Kutoa maoni au uamuzi kuhusu jambo ambalo bado halijatolewa hukumu mahakamani ni kuingilia uhuru wa mahakama, hivyo unaweza kusababisha kupotosha mwenendo wa shauri au kesi iliyopo mahakamani.

Jambo hilo linaweza kutendwa na mtu yeyote kwa kuzingatia masilahi anayopata kutoka upande mmoja anaoupigania au kwa kutokujua sheria inatoa tafsiri gani juu ya shauri lililopo mahakamani, ingawa kisheria jambo la kimahakama lazima limalizwe mahakamani. Makala hii inahusu familia ya watu 13 wanaolala nje kwa zaidi ya siku 26 sasa baada ya kutolewa kwa nguvu na Godfrey Malila aliyejinasibu kuwa amenunua nyumba hiyo kutoka kwenye familia hiyo kupitia nyaraka zao za vikao vya mirathi. Huwezi kuamini lakini ndiyo hali halisi, fuatilia majibu ya maswali kadhaa aliyoulizwa Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye.

JAMHURI: Mkuu wa wilaya, wewe ukiwa Mwenyekiti wa Kamati yaUlinzi na Usalama ya Wilaya unaweza kuueleza nini umma ambao unashuhudia ubabe na nguvu ya pesa inavyobomoa nyumba wakati shauri la kesi hiyo lipo mahakamani na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya mhusika?

DC Nshenye: Ni kweli tatizo hilo lipo lakini si kweli kwamba hatua hazikuchukuliwa kwani aliyekuwa anabomoa, Godfrey Malila, tulimsimamisha kufanya hivyo hadi shauri la msingi litakapomalizika mahakamani.

JAMHURI: Kwa nini usitishaji huo haukwenda sambamba na kurudishwa ndani ya nyumba familia ambayo imetolewa wakati shauri hilo halijamalizika mahakamani kwa lengo la kutenda haki pande zote?

DC Nshenye: Nafikiri ushauri mzuri ni kwenda mahakamani tu. Tulimshauri Mwajuma Omari Mbwana afungue kesi Baraza la Nyumba dhidi ya Godfrey Malila kupinga kutolewa kwa nguvu ndani ya nyumba wakati kesi ya msingi haijakwisha.

JAMHURI: Kwani sheria inasemaje kwa mtu anayeingilia mwenendo wa kesi iliyopo mahakamani?

DC Nshenye: Unajua mimi si mwanasheria halafu mwanasheria anasema kesi iliyopo mahakamani haimtaji aliyenunua nyumba ni kesi ya familia ya mtu na mdogo wake, ndiyo maana sasa tukashauri mambo mawili, yawezekana ikafunguliwa kesi ya namna walivyoathirika ya kumshitaki huyo aliyewatoa ndani ya nyumba lakini pia sura ya pili ifunguliwe kesi ya pingamizi ya kupinga kutolewa ndani ya nyumba, huo ndiyo ushauri ambao tuliutoa.

JAMHURI: Lakini kwa mujibu wa Mwajuma Omary Mbwana, mtoto wa Boko Omary Mbwana anayedaiwa kufariki dunia amesema kesi ya kupinga ilifunguliwa Machi 3, 2018 lakini baraza la nyumba liliwaambia hapana, haiwezi kufunguliwa waiondoe, waliondoe shitaka hilo, hilo limekaaje?

DC Nshenye: Kesi ya kupinga ‘si’ imefunguliwa baada ya kutolewa ndani ya nyumba? Na kama ilifunguliwa kwa nini waiondoe na kama anasema hivyo, wakati anaiondoa aliwasiliana na uongozi wa wilaya? Yawezekana yeye akasema vyovyote anavyosema ili kupata nguvu lakini ninachokuambia mimi kwa maana ya mgogoro kuufikisha ‘si’ ameufikisha juzi hapa kwa hiyo hayo unayoniambia nashindwa kuyaelewa.

Suala la kufungua pingamizi mimi ndiye niliyemshauri na OCD ndiye aliyemshauri, kama ni kamati ya usalama ndiyo iliyomshauri na akafungua kesi ya pingamizi Juni 5, mwaka huu.

JAMHURI: Juni 3, mwaka huu mara baada ya kumsitisha, Godfrey Malila alikwenda tena kwenye nyumba hiyo na kubomoa mlango wa ‘geti’ ambao ulikuwepo na kuweka geti lake ili familia ambayo inalala nje isiingie tena ndani, hili limekaaje?

