NA MICHAEL SARUNGI

Ukosefu wa miundombinu rafiki kwenye
viwanja vya michezo nchini ni changamoto
inayokwamisha jitihada za dhati
zinazofanywa na wadau wa michezo
kuhakikisha michezo inakuwa moja ya
sehemu kubwa inayozalisha ajira kwa vijana
wenye vipaji vya michezo nchini Tanzania.
Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la
JAMHURI unaonyesha kuwa ukiondoa
viwanja vya Taifa, Uhuru na Azam
Complex, tayari kuna miaka zaidi ya 30
imepita bila ya uwepo wa jitihada zozote
za ujenzi au kufanya ukarabati kwa viwanja
vilivyopo ili kukidhi viwango vya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
Uchunguzi huo umebaini kuwa ukiondoa
viwanja vya Taifa, Azam Complex na
Uwanja wa Amaan, Zanzibar, viwanja
vilivyobaki havina vyumba vyenye hadhi ya

kuridhisha kwa ajili ya wachezaji, waamuzi,
waokota mipira (ball boys/girls) na
kubadilisha nguo wakati wa mchezo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu
Tanzania Bara (TPLB), Boniface Wambura,
amekiri uwepo wa changamoto hiyo na
kusema viwanja vingi vimejengwa miaka
mingi iliyopita kiasi cha kushindwa
kuendana na mabadiliko yanayotokea
katika soka.
Asilimia 90 ya viwanja 13 vilivyoidhinishwa
na TFF kutumika katika mechi za Ligi Kuu,
FDL, SDL na Kombe la Azam msimu huu,
ukiondoa Uwanja wa Taifa, Azam na Uhuru,
hakuna chenye uwezo wa kukidhi vigezo
vinavyotakiwa na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Duniani (FIFA).
Baadhi ya viwanja vinamilikiwa na Chama
Cha Mapinduzi (CCM) na vilijengwa
mwishoni mwa miaka 1970 na mwanzoni
mwa miaka ya 1980 na vyote havikidhi
masharti ya ulinzi, usalama na burudani
yanayoelekezwa na Shirikisho la Soka
Duniani ( FIFA).
Bodi ya Ligi imekwisha kuzungumza na
(CCM) wanaomiliki zaidi ya asilimia 90 ya
viwanja vinavyotumika katika Ligi ya VPL

(Ligi Kuu), FDL na SDL kuhusu uboreshaji
wa viwanja hivyo na kuahidi kuvifanyia
ukarabati.
Kocha wa timu ya Manispaa
ya Kinondoni (KMC), Etienne Ndayiragije,
amesema suala la uchakavu wa viwanja
hasa mikoani ni tatizo kubwa kwa
maendeleo ya michezo nchini.
Etiene amesema changamoto hiyo inahitaji
kutafutiwa ufumbuzi wa haraka ili kuokoa
vipaji vya vijana vilivyoko hatarini kupotea,
hasa vijijini.
Viwanja vya mikoani havina vyumba kwa
ajili ya wasimamizi wa michezo, sehemu za
wachezaji kupasha misuli (indoor warm-up
areas), vyumba vya habari (press centres)
na vyumba vya madaktari (doping and first
aid rooms). Vilevile havina miundombinu ya
mawasiliano (public address system) na
sehemu za kukaa walemavu.
Klabu nchini zinapaswa kufanya kila
linalowezekana kuhakikisha zinakuwa na
viwanja vyao vya mazoezi na kuchezea ili
kupunguza gharama kubwa wanazozitumia
kukodi mahala pa kufanyia mazoezi na
wakati wa mechi na hili litawezekana kukiwa
na nia ya dhati ya kukuza michezo kwa

viongozi.
Kocha Mkuu wa Dodoma FC ya Dodoma,
Jamhuri Kihwelu, amesema matatizo ya
viwanja yameanza kuwa majanga makubwa
kutokana na vingi kutokuwa rafiki, kutokana
na kujengwa miaka mingi iliyopita huku
miundombinu yake ikiendelea kubaki ile ya
miaka ya 1980.
Ukosefu huu wa miundombinu rafiki
umewawezesha watu wanaoitwa
makomandoo (mabaunsa) wa baadhi ya
klabu kulazimisha kuingia vyumbani
kufanya mambo ya ufundi yanayoashiria
imani za kishirikina kinyume cha Ibara ya 17
ya Kanuni za Usalama za Fifa inayozuia
watu wasiohusika kuingia kwenye vyumba
vya wachezaji kubadilisha nguo.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole,
amesema CCM inafanya vitu kwa awamu,
kazi ya kwanza kwa Serikali ya Awamu ya
Tano ilikuwa ni kuhakiki mali zake,
kinachofuata ni uimara na ubora wa mali
hizo vikiwemo viwanja vya michezo.
Viwanja hivi vinahitaji kufanyiwa ukarabati ili
kuweza kuendana na mabadiliko ya
kiteknolojia ya michezo inayoendelea

kubadilika kila kukicha katika ulimwengu wa
michezo.

Mwisho

By Jamhuri