Siku zilizopita katika Safu hii, niliwahi kuzungumzia Azimio la Arusha, dira iliyoaminika ingewapeleka na kuwafikisha Watanzania kwenye Ujamaa kamili chini ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Kwa kweli kwa miaka ile ya kuanzia mwaka 1960 hadi mwaka 1990, Azimio lilistahili kuwapo, kwani nchi ilikuwa katika harakati za ukombozi; ukombozi wa kiafikra, kisiasa, kiuchumi, kiutawala na kiutamaduni.

Mabadiliko ya siasa duniani na hasa Azimio la Zanzibar la Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1990 yaliyotaka masharti ya uongozi yawahusu pia wananchi wanaoongozwa, na viongozi kulegezewa ili nao wapate kushiriki mambo ya biashara; kwa maana ya uchumi binafsi.

 

Wananchi walianza kuonesha dalili za kutopokea, na viongozi kuanza kushabikia na kushirika katika biashara na kuyapa kisogo masharti ya uongozi. Azimio la Arusha likaenda na maji.

 

Azimio la Arusha katika umri wake wa miaka 25 yaani robo karne si haba, limefanya mambo mengi chini ya kaulimbiu yake moja kubwa iliyosema “Ili tuendelee tunahitaji vitu vine” — Ardhi, Watu, Siasa Safi na Uongozi Bora.

 

Nasema bila woga wala soni, asilimia 65 ya maendeleo ya watu na vitu yalipatikana na kutia moyo. Asilimia 35 mambo hayakuwa mazuri na yalihuzunisha. Lakini yote hayo ndiyo majambo ya safari yoyote. Hakuna safari isiyo na mazonge mazonge.

 

Watanzania hasa wazalendo walilipenda sana Azimio lao. Waliandamana nchi nzima kuliunga mkono lilipotangazwa. Wasanii mbalimbali katika vikundi vya ngoma, kwaya na michezo waliimba na kulisifu. Wanamuziki wa Bendi ya Nuta Jazz (sasa Msondo Ngoma) walichombeza na kuimba:

 

“Twakusifu sana rais wetu, na mawaziri wote wowowo! kaskazini na mashariki nzima, twatoa sifa wowowo! Na makabwela wote, tuko nyuma yako, sisi sote wowo kwa kukusikiliza, Atakayekataa azimio lako ohh! adui wa Tanzania, Sisi sote woo! Twakubali woo Azimio woo! Atakayepinga Azimio lako woo ni bepari woo!

 

Nia yangu ni kuwakumbusha vijana wa zamani na kuwajuza vijana wa leo. Azimio lilikuwa na nguvu na lilipendwa sana na wazalendo. Ingawa sasa halipo na haliwezi kurudi. “Anahitajika mtu mwendawazimu labda kulirudisha,” ni maneno ya Mwalimu Julius Nyerere.

 

Ninachotaka kueleza katika makala haya ni vile vitu vinne ambavyo Azimio la Arusha limevitangaza kwamba ni muhimu katika maendeleo ya Mtanzania. Siasa Safi na Uongozi Bora vimeachwa na vimetupwa na Watanzania wenyewe; ambao wamekubali kufuata ushauri na masharti ya watu wa ughaibuni.

 

La ajabu; wale waliopinga Siasa Safi na Uongozi Bora leo ndiyo  vinara wakubwa walio mstari wa mbele kuhubiri demokrasia na utawala bora, na wameshikilia bango lenye maneno ‘Mfumo wa Utandawazi’.

 

Mtanzania, kumbuka na tambua vitu vilivyobakia ni ardhi na watu ambavyo ni mali, mtaji na nyenzo kubwa ya kuleta maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii. Iwe katika Siasa ya Ujamaa, ubepari au mfumo wa utandawazi. Tanzania imo katika matumizi ya ardhi na watu, na imeridhia ushauri na masharti ya mfumo wa utandawazi.

 

Wiki mbili zilizopita, vyombo vya mawasiliano na umma vimetufahamisha kuwa wanakijiji wa Gama Makaani, Kata ya Magomeni na wakazi wa Kijiji cha Mihunga, Kata ya Miono, wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, kwa wakati tofauti wametoa vilio vyao kwa Serikali kuhusu maeneo yao ya ardhi kuchukuliwa na wawekezaji.

 

Wanavijiji hao wanasikitika na kuhofu — wao na vizazi vyao kukosa maeneo ya kilimo na shughuli za kiuchumi. Serikali inatakiwa kuondoa hofu hiyo kwa umakini.

 

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto (Chadema), amenukuu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh, ikisema viwanja vilivyopimwa kugawiwa watu hawakupewa hati. Zaidi ya viwanja 7,342 ni vya mashaka na viwanja 160 vya Dar es Salaam vyenye thamani ya Sh. 555 milioni vimegawiwa kwa viongozi na maafisa wa ardhi wenyewe.

 

Juzi juzi, Waziri wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Terezya Huviza, amekaririwa na vyombo vya mawasiliano na umma, akiwataja baadhi ya wabunge, viongozi wa dini na wafanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam kuwa ni vinara wa uvamizi na uuzaji wa viwanja jijini.

 

Amezungumza hayo alipotembelewa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, Ofisi ya Baraza la Mazingira (NEMC).

 

Hayo ndiyo maajabu ya utawala tulionao kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa, kuanzisha na kuendeleza migogoro, wizi na ubadhirifu katika mgawano na matumizi ya ardhi kwa wananchi.

 

Naiomba na kuishauri Serikali iwe kali kwa watendaji wake wa ardhi wanaofanya matendo hayo, ambayo ni kinyume cha kanuni na sheria za ardhi. Washtakiwe na kuhukumiwa.

 

Namalizia kwa kusema hali si nzuri mijini na vijijini. Tabia ya kuoneana soni, kutetea maovu, kushadadia na kuendeleza dhuluma dhidi ya wananchi wenye ardhi yao iachwe, ikomeshwe na izimwe.

 

Vyombo vya kukamata wahalifu, vya sheria na kuhukumu kwa nini visitumike ipasavyo? Wahenga wamesema ikiwa kilemba kwenye rasi kina matope, shuka kiunoni ina hali gani?

973 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!