*Maandalizi ya mabadiliko makubwa yaanza

*Mapendekezo ni halmashauri ziwe

majimbo

*Viti Maalumu navyo kupitiwa na

marekebisho

*Malengo ni kuleta tija na uwakilishi makini

DAR ES SALAAM
NA MWANDISHI WETU

Mabadiliko makubwa ya sheria
yanapendekezwa, yakilenga kupunguza
idadi ya majimbo, wabunge wa
kuchaguliwa, wabunge wa Viti Maalumu na
kuwa na uwakilishi wenye tija.
Habari za uhakika kutoka serikalini

zinasema tayari wataalamu wa sheria
wameshapewa kazi ya kuainisha vipengele
kwenye sheria husika, ikiwamo inayoipa
nguvu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
kugawa majimbo ya uchaguzi.
Mabadiliko yanalenga kupunguza idadi ya
wabunge na gharama kubwa ya kuwalipa
wabunge ambao baadhi yao wanatajwa
kuwa ni ‘mizigo’ kwa walipa kodi.
Shughuli hiyo imeanza kufanywa kwa
umakini na usiri mkubwa, lengo likiwa
kuandaa mapendekezo ambayo baadaye
yatafikishwa kwa wadau mbalimbali. Lakini
baadhi ya wabunge waliozungumza na
JAMHURI wameanza kuonyesha ukinzani,
shaka yao kuu ikiwa ni kupoteza nafasi ya
kuwania ubunge endapo mabadiliko hayo
yatapitishwa.
Miongoni mwa mabadiliko ambayo huenda
yakaanza kuonekana kwenye Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2020 endapo mpango huo
utafanikiwa ni kubadili mfumo wa sasa wa
majimbo yaliyopo, na badala yake
halmashauri zikawa ndiyo ‘majimbo’ mapya.

Kwa hatua hiyo, ina maana baadhi ya
manispaa au halmashauri ambazo zina
majimbo ya uchaguzi zaidi ya mawili,
huenda zikajikuta zina jimbo moja. Lakini
kuna mapendekezo kuwa kila wilaya ndiyo
iwe jimbo. Hata hivyo, mapendekezo hayo
yanaonekana kutoungwa mkono kutokana
na baadhi ya wilaya kuwa kubwa na
nyingine zikiwa na idadi kubwa ya watu.
Kwa sasa idadi ya wabunge inayopaswa
kuunda Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni 393. Mchanganuo wake na
idadi ikiwa kwenye mabano ni kama
ifuatavyo: Wabunge wa Majimbo (264),
Wabunge wa Viti Maalumu (113), Wabunge
wa Kuteuliwa na Rais (10), Wabunge
kutoka Baraza la Wawakilishi (5), na nafasi
moja ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (1).
Habari zilizopatikana kutoka serikalini
zinasema kwenye mabadiliko
yanayokusudiwa kufanywa, endapo
yatapita, idadi ya majimbo itakuwa ni ile
idadi ya halmashauri zilizoko nchini, hasa
kwa upande wa Tanzania Bara. Tanzania
Bara ina halmashauri 186 ambazo ziko

katika wilaya 141 za mikoa yote 26. Kati ya
hizo halmashauri, sita ni za majiji.
Idadi ya wabunge wa kuchaguliwa kwenye
majimbo ambayo sasa ni 264, huenda
ikashuka hadi wabunge 180, ikiwa na
maana majimbo 84 yatakuwa yamefutwa.
Chanzo cha habari kimesema eneo jingine
linalonuiwa kurekebishwa ni la uwakilishi wa
wabunge wa Viti Maalumu ambao kwa sasa
idadi yao ni 113.
Fomula inayokusudiwa kuwemo kwenye
mapendekezo ya mabadiliko ni kuhakikisha
kuwa wanawake wanakuwa asilimia 35 ya
wabunge wote. Kwa kuchukua idadi ya
wabunge 180 pamoja na wengine 16 (wa
Kuteuliwa na Rais, kutoka Baraza la
Wawakilishi na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali), idadi itakuwa wabunge 196. Kwa
hiyo, asilimia 35 ya wabunge 196 ni takriban
wabunge 69.
Endapo mabadiliko hayo yatafanywa, hiyo
ina maana idadi ya wabunge wote wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania (kwa muundo wa sasa wa