DC Nshenye: Nilipigiwa simu na mwandishi wa habari, Ngaiwona Nkondora, kunitambulisha jambo hilo na mimi nikatuma polisi kwenda pale walikuta utepe umefungwa wakamwamuru aondoe, lakini kuhusu masuala ya geti kwa kuwa halina madhara yoyote walimruhusu aweke na mimi nilipompigia Kamanda wa Polisi Wilaya ya Mbinga (OCD) alisema ni yeye alimruhusu kuweka geti hilo ili kuimarisha ulinzi ndani ya nyumba yake hiyo.

JAMHURI: Suala la kuruhusu geti liwekwe kwa ajili ya ulinzi wa nyumba na wale wanaolala nje kipi kina thamani?

DC Nshenye: Hilo swali linaweza likawa ni gumu, unaweza ukamuuliza aliyeyelala nje, tumemtafutia nyumba amekataa huku akidai arudishwe kwenye nyumba yake hiyo hadi shauri litakapomalizika, sijui tunafanyaje kwa kesi kama hiyo.

Hivyo kwa kuwa amekubali kukaa nje mpaka kesi itakapokwisha, basi tusubiri kesi iishe, kwa sababu sisi tulitaka wakati anasubiri kesi akae ndani ya nyumba.

JAMHURI: Kipi kilitangulia kati ya kutolewa nje na kesi iliyopo mahakamani iliyofunguliwa na Godfrey Malila kumtaka Mwajuma Mbwana aondoke ndani ya nyumba?

DC Nshenye: Ataingiaje ndani wakati ‘ndani’ ametolewa kwa mujibu wa sheria ambayo imetumika? Alikwishatolewa na amefungua kesi ya kupinga kuondolewa ndani.

JAMHURI: Godfrey Malila alifungua kesi ya kumtaka Mwajuma atoke kwenye nyumba na kesi hiyo haijamalizika na yeye amekwenda kuwatoa kinguvu, kiusalama katika ngazi yako limekaaje hilo mlipokaa kwenye vikao vyenu?

DC Nshenye: Na ndiyo maana tukashauri afungue kesi apinge, na tukamzuia Godfrey Malila asivunje.

JAMHURI: Katika sakata hilo kuna viashiria vya utakatishaji pesa pale uliposema nyumba hiyo imeuzwa kwa gharama zaidi ya Sh milioni 100 wakati ofisi ya ardhi wilayani mwako kupitia mthamini, nyumba hiyo imeonyeshwa ina thamani ya Sh milioni 35 na hati ya mauziano inaonyesha mlipaji amelipa Sh milioni 15, ipi gharama halisi ya nyumba hiyo?

DC Nshenye: Hilo linahitaji uchunguzi, kwa kuwa nimelisikia leo kwa sababu mimi si dalali wa hiyo nyumba na kama ikithibitika nyumba ina gharama ya juu na bei iliyowekwa ni ya chini hilo ni kosa.

JAMHURI: Kikao cha mirathi kwa kesi iliyotolewa hukumu Mahakama ya Mwanzo Mfaranyaki mwaka 2018 imeonekana Mwajuma Mbwana amedai sahihi yake kughushiwa kwa kuwa hakushiriki kikao cha mirathi, hilo unalizungumziaje DC?

DC Nshenye: Mimi nashindwa kukuelewa umesema umewatuma vijana wako na maswali yote unayoniuliza waliniuliza vijana wako na niliwajibu kuwa hilo ni la kiuchunguzi, kwani unaweza kumuuliza mtu wa sheria akasema hilo si sahihi wakati ni sahihi au ukamuuliza polisi akasema ni sahihi wakati si sahihi, lakini ukiniuliza mimi naweza kusema si sahihi wakati kumbe ni sahihi.

Kauli ya wakili wa Malila

Gazeti hili liliwasiliana na wakili wa Gofrey Malila na kumuuliza maswali yafuatayo:

JAMHURI: Wakili Dikson Ndunguru, wakati wa shauri hili kwa mara ya kwanza ukiwa Mahakama ya Mwanzo Mfaranyaki mwaka 2018 ulishindwa kutoa cheti cha kifo cha Boko Omary Mbwana lakini baadaye cheti kilionekana, unaweza kueleza ulikipataje?

Wakili Ndunguru: Cheti kilikuwepo na Boko alifariki dunia katika Kijiji cha Mbingamharule, wilayani Songea na hata Mwajuma analijua hilo.

Kuhusu muhtasari wa kikao cha familia kujadili mirathi Mwajuma alishiriki na aliweka saini ya kuandika na dole gumba hivyo hakuna shida yoyote juu ya hilo.

JAMHURI: Je, raia wa nchi nyingine anaweza kuingizwa kwenye mirathi ya Tanzania wakati yeye si raia wa Tanzania?

