*Madudu yake yanamchafua Rais Kikwete

Mara tu baada ya mawaziri wanne kujiuzulu na wengine kuondolewa kutokana na tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu katika Operesheni Tokomeza, mwandishi mmoja aliandika makala iliyokuwa inasomeka, “Kikwete ana mkosi gani na mawaziri wake?”

Alirejea matukio mengine yaliyosababisha mawaziri wake wajiuzulu. Alichokuwa anahoji ni kitendo cha mawaziri hawa kutokuwajibishwa hadi Bunge lishinikize. Alihitimisha makala yake kwa kuonya kuwa kuchelewa kuchukua hatua hadi Bunge lishinikize, ni kutokutendea haki wananchi na Taifa, kwani tayari wananchi wanakuwa wameshaumia vya kutosha na kama ni hasara inakuwa imeshakuwa kubwa.

Mwandishi huyo anasema kuwa athari mbaya zingeweza kuepukwa kama Rais na Waziri Mkuu wangekuwa makini kufuatilia nyendo za kila waziri kulingana na mahitaji ya wananchi na Taifa. Akashauri hatua ya Bunge iliyowang’oa mawaziri wanne iwe fundisho kwa Rais Kikwete katika kipindi chake kifupi kilichosalia.

Naamini Mheshimiwa Rais anasoma magazeti au kupewa taarifa na wasaidizi wake juu ya vitendo vya wateule wake, maoni na malalamiko ya wananchi anaowaongoza. Kama wasaidizi wake hawafanyi hivyo, basi hawatendi haki kwake yeye, wananchi na Taifa letu.

Wasaidizi hao watakuwa sababu ya wananchi wasio na hatia kuumia huku ustawi wa Taifa letu ukiporomoka. Matokeo yake ni kumfanya Rais wetu kuonekana kama asiyejali, mbinafsi na mwenye roho mbaya.

Hali hii inaweza kumchafua Rais na familia yake kwa kuwahusisha na uchafu ambao hawastahili au hawaujui kabisa. Kutokuwajibika kwa wasaidizi wa Rais hakuna maana nyingine zaidi ya kumharibia jina na historia Rais wetu.

Nimeshawishika kuandika makala haya kutokana na mfululizo wa tuhuma na uamuzi wenye utata unaotokana na mmoja wa wateule wa Rais, Lazaro Nyalandu, ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii. Tuhuma hizi si ngeni tena katika mitandao ya kijamii na magazeti mbalimbali nchini. Unajiuliza kuwa kwa hali hii huko Maliasili na Utalii kuna linalofanyika kweli?

Mmoja wa waandishi ameorodhesha tuhuma zinazomkabili Nyalandu kwa mujibu wa mitandao ya kijamii kuwa ni pamoja na kesi za jinai wakati akiwa Marekani, kudhulumu watoto, kuvunja kihalifu vizuizi vya barabarani kule Singida, tuhuma za kuwa jangili namba moja, kupokea “asante” kutoka kwa kampuni za utalii na uwindaji, kutishia watu kwa bunduki, kuhusishwa na Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA), kusema uongo kwenye wasifu (CV) yake na nyingine nyingi.

Pamoja na tuhuma hizi, magazeti kadhaa yametaarifu uamuzi wa kibabe na utata kisheria aliofanya mara tu baada ya kuteuliwa kuwa waziri kamili. Uamuzi huo, ambao anasemekana kuwa na maslahi binafsi kwake kuliko Taifa, umemfanya kutelekeza kabisa vikao vya Bunge Maalum la Katiba kwani tangu lianze alionekana mara moja tu na kwa saa chache wakati Rais alipokwenda kuzindua Bunge hilo.

Inasemekana kuwa Nyalandu anatumia kuwapo kwa Bunge la Katiba kama fursa kufanya mambo yake kwa kuwa akili za Watanzania wengi ziko Dodoma, na pia vyombo vingi vya habari vimejikita zaidi kuandika habari za Bunge hilo. Hivyo si rahisi madudu anayofanya kujulikana kwa walio wengi! Hali hii ya kukacha Bunge kwa kisingizio cha uwaziri pia imehojiwa na baadhi ya wapiga kura wake wa Singida Kaskazini.

