Kuna habari kwamba vijana 2,000 wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA) walikuwa wanafanya juu chini kuzuia Mkutano Mkuu wa CCM Dodoma usifanyike.

Hii ni baada ya vijana hao wa Bavicha kuona kwamba wakati mikutano ya siasa imepigwa marufuku kambi ya Upinzani, chama tawala kinapewa uhuru na nafasi ya kufanya mikutano hiyo.

Sisi sote tunajua mazingira ya nchi yetu ya Tanzania. Katika jambo hili la Bavicha kukusudia kuzuia mkutano wa CCM usifanyike kuna mambo mawili.

Kwanza, si Bavicha tu bali pia Chadema yenyewe itaonekana inataka kuleta vurugu nchini, huku ikifumbiwa macho sababu iliyoifikisha hapo. Jambo la pili, itaonekana kwamba vijana wa Chadema wanatumiwa na viongozi wa chama chao kana kwamba wao wenyewe hawawezi  kujiamulia mambo.

Tuliosoma wakati wa mkoloni tuliambiwa kwamba wanafunzi tulikuwa raia wa kesho, kwa hiyo hatukutakiwa kujihusisha na masuala yaliyohusu maisha yetu na jamii.

Lakini leo mambo ni tofauti. Tunakubaliana kwamba vijana wa nchi hii ni raia wa leo, ndiyo maana wakifikia umri wa miaka 18 wanaweza kupiga kura, tena baada ya kushiriki mikutano ya siasa ya kampeni. Na wakifikia umri wa miaka 21 wapo huru kugombea ubunge au udiwani.

Hi maana yak e ni kwamba tayari vijana wetu wa leo ni wanasiasa na wana haki ya kufanya siasa bila kutumiwa na mtu yeyote.

Historia yaTanzania inaonesha kwamba vijana walikuwa mstari wa mbele katika kutumikia makabila yaliyotulea bila kutumiwa na viongozi wa jamii.

Katika vita ya kikabila, baadhi ya makabila wapiganaji watu wazima waliruhusiwa kutumia bangi walipokuwa wanakwenda uwanja wa mapambano kuwatoa woga, lakini vijana walipigana bila kulazimika kutumia bangi. 

Vijana wa Kimaasai morani ni walinzi kamili wa jamii zao na mali ya jamii. Wanajua wajibu wao kwa jamii na wala si suala la kusema kwamba wanatumiwa na viongozi.

Wakati wa Mjerumani, Wahehe walipopinga uvamizi wa Wajerumani alikuwa kijana aliyemuua kamanda wa kikosi cha Wajerumani kilichokuwa kinakwenda kuvamia Kalenga, makao makuu ya Mkwawa, mwaka 1891.

Kwa kuwa kamanda huyo wa Wajerumani, Emil Von Zelewsky, alizoea kujiita ‘Nyundo’, basi Mkwawa, kiongozi shupavu wa Wahehe, alimrithisha kijana yule jina la ‘Nyundo’.

Wakati wa harakati za kudai uhuru zilizoongozwa na chama cha TANU, vijana wa TANU walijituma sana. Waliandaa mikutano ya hadhara, waliimba nyimbo za siasa kwenye mikutano hiyo, walikusanya michango ya TANU kwa uaminifu mkubwa, waliwafundisha watu wazima kusoma na kuandika na walipeleleza nyendo za wapinzani wa TANU.

Vijana wa kike wa TANU walifichua mbinu mbalimbali za wapinzani wa TANU ambazo hawakuweza kufichua vijana wa kiume. Matokeo yakafanikiwa ingawa jeshi la polisi lilikuwa limeanzishwa mwaka 1916, halikuwa na polisi wa kike, mkoloni aliona kazi nzuri iliyokuwa inafanywa na vijana wa kike wa TANU. Kwa hiyo, aliamua kuanzisha kikosi cha polisi wa kike mwaka 1959.

Azimio la Arusha lilipotangazwa Februari 1967 walikuwa vijana wa Shule ya Sekondari ya Tanga waliojituma bila kuagizwa kuanzisha safari za miguu za kuunga mkono Azimio la Arusha ambapo walisafiri kwa miguu kutoka Tanga mpaka Dar es Salaam wakiongozwa na Hamisi Semfuko.

Kule Marekani tunajua kuna vijana wamejitokeza kwenda kutumikia watu wengine nje ya Marekani (US Peace Corps) mpaka Umoja wa Mataifa ukaamua kuanzisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Watu wa Kujitolea.

Sasa tuangalie kwa ufupi chanzo cha kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Julai 10,1963. Ilikuwa Agosti 25, 1962 vijana wa TANU waliokutana Tabora walipoazimia kuitaka Serikali ianzishe chombo cha kushirikisha vijana katika ujenzi wa Taifa. Ilikuwa katika mazingira hayo Rais Julius Nyerere alipozindua rasmi jeshi hilo mwaka 1963 alisema, “Umuhimu wa JKT unatokana na Taifa kuhitaji huduma za vijana, na vijana kuitikia wito huo wa kulitumikia Taifa lao kwa jukumu lolote lihitajiwalo”.

Nako huko kwenye vyama vya siasa, huduma za vijana zinahitajika kama zilivyohitajika wakati wa TANU, na vijana wapo tayari kutumikia vyama vyao. Hawatumiwi na viongozi wa vyama hivyo.

Na kwa upande wa Upinzani kila baya wafanyiwalo wapinzani vijana wa vyama, hivyo linawagusa pia. Maji ya upupu humwagiwa wote – watu wa wazima na vijana. Kukatazwa kufanyika shughuli za siasa huzuiwa wote.

Ukweli ni kwamba vijana wanazijua vizuri zaidi haki zao za kisiasa na za kijamii kuliko wanavyojua watu wazima. Kwa hiyo, huzipigania zinapokiukwa. 

Serikali na Jeshi la Polisi wakiupuuza ukweli huu, watajikuta wanaiingiza nchi kwenye matatizo na mgawanyiko. Twende tusubiri.

By Jamhuri