EDITHA MAJURA
Dodoma

Imani za kishirikina zinaweza
kumsababishia Shukurani Samweli (34)
ulemavu, vidole vyake vitatu vya mkono wa
kushoto vitaondolewa kutokana na kuoza
kulikosababishwa na kuunguzwa na mvuke
wa maji moto.
Mwanamke huyo mwenye watoto watano,
ameshindwa kuendelea kunyonyesha mtoto
wake mwenye umri wa miezi minne, kwani
hata maziwa yote mawili yameharibika
kufuatia tukio hilo lililompata akiwa kwa
mganga wa kienyeji.
Daktari bingwa wa upasuaji katika Hospitali
ya Rufaa ya Dodoma, Peter Mbele, ambako
Shukurani amelazwa, amesema
walimpokea hospitalini hapo Julai 7, mwaka
huu, akiwa katika hatari ya kupoteza maisha
kutokana na vidonda vilivyosababishwa na
kuungua.

Amesema kumbukumbu za hospitali
zinaonyesha mgonjwa huyo alifikishwa
hospitalini hapo na waumini wa Huduma ya
Uponyaji ya Efatha, wakisema walimkuta
ndani ya nyumba peke yake wakati
wakihubiri Injili maeneo ya Nzuguni A.
Dk. Mbele amesema walijikita katika
kumuokoa badala ya kutafiti kiini cha tukio
hilo.
“Yaani bila maswali yako (JAMHURI)
tusingefahamu aliungua akiwa kwa mganga
wa kienyeji, huyu hapa ni mama yake
mzazi, nilikuwa nahojiana naye ndiye
ananifahamisha eti alikuwa na mapepo
wakampeleka kwa mganga,

” ameeleza Dk.

Mbele.
Kwamba huko akafunikwa kwa mashuka
mbele yake akiwa amewekewa sufuria
lenye maji ya moto, ndipo mvuke
ukamuunguza sehemu za mbele kichwani,
usoni, mikono yote, lakini vidole vya mkono
wa kushoto hasa vitatu vya mwisho
vimekufa na havifai kabisa, maziwa yote na
sehemu za miguu yote.
Akizungumza na JAMHURI hospitalini hapo,
Mama Shukurani, amesema mapepo
yalimfanya akatae kunyonyesha mtoto wake
mchanga kwa takriban siku nne, ndipo

shangazi yake (bila kutaja jina) akaamua
wampeleke kwa mganga wa jadi.
Dk. Mbele akizungumzia tatizo la Shukurani
kutonyonyesha mtoto, amesema
hawajachunguza tatizo hilo, kwakuwa
ndugu zake hawakuwafahamisha lakini
litafanyiwa kazi na wataalamu wa saikolojia.
“Wananchi waache kutanguliza imani na
mila zinazohatarisha maisha yao, mtu
akipata tatizo la afya apelekwe hospitalini ili
achunguzwe na kutibiwa kwa njia salama
badala ya kujisababishia matatizo zaidi,

ameasa Dk. Mbele.
Naye Shukurani akiwa Wodi Namba 7
hospitalini hapo, amemtaja shangazi yake
kwa jina moja la Grace kuwa ndiye
anayemfahamu mganga huyo wa jadi na
ndiye aliyempeleka huko.
“Ndugu zangu walichanga fedha kunipeleka
kwingine lakini yeye akasema twende huko,
mganga mwenyewe ni binti tu wala si
mkubwa, wakanifunikiza kwa mashuka
mbele yangu kukiwa na sufuria lenye maji
ya moto mpaka nikaungua hivi,

” ameeleza

Shukurani.
Anasema alipiga kelele sana lakini watu
waliokuwa hapo (nyumbani kwa mganga)
walimshikilia kwa nguvu akiwa amefunikwa

kwa blanketi mpaka alipoishiwa nguvu na
kuanguka.
Akamsikia shangazi yake (Grace) akisema:
“Sasa tumeua.” Nikamsikia mama akisema:
“Sawa muueni si ndivyo mnavyotaka.” Kisha
akapoteza fahamu.
Baadaye alihadithiwa na ndugu zake
waliokuwa nyumbani kwa mama yake
kwamba watu akiwemo mganga wa kienyeji
walimrejesha wakiwa wamembeba
mikononi utadhani alikuwa amekufa.
Anasema baadhi ya ndugu walipata wazo la
kumpeleka hospitalini, lakini shangazi yake
Grace alikataa akilazimisha atibiwe akiwa
nyumbani.
“Walileta kababa kamoja kalevilevi hivi,
nasikia alikuwa daktari zamani, akawa
anakuja kila asubuhi na vifaa vyake
anatumia maji ya moto kukwangua vidonda,
maumivu niliyokuwa ninayapata ni Mungu
peke yake anajua, yaani nilijua nakufa,

