Kati ya mambo makuu yanayodhoofisha juhudi za kuhifadhi wanyamapori, hususan kupambana na ujangili, ni kutoonekana kumhusu mwananchi wa kawaida.

Juhudi za uhifadhi na kumpambana na ujangili zinaonekana kutomhusu Mtanzania wa kawaida kwa sababu mbalimbali, na hasa yafuatayo:

Jambo la kwanza ni wanyamapori kuonekana kama ni kwa ajilli ya watalii kutoka nje ya nchi. Hili jambo limeendelea kuwa kama dhana, hivyo kiutendaji na kimiundombinu hata baada ya Watanzania wazawa kuonesha kupenda sana kuangalia wanyama.

Kiashiria kikubwa cha kuonesha hamu kubwa Watanzania waliyo nayo ya kuona wanyama imejionesha kila mwaka wakati wa Saba Saba. Kipindi hicho cha wiki moja, banda au tuseme eneo la wanyama linavuta watu wengi zaidi kuliko banda jingine lolote.

Wingi wa watu katika eneo hilo unaweza kuwa mkubwa kiasi kwamba wakati wote kuna nafasi ya kusimama tu, na hivyo kuwa na msukumano na kutokuwa na nafasi wala muda wa watu kuangalia wanyama wakatosheka.

Kipindi hicho hicho cha Saba Saba huwa inatolewa fursa ya watu kwenda kutalii kwenye Hifadhi ya Mikumi. Nako wingi wa watu wanaojiandikisha kutaka kwenda kutalii kwenye hifadhi hiyo kunaonesha kuwapo Watanzania wengi ambao wangependa kutembelea hifadhi za wanyamapori kama kuna uwezekano huo.

Hamu au kiu ya kuona wanyama inayojidhihirisha wakati wa Saba Saba inaelekea haijafanyiwa kazi stahili. Bado, japo ada za viingilio kwa Watanzania katika hifadhi za wanyamapori vipo chini, miundombinu ndani ya hifadhi hizo na mazingira mazima ya utalii siyo rafiki kwa Mtanzania wa kawaida.

Mbali na kutoonekana juhudi za makusudi za kuelekeza utalii kwa Watanzania wa kawaida, matumizi mengine ya wanyamapori yamebakia yakiwa yanaelekezwa kwa watumiaji wenye uwezo mkubwa kifedha, hususan wawindaji wa kigeni.

Aidha, juhudi zilizoelekezwa kumnufaisha mwananchi kupitia Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs) zinakabiliwa na matatizo mengi ya kiufundi kiasi kwamba nia hiyo ya Serikali ya tangu miaka ya 1970 bado haijaleta manufaa ya kweli kwa Mtanzania wa kawaida.

Pamoja na utalii, kikubwa kingine ambacho Mtanzania wa kawaida angependa kunufaika nacho, ni kupata nyama ya porini kwa kitoweo. Na hili siyo la Watanzania tu, au watu wa nchi maskini, ni jambo la ulimwengu mzima. Kwa mfano, ni jambo la kawaida huko Marekani na Canada kwa raia wa kawaida kukata leseni ya kuwinda mnyamapori na akatumia nyama yake kwa kitoweo.

Kadhalika, ni jambo la kawaida kukuta mtu kaweka nyama ya mnyama ukubwa wa swala, na hata ukubwa wa pofu kwenye jokofu (freezer) kwa matumizi ya mwaka mzima.

 Katika nchi hizo, hata kwenye migahawa midogo (restaurants) kwa mikubwa (hotels), wanatumia nyamapori (venison) kihalali kabisa. Hapa kwetu nyama hiyo inatumika sehemu chache, lakini kiuhalifu; maana nyama inapatikana isivyo halali! Tuliwahi kuwa na shirika la uwindishaji na uvunaji wa wanyamapori – Tanzania Wildlife Corporation (TAWICO), ambalo  sasa hivi halipo; na hakuna mbadala.

 Mwananchi wa kawaida, hasa yule anayeishi karibu na mbuga za wanyama, asipoweza kupata kitoweo na manufaa mengine kutokana na wanyamapori kihalali, inamfanya asione umuhimu wa kuhifadhi wanyama hao. Na zaidi anapata adha, kero na hasara kutokana na uharibifu wa wanyama kwa mazao na mifugo yake. Na hivyo kauli za kwamba utalii na uwindaji una mchango mkubwa katika pato la Taifa zinakuwa hazina maana kwake. Hali hii si salama kwa wanyamapori.