Wakili Ndunguru: Inawezekana kama atakuwa raia wa Tanzania lakini akawa safarini nje ya nchi, hivyo anaweza kurudi na kujumuishwa kwenye mirathi.

Kuhusu Joseph Mbwana na Zacharia Omary Mbwana kujumuishwa kwenye mirathi ya familia ya Boko ni halali kwa kuwa amesema wote ni watoto wa marehemu Boko Omary Mbwana raia wa Tanzania.

Pia kuondolewa kwenye nyumba ilikuwa sahihi kwa kuwa aliyefungua kesi Godfrey Malila dhidi ya Mwajuma Omary Mbwana aliondoa shitaka hilo kwa kuandika barua kwenye Baraza la Nyumba na Ardhi wilayani Mbinga.

Kama mfungua kesi ameandika barua ya kuondoa shitaka mahakamani sasa ni nani atapinga hilo wakati sheria ipo wazi mfungua kesi akiondoa ni mwisho wa kesi.

Naye Wakili Eliselius Ndunguru ambaye alikuwa wa kwanza kusimamia kesi hiyo akiwa upande wa Mwajuma alieleza aliposoma maelezo ya upande wa pili akagundua kwamba wao wanasema hiyo nyumba ameuza msimamizi wa mirathi lakini alipomuuliza Mwajuma, baba yake alifariki dunia lini, ndipo akagundua hakuna ushahidi kwamba amefariki dunia.

“Tukiwa Mahakama ya Mwanzo Mfaranyaki, Songea nilieleza mahakamani kuwa kuna utata kama huyu mtu amefariki dunia au yupo hai, katika kesi hiyo hapo Mahakama ya Mwanzo aliombwa msimamizi wa mirathi lakini hakutokea na badala yake alimtuma mwakilishi kijana mmoja anaitwa Damas Ngai na ndipo nilimshauri Mwajuma apinge kwani kisheria lazima afike msimamizi wa mirathi mwenyewe,” alisema Wakili Ndunguru.

Lakini katika hatua za mwanzo amesema cheti cha kifo hakikuwahi kuonekana hivyo ni kweli kina Godfrey Malila walishindwa kuonyesha cheti cha kifo na hata alipomhoji wakili mwenzake Ndunguru, huyu mtu aliyedaiwa amekufa ushahidi wake upo wapi, Ndunguru alijibu hakuna anayejua alikufa lini lakini kwa kuwa hakuonekana muda mrefu ndiyo maana tunaendelea na kudhani kuwa amefariki dunia (presumption of death).

Anasema alimshauri Mwajuma aombe Mahakama ya Mwanzo impatie cheti cha kifo lakini hakupata cheti hicho kwa wakati na baada ya muda alipewa na kikisomeka kuwa alikufa akiwa Kijiji cha Mbingamharule, mwaka 1990.

Kwa upande wake Mwajuma anaeleza watoto hao wawili si watoto wa baba yake Boko kwa kuwa mama yake mzazi Joyce Injima alikwenda Msumbiji na kaka yake Saidi Omary Mbwana, hivyo hao wawili amezaa na baba yake wa kambo huko Msumbiji na hao watoto ni raia wa Msumbiji.

Mwajuma amesema hajawahi kushirikishwa kwenye kikao cha mirathi na hata saini ya kuandikwa na ile ya dole gumba si zake na yupo tayari serikali iwatumie wataalamu wa alama za vidole kujiridhisha kwamba saini hizo zimeghushiwa.

“Pia katika muhtasari wa mirathi huyo aliyejitambulisha kuwa Mohamed Said Muzuri ni mdogo wa baba yetu Boko si kweli, huyo ni binamu ya baba na alikuwa anafanya kazi kwa Godfrey Malila, amejengewa nyumba na Malila kwa ahadi ya kumfanikishia kuipata nyumba hiyo kwa njia yoyote na ndiyo maana ametoroka Mbinga.

“Ni kwamba walikwenda kwenye uongozi wa wilaya lakini hawakupata ushirikiano na OCD wa wakati huo alipiga hadi mabomu ya machozi kutawanya watu na ndipo ulipoanza ugonjwa wa baba yake mdogo, Nassoro Mbwana, hadi leo na hiyo ilitokana na mnunuzi wa nyumba Godfrey Malila kudaiwa kumwaga fedha kwa baadhi ya viongozi wa serikali,” amedai.