anasema Shukurani.
Lakini siku moja akasikia watu nje
wakisogelea nyumba aliyokuwamo,
wakiimba nyimbo za Mungu, akajivuta
mpaka akaufikia mlango na kuufungua,
akawaona nao wakamuona na kumsogelea.

Baada ya kumuombea na kumhoji, watu
hao wakashauriana kisha wakamchukua na
kumpeleka hospitalini.
Anasema: “Kwa kweli bila wale watumishi
wa Mungu, ningefia ndani.”
Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini
mganga wa jadi aliyehusika na tukio hilo
anafahamika kwa jina la Mama Simon au
Molen, ambaye pia ni mke wa Diwani wa
Kata ya Nzuguni, Aloyce Luhenga.
Jumatatu wiki iliyopita, JAMHURI lilifika
nyumbani kwa diwani kuzungumza na
Molen, ambaye amekiri kuhusika kwenye
tukio hilo lakini amekana kuwa mganga wa
jadi.
“Watoto wetu husumbuliwa na matatizo
yatokanayo na mapepo, kila
tunapowapeleka kwa waganga wa jadi
kutibiwa, tunajifunza mbinu zao na kukariri
miti wanayotumia, kisha tukaanza kutumia
mbinu na miti hiyo kusaidia watu wenye
matatizo kama haya,

” anaeleza Molen.
Anahadhithia kuwa awali alimshuhudia
Shukurani akikataa kumnyonyesha mtoto,
akikataa hataki kuonana wala kuzungumza
na yeyote huku akiwa amejifunika shuka
mpaka usoni.

“Nilimkemea akaanza kumnyonyesha
mtoto,

” anasema Molen na kuongeza kuwa

kwa kushirikiana na shangazi yake,
anayemtaja kwa jina la Kubwibwi,
wakampeleka Shukurani nyumbani kwake
(Molen) ambako walimfanyia anchokiita
tiba.
Ilikuwa jioni, hakumbuki ilikuwa siku gani
lakini anasema ilikuwa mwishoni mwa
mwezi Mei au mwanzoni mwa mwezi Juni,
mwaka huu.
Molen anasema kwa kawaida huwa
wanamtumia binti yao (mtoto wa Diwani
Luhenga) aliyemtaja kwa jina moja la Rose,
kwamba ana “watu kichwani” (mapepo),
hivyo huwa anawaongoza wakati
wakitekeleza shughuli hizo na hata siku hiyo
ndiye alikuwa kinara wa kazi hiyo.
Tulimwita Rose kwa kumpigia simu, akaja
mara tu alivyotoka kazini, alipofika tukaanza
kumhudumia mgonjwa lakini hatimaye
tukashangaa kuona ameungua.
“Tuligundua mapepo yake si kama
tuliyozoea kuwatolea wengine, ambayo
huwavaa tu, huyu mapepo aliyonayo
yametumwa kumuua ndiyo maana
ameungua kimiujiza,

” ameeleza mke huyo

wa diwani.

Iliwalazimu kusaidiana kumbeba na
kumrejesha kwao ambapo ni jirani na
kuwaeleza kilichojiri, wakati huo Rose
alikuwa ameondoka kurejea kwake, maana
ana mtoto mdogo.
Anasema alishauri wampeleke mgonjwa
hospitalini lakini ndugu zake waliamini
angepona hata akiwa nyumbani.
“Tulifahamishwa na Kubwibwi (Grace) kuwa
kesho yake walienda kwa mganga
mwingine, wakapewa dawa ambayo
waliamini ingemponya,

” anasema.

Kwa upande mwingine, wanafamilia hiyo
wengi wakajenga uhasama na wao, hali
iliyosababisha wasitishe kumpelekea
maziwa mtoto aliyeachishwa kunyonya,
baada ya tukio hilo ili kuepusha migogoro
zaidi.
Lakini uhusiano kati yao na shangazi yake
Shukurani, Kubwibwi (Grace) haukuathiriwa
kwa sababu anasema ameolewa na ndugu
yake (bila kutaja jina) anayetunza mifugo na
anaishi hapo nyumbani kwao.