Uamuzi tata aliofanya Nyalandu ni pamoja na kuvunja sheria na taratibu za utumishi wa umma kwa kuwaondoa kwenye nyadhifa zao watendaji waadilifu na kuwapandisha vyeo wenye tuhuma za ujangili!; kutumia mamilioni ya Serikali kumleta, kumlisha na kumlaza mwandishi wa habari wa Uingereza aliyeitukana Serikali na Rais wetu – (hata hivyo ukarimu huu ukawa sababu ya aibu kubwa zaidi kwetu); kudharau maoni ya wataalamu na kuamua kurefusha msimu wa uwindaji ili kuwafurahisha matajiri wenye vitalu bila kujali athari za uamuzi huo kwenye ustawi wa wanyamapori na uchumi wetu; kuongeza muda wa kulipa ada za vitalu vya uwindaji; kushiriki katika mchezo mchafu na jaribio lililoshindwa la ‘kuuza’ Hifadhi ya Taifa Katavi kwa makaburu wa Afrika Kusini akishirikiana na James Lembeli.

Tuhuma hizi na uamuzi huu vimejadiliwa mno kwenye mitandao na magazeti. Sina haja kuendelea kujadili hapa. Langu ni swali tu kwa mamlaka za uteuzi wa Nyalandu. Je, inawezekana kwamba tuhuma zote hizi ni majungu au kumuonea Nyalandu? Hamna tuhuma za kweli hapa? Je, uamuzi aliofanya Nyalandu ni sahihi na unakubalika?

Ukweli ni kwamba, hata kama mabosi wa Nyalandu wanaziona tuhuma zake kuwa ni majungu na wanakubaliana na uamuzi wote aliofanya, ni vema wajue kuwa tayari uamuzi wake umeanza kuleta athari kubwa katika uchumi.

Je, wakubwa hawajui kuwa tayari Marekani, ambalo ni soko kubwa la nyara zinazotokana na uwindaji wa kitalii, wamepiga marufuku nyara za baadhi ya wanyamapori kutoka Tanzania na kuwashauri watu wake kufuta safari na kwenda kwenye nchi nyingine?

Je, wakubwa hawajui kuwa ulinzi wa wanyamapori wetu unategemea sana fedha zinazotokana na uwindaji wa kitalii? Je, Hazina wataielewa Wizara itakaposhindwa kuwasilisha mapato kama ilivyopangiwa? Hili ni bomu na si muda mrefu litalipuka. Tusubiri.

Wengi kwenye magazeti na mitandao ya kijamii wamekuwa wanashangaa kwamba Nyalandu kwa tuhuma alizo nazo, amewezaje kupenya hadi kufikia ngazi za unaibu waziri na sasa waziri kamili! Wengi wameishia kuvilaumu vyombo vya usalama kwa kumpotosha Rais au vyombo hivyo kuwa na maslahi binafsi kupitia kwa Nyalandu. Kama hili ni kweli basi tumekwisha!

Wengine wanadai kuwa Nyalandu ana kismati (bahati tu). Wanahoji, ile vetting iliyopaswa kufanywa kwa watu wanaokabidhiwa majukumu nyeti imeishia wapi? Kama ilifanywa, walishindwa vipi (Usalama wa Taifa) kuyajua haya?

Binafsi nitaelekeza mshangao wangu kwa mabosi wa Nyalandu kwa kushindwa kumchukulia hatua au hata kukemea uamuzi tata ambao tayari umeliingizia Taifa hasara ya mabilioni. Kwa mfano, hivi jaribio la kutaka kuuza Hifadhi ya Taifa ni kosa dogo kiasi hicho!  Mbona linachukuliwa kama mzaha?

Hebu tujikumbusheni enzi za Mwalimu. Alimvua uwaziri  wa sheria Abdallah Fundikira kwa tuhuma za rushwa. Alimfukuza uwaziri wa mawasiliano, Augustine Mwingira, na Meneja Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), Lawrence Mmasi, baada ya kununua ndege mbovu kwa bei isiyostahili kwa ajili ATC kutoka kwa mfanyabiashara wa Kipalestina, George Hallack.

Alimtimua Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Meli Tanzania (TSC) George Mbowe, kwa kumuuzia mfanyabiashara wa Kihindi, Akberali Rajpar, meli ya Shirika la Meli za Mwambao (TACOSHIL) – mv Jitegemee, kwa bei ya kutupa na kwa mazingira ya kutatanisha. Aliwafukuza kazi Meneja Mkuu wa Shirika la Vifaa vya Elimu (TES), Gervas Chilipweli, na mdhibiti wake wa fedha, Mujibur Rahman, baada ya kugunduliwa kwa hujuma na ubadhirifu mkubwa wa fedha katika shirika hilo.  Alimfukuza kazi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abdulnuru Suleimani, kutokana na malalamiko ya wananchi juu ya kukithiri kwa rushwa katika uongozi wa mkoa.

