Leo Alhamisi, Aprili 26, 2018 katika maadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, tumeshuhudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli akitangaza kuipandisha hadhi Manispaa ya Mji wa Dododma kuwa Jiji.

Kutokana na hatua hiyo ambayo imekuwa ya ghafla na ambayo haikutegemewa kutangazwa mapema namna hiyo, watu wengi watakuwa wanajiuliza ni vigezo gani hasa vinavyozingatiwa ili Mji au Manispaa viweze kupandishwa hadhi na kuwa jiji.

Rais ana mamlaka ya kupandisha hadhi ya Mji au Manispaa kuwa Jiji lakini anazingatia sheria pamoja na vigezo ambavyo hutumika katika kupandisha hadhi.

Hivi hapa ni baadhi ya vigezo ambavyo huzingatiwa katika kupandisha hadhi ya mji au manispaa kuwa jiji.

Eneo

Eneo kwa maana ya kilomita za mraba ambapo manispaa husika lilipo, huwa ni kitu muhimu kunachozingatiwa katika kupandisha hadhi na kuifanya jiji. Manispaa ya Dodoma ina ukubwa wa kilometa za mraba 250
ambazo hazina shaka kwa kupewa hadhi ya Jiji. Japo eneo ambalo limetumiwa kwa makazi na shughuli nyingine za kibiashara siyo lote, lakini kulingana na maendeleo ya kila siku, jiji hilo litapanuka na kuwa kubwa zaidi.

Miundombinu

Hapa miundombinu ya kila namna huangaliwa. ni jinsi gani usafiri unapatikana kirahisi katika eneo husika, kwa maana ya barabara, huduma za afya, elimu, pamoja na huduma za kijamii kama vile maji na umeme. Kwa jiji la Dodoma, hakuna shaka kwamba huduma hizi zinapatikana kirahisi na zinaendele kuongezeka na kuboreshwa kila kunapokucha.

Wingi wa watu

Hapana shaka kabisa kusema kuwa Dodoma imekuwa na ongezeko kubwa la watu. Ukianzia wafanyakazi wa serikali waliohamishiwa humo, wakazi waliokuwepo, wawekezaji mbalimbali wanaowekeza, wafanyabiashara na hata watu mbalimbali wanaofuata huduma zilizohamishwa kutoka Jiji la Dar es Salaam kwenda Dodoma. Tumeshuhudia wenyewe makazi mapya yakianzishwa Dodoma jambo linalohihirisha kuwa ongezeko la watu ni kubwa hivyo kufanya idadi ya wakaazi wake kuwa kubwa.

Mapato

Ni kawaida kuwa eneo lenye wingi wa watu, basi na mahitaji mbalimbali huongezeka. Kuongezeka kwa mahitaji kufanya biashara nayo kukua. Kutokana na wafanyabiashara kulipa kodi serikalini kiwango cha mapato nacho huongezeka. Dodoma kwa sasa imezidi kuwa na wafanyabiashara wengi pamoja na watoa huduma wengine mbalimbali ambo wanalipa kodi serikalini. hivyo ni wazi kuwa kiwango cha mapato kimeongezeka jambo ambalo linachangia kuipa sifa ya kuwa Jiji.

Vilevile uamuzi wa kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi ni kigezo tosha cha kuipa Manispaa yake hadhi ya Jiji, serikali yote imehamia Dodoma na hii inatuhakikishia kwamba eneo hilo litakua kwa kasi kubwa.

Hivi ni baadhi tu ya vigezo ambavyo huzingatiwa katika kupandisha hadhi na kufanya eneo kuwa jiji. Vigezo hivi vinaweza kutofautiana kutoka eneo moja hadi jingine hivyo siyo lazima kigezo kilichozingatiwa eneo fulani kifanye kazi sawa katika eneo jingine.

Unadhani vigezo vingine ni vipi? unaweza kuweka comment yako hapo chini.

4232 Total Views 1 Views Today
||||| 3 I Like It! |||||
Sambaza!