Tiba nyumbani

Molen anasema wiki kadhaa baadaye,

Kubwibwi na mama yake Shukurani
walimfuata baba wa familia (Luhenga)
kuomba awasaidie kugharamia matibabu ya
Shukurani akiwa nyumbani kwao.
“Kuna baba mmoja hapa Nzuguni
anafahamika kwa jina la Faksad, huwa ni
mtaalamu sana wa kutibu vidonda
vilivyotokana na kuungua moto, akitumia
dawa za hospitali, tuliwashauri wamfuate,

ameeleza na kuongeza:
“Yaani akimpaka mgonjwa yale madawa
yake na kumchoma sindano hata mara mbili
tu, anapata nafuu kabisa lakini kwa huyu
ikawa tofauti kutokana na kuwekwa ndani
kwa muda mrefu.”
Anabainisha kuwa fedha za kumlipa
mtaalamu huyo wa afya asiye rasmi,
zilitolewa na mumewe (Luhenga), ambaye
aliwapiga marufuku kujihusisha na shughuli
hizo.

Waumini wa Efatha waeleza

Ester Khalfan, akizungumza na JAMHURI
amethibitisha kuwa Julai 7, mwaka huu,
akiwa na waumini wenzake wa Huduma ya
Uponyaji ya Efatha, jijini Dodoma walikuwa

wakieneza Injili nyumba kwa nyumba na
walimkuta Shukurani ndani ya nyumba
iliyopo Kata ya Nzuguni.
“Tulimfanyia maombi na mapepo yakasema
kwamba yanataka kumuua, kwakweli
alikuwa na hali mbaya kiasi cha kutisha,
vidonda vingi vilikuwa vimeoza, kuingia
ndani ya nyumba aliyokuwamo ilihitaji moyo
sana,

” anasema Ester.

Walimpata mama yake Shukurani ambaye
baada ya kumbana alieleza ukweli kwamba
aliungua kwa mvuke wa maji ya moto,
akiwa kwa mganga wa kienyeji na mpaka
wakati huo alikuwa amebakizwa ndani kwa
takriban wiki tatu.
Baada ya maombezi walishauriana na
kumpeleka hospitali ya rufaa ya mkoa,
ambako baada ya kueleza mazingira
waliyomkuta na hali aliyokuwa nayo kuwa
mbaya kiasi cha kwamba lolote lingeweza
kutokea, alipokewa na kupelekwa wodini.
“Tulielekezwa kupeleka maombi kitengo cha
kutoa idhini kwa wagonjwa
wanaostahili kutibiwa bila kuchangia
gharama za huduma, nikafanya hivyo na
tunashukuru Mungu anaendelea na
matibabu hospitalini,

” ameeleza Ester.
Anasema mpaka wakati huo hawakuwa

wakifahamu mganga aliyesababisha
madhira hayo kwa Shukurani, kwa sababu
walimkuta katika hali ya kutisha na kuona
jambo la msingi ni kuhakikisha anapatiwa
matibabu.

Diwani Luhenga anena

Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo
zinazoelekezwa kwa familia yake, Luhenga,
anasema mtoto wake siyo na hakuwahi
kuwa mganga, hata jamii inayofahamu
familia yake ikihojiwa itaeleza ukweli huo.
Hata hivyo amekiri kuifahamu familia ya
Shukurani, ambayo amekuwa akiisaidia kwa
hali na mali kwa takriban miaka mitatu,
tangu baba yao afariki dunia kwa
kujinyonga ndani ya nyumba yao.
“Lakini kuhusu hayo mambo ya imani zao
siyafahamu na sihusiki kwa namna yoyote
na sipo nyumbani kwa takriban miezi miwili,
sipo nyumbani kufuatia kufiwa na baba
yangu na hivi karibuni nimefiwa na ndugu
yangu, hata tunavyozungumza nipo kijijini
kwetu,

” amesema Diwani Luhenga.

Kamanda Giles Muroto azungumza

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma,
Giles Muroto, ameelekeza suala hilo
lishughulikiwe na Mkuu wa Upelelezi wa
Wilaya ya Dodoma (OC-CID) na kuahidi
kutoa taarifa pindi upelelezi
utakapokamilika.

Mwisho

By Jamhuri