Hii ni mifano michache tu. Hizi tuhuma na uamuzi wa utata wa Nyalandu hautoshi kumvua uwaziri? Inashangaza zaidi yeye anapogeuka kuwa ndiye mfukuzaji! Ila sasa angalau angefukuza wazembe na majizi. Ajabu ni pale anapofukuza waadilifu na kuajiri watuhumiwa wa rushwa na ujangili!

Hiki kiburi anakipata wapi? Nyalandu amenukuliwa hivi karibuni akiapa kuwa lazima Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi; ang’oke na kwamba tayari amemwambia mkuu wa nchi na ameahidi atamuondoa karibuni! Hapa ndipo ninapopata shaka. Kwa kosa gani? Nyalandu anatuhumiwa kumhujumu Waziri makini, Khamis Kagasheki na hatimaye akafanikiwa kumng’oa!

Baada ya hapo kawang’oa wakurugenzi watatu ambao kwa lugha ya mitaani ni ‘majembe’. Sasa katangaza kumuondoa Mama Tarishi ambaye siyo siri kwamba ni “Iron Lady” kutokana na uadilifu, umakini na kufuata kwake sheria, kanuni na taratibu. Je, katika Wizara hii kunatakiwa watu wa namna gani? Muda si mrefu Wizara hii itashikwa na majangili kwenye kila idara.

Ukifuatilia mitandao ya kijamii juu ya yale yanayojiri ndani ya Wizara hii, kuna madai na hisia nyingi zinazojitokeza miongoni mwa wanajamii zikijaribu kuonesha kinapotoka kiburi cha Nyalandu. Na hapa ndipo niliposema kuwa kama yanayotokea na kuandikwa kwenye mitandao na magazeti Rais hafikishiwi na wasaidizi wake, basi ni kutokutenda haki kwake, familia yake, chama chake, Watanzania na Taifa zima.

Hii inatokana na ukweli kuwa wapo wanaothubutu kumhusisha Mheshimiwa Rais wetu, familia na chama chake na kashfa hizi za Nyalandu. Kwamba si rahisi kuchukua hatua kwa kuwa yeye na Nyalandu lao moja!

Kwa bahati mbaya sana, mara kadhaa Nyalandu mwenyewe amekuwa anajinadi kuwa ana uhusiano wa karibu na Mkuu wa nchi na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Si uhusiano wa kiutendaji, bali uhusiano binafsi.  Na hata baadhi ya uamuzi tata aliofanya anadai kuagizwa na wakuu hawa, japo inapokuja kutangazia umma hasemi hivyo!

Kwa mfano, suala la kuwaondoa kazini wakurugenzi wa wanyamapori na yule wa Bodi ya Utalii anadai kuagizwa na Rais. Rais atakuagiza vipi ukafukuze watu aliowateua yeye? Kwani hawezi kuwafukuza mwenyewe? Mbona haya maagizo asiyatoe kwa Wizara nyingine? Lakini hata kama Rais kakuagiza, kakuagiza ufanye hivyo kwa kukiuka sheria na kusema uongo?

Jingine ni lile la kwenda Afrika Kusini yeye na rafiki yake Lembeli ‘kuiuza’ Hifadhi ya Katavi. Pamoja na kuonywa na wataalamu kuwa wanunuzi ni matapeli, alilazimisha kuwa lazima aende kwa kuwa yalikuwa maagizo ya Waziri Mkuu. Nataka kuamini kuwa kama kweli Waziri Mkuu aliagiza hilo, basi itakuwa imetokana na Nyalandu na Lembeli kumpotosha kwa makusudi.

Nina hakika angeelezwa utata wa African Parks Network (APN), kamwe asingekubaliana na upuuzi huo na asingebariki ziara hiyo ambayo tunaambiwa kuwa walienda watu watano kwa siku nne, eti kuwajulisha APN kuwa Tanzania haina mpango wa kubinafsisha hifadhi!

Nikinukuu maneno ya mmoja wa waandishi – hivi inaingia akilini kuambiwa kuwa “binti kachumbiwa, wazazi watokee kumkataa mchumbiaji, na kisha wazazi hao waungane na wasindikizaji kadhaa wafunge safari ndefu na kwa gharama kubwa kwenda kumwambia mchumbiaji kuwa hatamuoa binti yao?”

