Tumeambiwa kwamba Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) limesitisha mashindano ya Miss Utalii baada ya kuona uendeshaji wa mashindano hayo umekosa uzalendo na hauzingatii utamaduni wa Tanzania.

Katika siku chache zilizopita suala la uzalendo limezungumziwa vya kutosha. Uzalendo, kwa maana yake halisi, ni hali ya mtu kuipenda nchi yake hata anakuwa tayari kuifia.

Vile vile tumemsikia Leticia Nyerere, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), akizungumzia wananchi wengi katika Tanzania yetu ya leo walivyokosa uzalendo kiasi cha kupuuza utamaduni wa Tanzania, hata wametenda mambo yasiyo ya kawaida.

Tumemsikia Rukia Ahmed, Mbunge wa Viti Maalum (CUF), akitaka mashindano ya urembo yaliyopewa jina la ‘Miss Tanzania’ yafutwe kwa kuwa hayana tija na yanakosa uzalendo. Leticia Nyerere alitoa mifano mbalimbali kuthibitisha watu mbalimbali wasivyozingatia uzalendo na utamaduni wa Tanzania.

Kwa mfano, alisema kwamba siku hizi wanafunzi wengi wa shule wana tabia ya kukaa kwenye viti ndani ya daladala huku watu wazima na wazee wakiwa wamesimama na wananing’inia. Pia alisema kwamba majina ya marais wa Tanzania waliopita hayatajwi kwa heshima.

Kwa bahati mbaya kila jambo baya linalokea katika nchi yetu haraka haraka watu humnyooshea mkono Rais Jakaya Kikwete. Kumnyooshea mkono rais au kiongozi wa nchi kwa jambo ambalo hahusiki nalo pia ni kukosa uzalendo, maana uzalendo ni pamoja na kumpenda na kumheshimu kiongozi wa nchi.

 

Tumesikia watu mbalimbali wakiwazungumzia mawaziri wasiofanya vizuri wanaoitwa “mawaziri mizigo”. Watu wengine wanadai kuwa mtu wa kulaumiwa ni rais aliyewateua mawaziri hao. Swali la kujiuliza hapa ni je, kwani rais amewazuia wasifanye vizuri?

 

Hivyo ndiyo hali halisi ya mambo katika Tanzania yetu ya leo. Uzalendo, heshima na nidhamu ni vitu ambavyo vinaendelea kututoka kwa kasi kubwa!

Kama mawaziri wote wangekuwa wabovu basi tungekubaliana kumnyooshea mkono rais. Lakini kuna hawa akina Magufuli na Mwakyembe wanaofanya kazi nzuri inayomvutia kila mwananchi. Je, na hawa hawakuteuliwa na rais huyo huyo?

Tufike mahali tukubaliane kwamba mawaziri wasiofanya vizuri ni viongozi walioshindwa kujituma, ni hao wenyewe waliokosa uzalendo na wala si mtu aliyewateua. Aliyewateua alikuwa na nia njema.

Tumesikia wabunge wakifanya vurugu bungeni, kitendo kinachodhalilisha Bunge na nchi kwa jumla. Hayo ni matokeo ya baadhi ya wabunge kukosa uzalendo kiasi cha kutoona vibaya kuidhalilisha nchi.

Tumeshuhudia viti vingi bungeni vikiwa wazi. Havina wabunge wa kuvikalia. Wakati mwingine tumesikia pia kwamba kati ya mawaziri 50 (wakiwamo naibu mawaziri) wanaoonekana ni watatu katika vikao vingine vya Bunge.

Si kweli kwamba mawaziri hao wote na wabunge wanaokosekana wanakuwa na kazi muhimu za kufanya nje ya Bunge. Ni kundi la watu lililokosa uzalendo hata hawaoni sababu ya kuwawakilisha watu wao bungeni.

Maana anafika mahali mtumishi wa kawaida wa Serikali anajiuliza, “Kama mawaziri wanaolipwa mishahara minono wanakuwa watoro kwa nini na mimi nisiwe mtoro?”

Tukitaka kusema kweli, tutakubaliana kwamba uzalendo katika nchi yetu umetoweka kwa sababu viongozi wameshindwa kuonesha uzalendo wao mbele ya umma.

Ni katika mazingira hayo viongozi mbalimbali katika nchi hii, katika ngazi zote za uongozi wana haki ya kulaumiwa kwa kukosa kuiga uzalendo ambao Rais Kikwete ameendelea kuonesha kwa vitendo kwa nyakati mbalimbali.

Tazama! Mwaka jana Tanzania ilishika nafasi ya 10 barani Afrika kwa utawala bora kati ya nchi huru za Afrika zaidi ya 50. Utawala bora huendana na uzalendo wa kuwatendea wananchi mambo kwa haki.

Tazama! Rais Kikwete hakupandisha chati ya uwazi Tanzania katika suala la utawala bora tu. Pia ni katika kipindi hiki tumeona kwa kiasi kikubwa uwazi katika mikataba mbalimbali ikiwamo ya madini.

Lengo ni kuhakikisha maliasili za Tanzania haziendelei kuporwa kwa urahisi. Na huo ni uzalendo. Ni moyo wa kutaka kuona kwamba maliasili za nchi hii zinainufaisha Tanzania na watu wake.

Tazama! Majuzi tu baadhi ya marais katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, waliamua kuitenga Tanzania katika masuala mbalimbali baada ya kuona kwamba Tanzania ya Kikwete imeshikilia msimamo wenye lengo la kulinda ardhi yake na masuala mengine.

Tazama! Hotuba ya Rais Kikwete nchini Afrika Kusini wakati wa mazishi ya Nelson Mandela ilivyojenga heshima ya Tanzania. Hakuna mwaka wa kuorodhesha mambo yote ambayo Rais Kikwete ameyafanya katika kutimiza uzalendo wake. Kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za urais mwaka 2010 pia ni uzalendo.

Kwa jumla basi, nchi inakosa uzalendo si kwa sababu tuna rais ambaye si mzalendo, bali kwa sababu viongozi wengi si wazalendo. Hawaipendi Tanzania na watu wake!

Kuna wabunge ambao mpaka leo wameacha kutekeleza ahadi zao kwa kuwa wamekosa uzalendo. Waliomba ubunge ili wajinufaishe wenyewe.

 

 

1007 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!