Wiki iliyopita, Dk. Khamis Zephania alieleza vyanzo na madhara ya magonjwa ya saratani ya tumbo na vidonda vya tumbo kwa mama wajawazito. Sasa mfuatilie zaidi katika sehemu hii ya 16…


 

Jinsi vidonda vya tumbo vinavyochunguzwa


Kuna mamilioni ya watu duniani — wanaume kwa wanawake — wanaoishi na vidonda vya tumbo. Hata watoto wadogo wanaweza kupata vidonda vya tumbo. Lakini asilimia kubwa ya watu hawapati vipimo. Watu huchukulia tu kwamba wana vidonda vya tumbo.

Kwanza, daktari atachukua historia ya dalili zako na vipengele hatari, ikiwa ni pamoja na lini ulikuwa na tatizo la kutosagika kwa chakula na maumivu; jinsi gani maumivu yalivyo; kama hivi karibuni umepoteza uzito; ni dawa gani ulikuwa unatumia; tabia yako juu ya uvutaji na unywaji; na kama kuna mtu yeyote katika familia yenu ana vidonda vya tumbo.

Daktari atatazama tumbo na kifua, pia na rektamu kuona kama kuna dalili ya kutoka damu. Pia, anaweza kukupima kama una upungufu wa damu (anaemia).

Kama hakuna dalili yoyote ya damu na dalili zako si kali, daktari anaweza kukushauri dawa ambazo hupunguza asidi ya tumbo.

Maelezo ya mgonjwa mara nyingi humfanya daktari aweze kufahamu kuwa mgonjwa ana vidonda vya tumbo au la.

 

 

Lakini, kama dalili zako zitakuwa kali licha ya kutumia dawa, vipimo zaidi vitahitajika. Baadhi ya vipimo vitachukuliwa ili ithibitike kwa uhakika kama ni vidonda vya tumbo. Vipimo hivi ni kama vile kipimo cha damu, kipimo cha pumzi, kipimo cha choo (stool antigen test), upper GI X-Ray, na endoscopy.

 

 

Kipimo cha damu (blood test): Kipimo cha damu kinaweza kutambua kama bakteria H. pylori yupo. Hata hivyo, kipimo hiki hakiwezi kutambua kama katika siku za nyuma mgonjwa alikuwa na vidonda vya tumbo au kaathiriwa kwa sasa.

 

 

Pia, kama mtu alikuwa anatumia antibiotics au proton pump inhibitors, kipimo cha damu kinaweza kutoa majibu yasiyo sahihi.

Kipimo cha pumzi (breath test): Kipimo kingine kinachoweza kupima vidonda vya tumbo ni kipimo cha pumzi kinachojulikana kama breath test. Katika kipimo hiki, atomu ya kaboni mnunurisho (radioactive carbon atom) hutumika kuchunguza H. pylori.


 

Mgonjwa hunywa kikombe cha maji safi kilicho na radioactive carbon kama sehemu ya kitu (urea) ambacho bakteria H. pylori ataivunja. Saa moja baadaye mgonjwa atapuliza ndani ya mfuko uliozibwa. Kama mgonjwa ameathirika na H. pylori, sampuli ya pumzi itakuwa na radioactive carbon ndani ya carbon dioxide.Kipimo cha pumzi pia hutumika kutazama ni jinsi gani matibabu yameweza kumwondoa H. pylori. Kipimo hiki cha pumzi ambacho ni uvumbuzi wa hivi karibuni, kina usahihi zaidi kwa aslimia 95.

 

 

Kipimo cha choo (stool antigen test): Hiki ni kipimo ambacho hutumika kutambua kama H. pylori yumo ndani ya kinyesi. Kipimo hiki pia hutumika kufahamu ni kwa jinsi gani matibabu yamefanikiwa kuondoa bakteria.

 

 

Kipimo cha X-Ray (Upper gastrointestinal X-Ray): Kipimo hiki hutazama umio, tumbo na duodeni. Mgonjwa humeza maji ambayo yana bariamu. Bariamu hufunika eneo la mmen’genyo wa chakula na huonekana katika X-Ray kukifanya kidonda kuwa rahisi kuonekana. Upper GI X-Ray hutumika tu kutambua baadhi ya vidonda.

 

 

Endoscopy: Kwa uangalifu sana, daktari ataingiza mrija mwembamba wenye kamera ndogo sana unaoitwa endoscope chini ya koromeo kupitia umio hadi kwenye tumbo na duodeni. Daktari anaweza kuona sehemu ya juu ya eneo la mmeng’enyo wa chakula kwenye monitor na kutambua kama kidonda kipo.

 

 

Endoscopy hufanywa ikiwa mgonjwa ana dalili kama vile kupungua uzito, kutapika (hasa kama damu inaonekana katika matapishi), choo cheusi, kupungukiwa damu (anaemia) na ugumu wa kumeza chakula.

 

 

Endoscopy inaweza kuwa kwa ajili ya kutambua au kutibu. Madhara ya endoscope ni madogo sana.

 

Matibabu

Kinga: Hii ni njia yenye ufanisi ya kudhibti magonjwa. Kinga hii ni hatua ya kuhakikisha kwamba ugonjwa hautokei kabisa. Ni hatua ya kuepuka kitendo chochote kinachoweza kudhuru afya au kuharibu uhai, na ni hatua ambayo husaidia kufanya kitendo chochote chenye kuleta afya nzuri kama kufanya mazoezi, kupumzika, kula mlo mzuri wenye viinilishe, kufanya ibada na kuleta dhikri, ndoa na familia yenye furaha na amani.

 

Mambo ya kuzingatia ili kujikinga na vidonda vya tumbo: kula polepole, usile harakaharaka; usile huku unaangalia TV, shughulika na kula tu; usiweke chakula kingi mdomoni kwa mara moja, weka chakula kidogo mdomoni na kitafune vizuri kabla ya kumeza, kifurahie chakula mdomoni, hii itaongeza umeng’enywaji mzuri wa chakula.

 

Kula pale unaposikia njaa, kula kidogo kidogo na mara kwa mara hupunguza kujijenga kwa asidi kati ya mlo na mlo. Usifanye kazi nzito baada ya kula; punguza mawazo na ishi maisha ya furaha; usivute sigara; usinywe pombe; usitumie dawa (NSAIDs) kama vile Aspirin kwa muda mrefu; chunga matumizi yako ya kahawa; osha mikono yako kwa maji ya uvuguvugu baada ya kutoka msalani.

 

Itaendelea

 

3634 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!