halmashauri) watakuwa 202+69= 271.
Kwa hatua hiyo, tofauti ya ‘Bunge hilo
tarajiwa’ na Bunge la sasa itakuwa
wabunge 393-271= 122.
“Kwa maneno mengine ni kusema kuna
uwezekano wa nafasi 122 za wabunge
kupungua, hivyo kuokoa fedha nyingi. Haya
ni mawazo ya baadhi ya watu kuwa tuna
Bunge kubwa lisilolingana na wingi wa
Watanzania. India ambayo idadi yake ya
watu ni bilioni 1.3 lakini wana wabunge 545
kwenye Bunge Kuu (Lok Sabha), sisi idadi
ni watu milioni 55 au zaidi kidogo, lakini
tuna wabunge karibu 400. Hili jambo
linahitaji marekebisho,

” kimesema chanzo

chetu.
Mshahara wa sasa wa mbunge ni wastani
wa Sh milioni 12 kwa mwezi. Kwa mwaka,
mshahara huo ni Sh milioni 144. Kwa
mbunge mmoja katika kipindi cha miaka
mitano, mshahara wake ni Sh milioni 720.
Kiinua mgongo kwa kila mbunge kinasikiwa
kuwa Sh milioni 200.
Hii ina maana endapo utaratibu wa kuengua

nafasi za wabunge 122 utafanikishwa,
fedha zitakazokuwa zimeokolewa –
mishahara na mafao ya kiinua mgongo –
zitakuwa Sh bilioni 122 kwa muda huo wa
miaka mitano. Kiasi hicho cha fedha
kinaweza kujenga kilometa zaidi ya 100 za
barabara ya lami. Umbali huo ni sawa n
kutoka Kimara, Dar es Salaam hadi
Chalinze mkoani Pwani.
Kiwango hicho cha fedha kinaweza
kutumika kununua dawa na vifaa tiba kwa
Tanzania nzima kwa kipindi cha miezi sita.

BUNGE LA TANZANIA

Bunge limekuwepo tangu tupate Uhuru
mwaka 1961 kutoka kwa wakoloni wa
Kiingereza. Hata hivyo, Bunge limekuwapo
kabla ya Uhuru, yaani kuanzia mwaka 1926.
Wabunge nao wameendelea kuwepo kwa
vipindi tofauti na kwa idadi inayobadilika kila
wakati.
Bunge lilipoanza mwaka 1926, wabunge

walikuwa 21. Tulipopata Uhuru mwaka 1961
wabunge walikuwa wameongezeka kufikia
80. Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010 idadi iliongezeka hadi wabunge 357.
Tume ya Uchaguzi ambayo kisheria ina
mamlaka ya kuongeza au kupunguza idadi
ya majimbo, ilifanya hivyo na mwaka 2015
idadi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ikawa 393.
Kati ya wabunge wote hao, wanaotoka
upande wa Tanzania Bara ni 323; na kutoka
Zanzibar ni wabunge 70.
Kabla ya hamahama iliyoshamiri hivi
karibuni, Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kilikuwa na wabunge 280; Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (wabunge 69),
Chama cha Wananchi – CUF (wabunge 41),
ACT-Wazalendo (1), NCCR- MAGEUZI (1)
na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (1).
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi, amezungumza na JAMHURI na
kusema japo suala la kuwapo kwa
mabadiliko ya aina hiyo si la ofisi yake,
wananchi ndio waamuzi wa aina ya mfumo

unaowafaa.
Anasema idadi ya wabunge si tatizo kwa
mtazamo wake, na kwamba
kinachoangaliwa zaidi ni tija inayotokana na
idadi hiyo kwa ajili ya maendeleo ya nchi na
wananchi.
“Tunaweza kuwa na wawakilishi wengi
lakini mantiki ya wingi huo ikawa
haionekani. Tunaweza kuwa na uwakilishi
wa wachache ambao uwakilishi wao
unaweza kuwa au ukawa hauna mantiki.
“Kuangalia suala la gharama ni upande
mmoja wa hili jambo maana unaweza
kutumia gharama kubwa isiyo na tija, lakini
ukatumia gharama ndogo yenye tija,