Pamoja na kuhusishwa viongozi hawa wakuu na kashfa za Nyalandu, wapo wanaodai kuwa Nyalandu kafikia hapo alipo kwa kupigiwa chapuo na rafiki yake ambaye ni mtoto wa Mheshimiwa Rais wetu. Hisia za watu ni kwamba uteuzi wa baadhi ya viongozi wa Serikali unafuata uamuzi wa kifamilia zaidi badala ya taratibu zilizowekwa kiserikali!

Kashfa za Nyalandu pia zinakigusa Chama Cha Mapinduzi. Wapo wanaodai kuwa kapewa kazi maalum ya kukusanya fedha kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao! Kwa hiyo uamuzi anaofanya una baraka zote za chama na ndiyo sababu ya kiburi chake.

Inadaiwa kuwa upendeleo aliofanya kwa matajiri wa uwindaji wa kitalii na kurefusha muda wa msimu wa uwindaji, ahadi ya kuongeza umiliki wa vitalu kutoka miaka mitano hadi 15, kusita kuwakamata majangili papa ambao yeye mwenyewe amekiri kuwafahamu na mengineyo; yanalenga kuhakikisha kuwa wahusika wanachangia chama vilivyo kwenye Uchaguzi Mkuu ujao!

Yote haya ni hisia za wananchi. Zinaweza kuwa na ukweli au zisiwe na ukweli. Hisia hizi zimezua mdahalo kwenye moja ya mitandao ya kijamii. Hata hivyo, upande unaokataa hoja unaelekea kulemewa kutokana na kukosa jibu mujarabu kuwa kama Rais, familia yake na chama havihusiki na kashfa za Nyalandu, mbona hachukuliwi hatua? Nyalandu anajiamini nini kiasi cha kudai kuwa tayari kamshauri Rais amuondoe Katibu Mkuu na kwamba hili tayari limekubaliwa?

Inawezekana kabisa kuwa kashfa hizi hazina mkono wa Rais na kwa kiasi kikubwa napenda niamini hivyo. Ninachoona mimi ni kwamba pengine Mheshimiwa Rais amejiridhisha kuwa miezi 20 iliyobaki ni michache mno kufanya mabadiliko na kuweka waziri mwingine. Kwamba afadhali avumilie amalize ngwe yake!

Hata hivyo, napenda kumkumbusha Rais wangu kuwa muda huo ni mrefu mno kuruhusu uharibifu kwa Taifa zima na kumwacha yeye mwenyewe na madoa ambayo hayatafutika ndani ya kizazi hiki na vizazi vijavyo. Kwa maneno mengine, gharama ya kuendelea naye ni kubwa mno kuliko gharama ya kumuondoa sasa.

Kama katika kipindi cha miezi miwili tu aliyoteuliwa ameweza kutumia mamilioni ya Serikali kuliletea aibu kubwa Taifa kupitia waandishi wa kigeni kama kina Martin Fletcher na BBC, atashindwaje kuleta uharibifu katika kipindi cha miezi 20 iliyobaki? Kama katika kipindi hiki kifupi amefanikiwa kuifanya Marekani ipige marufuku kuingizwa nyara za uwindaji kutoka Tanzania, tuna matumaini gani naye katika miezi 20 ijayo?

Mheshimiwa Rais, hivi anajua kuwa sasa hivi ujangili ndiyo umepamba moto zaidi? Anajua kwamba ni muda sasa, pesa kwa ajili ya doria na matumizi mengine hazijapelekwa vituoni? Na kwamba badala yake, waziri wake yuko bize safarini nje ya nchi au kwenye vyombo vya habari akitangazia umma kuwa ujangili umepungua, atakamata majangili wote, Operesheni Tokomeza itaanza tena, utafanyika mkutano wa kimataifa Serena kujadili ujangili wa tembo, Serikali imepata misaada ya kupambana na ujangili nk! Haya yote yana tija gani zaidi ya kutaka kuuhadaa umma kuwa ni mchapakazi?

Hivi kipaumbele katika vita dhidi ya ujangili ni kuweka mabango uwanja wa ndege, kuitisha mkutano wa mamilioni Serena, kumgharimia Fletcher kuja kutuvua nguo au kuhakikisha kuwa fedha za doria zinafika vituoni kwa wakati?

Mheshimiwa Rais, kwa mtindo huu tembo watatoweka nchini kabla ya yeye kustahafu. Na sijui kuwa hili litatenganishwa vipi na historia yake. Tungependa jina lake lije kuandikwa kwa wino wa dhahabu. Nyalandu ni tatizo kubwa.

3414 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!