Kuna mambo yanayoweza kufanywa kumwezesha mwananchi kupata kitoweo cha nyamapori kihalali. Kimsingi sera na sheria vinaruhusu, ila kinachokosekana ni kanuni na miongozo sahihi na usimamizi wa dhati. Kukosekana kwa mambo haya ni kati ya changamoto kuu zinazoikabili Idara ya Wanyamapori na mamlaka iliyoundwa karibuni kusimamia uhifadhi na matumizi ya wanyamapori yaani Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori (Tanzania Wildlife Management Authority-TAWA).

 Tatizo kubwa lipo kwenye ucheleweshaji mkubwa wa mchakato wa kutunga vyombo/viwezeshi (instruments) vya kutekeleza sera; ukianzia hatua ya kutunga sheria, halafu kanuni, na kutoka hapo ipatikane miongozo ya utekelezaji. Uzoefu uliopo sasa ni kwamba kutoka hatua moja kwenda nyingine inatumia hadi miaka kumi na kuzidi.  Mathalani, masuala kadhaa kuhusu mwananchi kutumia wanyamapori yaliyokuwa kwenye Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 1974 hayakutungiwa viwezeshi hadi sheria imetungwa upya mwaka 2009; na hata hivyo vingine bado!

 Aidha, pale inapowezekana kuunda miongozo, bado taarifa zinachelewa, ama haziwafikii kabisa wananchi. Ucheleweshaji wa viwezeshi vya kutekeleza sera au sheria, vinafanya tuwe na sera au sheria isiyotekelezeka hadi kufikia kutunga sera na sheria nyingine!

Katika hali hiyo, Serikali inaweza kuridhika kuwa inafanya juhudi bali inashindwa kukamilisha mchakato kutokana na ukosefu wa fedha. Hili halijulikani kwa wananchi; na kama hata lingejulikana isingesaidia. Bado wanyamapori wanabakia kutokuwa na faida inayomgusa mtu wa kawaida kupitia njia halali. Hivyo hata, kaulimbiu za vita dhidi ya ujangili zinazodai wanyamapori ni kwa faida ya wote zinaonekana kuwa danganya toto. 

  Kwa hali hiyo, inapotokea jangili akampa mwananchi pesa au nyama, mwananchi huyo anakuwa hana sababu ya kusaidia Serikali kwa kutoa taarifa kuhusu jangili huyo.

 Mbali na utalii na matumizi ya wanyamapori kuonekana kutomgusa mwananchi wa kawaida, hata kaulimbiu zinazotolewa kuhusu vita dhidi ya ujangili hazijamgusa mwananchi huyo kimuktadha, kimaudhui, na kitaswira.

 Kutumia kaulimbiu ni jambo zuri sana na ambalo linaweza kuongeza ufanisi katika vita dhidi ya ujangili kwa gharama ndogo. Nazipongeza sana asasi na taasisi zilizoanzisha mbinu hii muhimu. Ukweli ni kwamba kutumia kaulimbiu (sloganeering) ni mbinu nzuri sana katika kampeni za makatazo, mapambano, au kuzuia mwenendo; kwa maana zinalenga kugusa fikra au dhamira, na ukishafanikiwa kubadili fikra au dhamira, kinachokuwa kimebakia ni mlengwa kufanya uamuzi sahihi mwenyewe. Ila ukikosea, matokeo yanaweza kuwa mabaya, na hata yakawe kinyume cha kilicholengwa.

Kwa bahati mbaya kaulimbiu zinazorushwa kwenye moja ya vituo vya televisheni hapa nchini zina makosa kadhaa ya kiufundi ambayo yanapunguza ufanisi katika kuwagusa wananchi na kuwashirikisha katika vita dhidi ya ujangili. Mbali na hili, kaulimbinu hizo, kama ambavyo tumekwishaona haziakisi hali halisi ya juhudi na manufaa yanayoonekana kwa wananchi.

Kwa ujumla iko haja ya Serikali kujipanga upya kuhusu ushirikishwaji wa wananchi katika vita dhidi ya ujangili na uhifadhi wa wanyamapori kwa ujumla. Ni muhimu sana kupata ushirikiano wa wananchi wa kawaida, na ushirikiano huo hautapatikana iwapo wananchi wenyewe hawataoni manufaa, na juhudi za kulinda wanyama hao haziwagusi moja kwa moja na kwa mtu mmoja mmoja.

 

Mwandishi wa makala hii ni Mshauri Mwelekezi wa Maliasili, Mazingira na Maendeleo Endelevu. Anapatikana kwa namba ya simu: 0784-463723 na kadhalika barua pepe: tkaiza@gmail.com au t_kaiza@yahoo.com

1217 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!