amesema.
Jaji Mutungi, anasema hana taarifa za
kuwapo mpango huo wa mabadiliko, lakini
kama upo, bila shaka wanaohusika kufanya
tafakari hiyo watakuwa wameona tija ya
mabadiliko hayo.
“Mwisho wa yote kinachotazamiwa ni
kuangalia zaidi masilahi ya nchi – tuangalie
value for money (thamani ya pesa). Pia
lazima kujua what was the spirit behind
(dhamira) – bila shaka wanalenga kwenye

masilahi ya nchi,

” anasema na kuongeza:
“Tunaweza kuwa na wawakilishi wengi,
lakini mantiki haionekani…gharama siyo
tija, jambo la muhimu ni kuangalia tija,
maendeleo yasiyo na effect kwa wananchi
siyo maendeleo.”
Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa
ikifanya mabadiliko mbalimbali, hasa ndani
ya CCM. Mwaka 2016, CCM ilifanya
mabadiliko kadhaa kwenye mfumo wake
ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya
vikao na wajumbe wa ngazi zote.
Mabadiliko hayo yakapitishwa na
Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM iliyoketi
jijini Dar es Salaam chini ya Uenyekiti wa
Rais John Magufuli.
Katika mabadiliko hayo, wajumbe wa
Halmashauri Kuu walipunguzwa kutoka 388
hadi 158. Idadi ya wajumbe wa Kamati Kuu
(CC) ikapunguzwa kutoka 34 hadi 24.
Kuhusu vikao vya kawaida vya NEC,
utaratibu mpya ukatangazwa wa kuwa
vifanyike kila baada ya miezi sita badala ya
minne ya awali, isipokuwa panapokuwa na
dharura.
Pia vikao vya kawaida vya CC vilipunguzwa

ili vifanyike kila baada ya miezi minne
badala ya miezi miwili.
Kwenye ngazi ya mkoa, wajumbe wa
Kamati za Siasa walipunguzwa kwa
kuondoa watatu ambao ni Katibu wa
Uchumi na Fedha na nafasi mbili za
wajumbe wa kuchaguliwa na halmashauri
za mikoa.
Kwa vikao vya kawaida vya Kamati ya
Siasa ya Mkoa, kwa mabadiliko hayo sasa
vinafanyika kila baada ya miezi mitatu
badala ya kila mwezi.
Kwa upande wa wilaya, wajumbe wa
Kamati ya Siasa walipunguzwa kwa
kuwaondoa Katibu wa Uchumi na Fedha,
Katibu wa Kamati ya Madiwani na wajumbe
wawili wa kuchaguliwa na halmashauri. Kwa
pamoja idadi yao ni wanne.
Kuanzia hapo vikao vya kawaida vya
Kamati ya Siasa ya Wilaya vinafanyika kila
baada ya miezi mitatu badala ya kila mwezi,
isipokuwa vinaweza kufanyika vikao
maalumu inapohitajika.
Idadi ya wanachama ya kuwezesha
kuanzisha shina kuanzia hapo ikawa ni
wanachama 50 hadi 300 na ile ya

kuanzisha tawi ni kuanzia 301 hadi 1,000.
Hata hivyo, idadi hiyo inazingatia eneo la
kijiografia na wingi wa wanachama.
Mabadiliko mengine yaliyosisitizwa ni ya
mwanachama kuwa na nafasi moja tu ya
uongozi wa kazi za muda wote kama
ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi
wa CCM, Toleo la 2012, Kifungu cha 22 na
23. Nafasi hizo ni Mwenyekiti wa Tawi, Kijiji
au Mtaa, Kata/Wadi, Jimbo, Wilaya na
Mkoa.
Mabadiliko hayo yanawagusa pia makatibu
wa Halmashauri Kuu wa ngazi zote
zinazohusika, wabunge, wawakilishi na
madiwani.
Vyeo visivyokuwa kwenye Katiba ya CCM
navyo vikapigwa marufuku, na kuanzia
hapo haviruhusiwi katika chama au jumuiya
zake.
Vyeo hivyo ni kama Mwenyekiti wa
Wenyeviti wa CCM, Makamanda (UVCCM),
Washauri (UWT) na Walezi (Wazazi).

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share