumo kwenye mahusiano na mwanamuziki, Juma, maarufu kama Jux.