Mwajuma anasema cha kushangaza zaidi ilipofika Juni 27, mwaka huu, Godfrey Malila alipokwenda kwenye nyumba yao na kuingia uani ambako walikuwa wanalala na kuanza kubomoa huku kesi aliyoifungua yeye mwenyewe dhidi yao ya kuwataka waondolewe kisheria ilikuwa bado haijamalizika, lakini hakuchukuliwa hatua yoyote kutokana na kuingilia kesi iliyokuwa inaendelea mahakamani.

“Mimi nilijua walipomsitisha kubomoa sisi tungerudishwa ndani ya nyumba hadi kesi ya msingi itakapomalizika lakini haikuwa hivyo, kwani aliendelea kulindwa na baadhi ya viongozi wa serikali wilayani Mbinga kwa kuwa suala la kubomoa si la mahakama bali ni la kijinai,” amesema huku akitoa mchozi Mwajuma.

Anaeleza kesi hiyo namba 56 ya mwaka 2018 ilifunguliwa Mahakama ya Mwanzo Mfaranyaki,  Songea kupinga kesi namba 56 ya mwaka 2017 ya kumteua msimamizi wa mirathi, Said Omari Mbwana, kwa kuwa hakuna taarifa za kifo cha baba yao.

Anasema kesi hiyo ilitupiliwa mbali kwa kilichoelezwa kwamba maelezo ya mlalamikaji Mwajuma hayakuwa na “mashiko” ndipo Mwajuma alipoamua kukata rufaa Mahakama ya Wilaya Songea na kuanza kumtafuta baba yake.

Mwajuma anaeleza kuwa cheti cha kifo kinaonyesha baba yao Boko Omary Mbwana alifariki dunia mwaka 1990 katika Kijiji cha Mbingamharule, Songea ambako alikwenda na kuelezwa na afisa mtenda wa kijiji kwa barua ya Novemba 15, 2018 kuwa hawajawahi kushiriki msiba ama kumzika Boko kijijini hapo.

Mwajuma aliondoka hadi Iringa nyumbani kwao Tanangozi, mwaka 2002, huko wakajibiwa na uongozi wa serikali ya kijiji kuwa Boko alikuwepo mwaka huo na nyumba yake wakaonyeshwa lakini waliambiwa yupo Migoli, jirani na Mtera ambako walikwenda na kuonana na uongozi wa serikali ya kijiji hicho.

Katika barua ya kijiji hicho ya Juni 29, 2018 iliyosainiwa na afisa mtendaji wa kijiji waliambiwa wanamfahamu na shughuli zake za biashara ya samaki na “hakai” sehemu moja.

Hivyo waliporudi Songea ndipo walifungua kesi ya kupinga mirathi ya baba yake dhidi ya ndugu aliyeuza nyumba hiyo wakishirikiana na mama yake mzazi ambaye anaishi Msumbiji na ‘mume’ mwingine na ana watoto naye wawili.

Afisa Ardhi katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Francy Kaganda, anasema nyaraka iliyotolewa mara ya mwanzo kwa Boko Omary Mbwana ilikuwa ya muda mfupi ambao hata hivyo hakuutaja, hivyo baada ya kupigiwa hesabu za gharama za umiliki kwa aliyenunua Godfrey Malila, ndipo aliandaliwa hati kwa mujibu wa sheria ambapo hatimiliki hiyo ilianza rasmi Julai Mosi 2018 na itadumu kwa miaka 33.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Mbinga alishughulikie suala hilo kwa mujibu wa sheria bila kuingilia muhimili mwingine.

Godfrey Malila, mfanyabiashara wilayani Mbinga alipopigiwa simu na mwandishi wa habari amejibu kuwa mkuu wa mkoa hana mamlaka na suala lake na mkuu wa wilaya haliwezi, kwa sababu yeye si mahakama.

“Mimi nitaisikiliza mahakama peke yake, lakini si mtu mwingine yeyote, kwa sababu nyumba hiyo ni yangu, nina hatimiliki,” anasema Malila.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Simon Maigwe, amesema jeshi hilo halihusiki na kesi ya madai, hivyo kushirikishwa katika kadhia hiyo si sahihi kwa kuwa walishauriwa hivyo na mwanasheria wa serikali.

Mwenyekiti wa Baraza la Nyumba na Ardhi Mbinga, Jesca Raphael, Juni 13, mwaka huu alifanya uamuzi wa kusogeza mbele hadi Julai 5, mwaka huu pingamizi alilofungua Nassoro Omary ambaye ni baba mdogo aliyemlea Mwajuma akiwa na miaka mitano hadi sasa baada ya kuachiwa na kaka yake kupinga kuondolewa kwenye nyumba. Kwa hiyo familia hiyo itaendelea kulala nje ya nyumba hadi Julai 5, mwaka huu.

613 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!