Wiki iliyopita, Jeshi la Polisi lilimtia mbaroni mmoja wa askari wake, baada ya kumkuta akiwa na risasi 200 ambazo haijajulikana alikotaka kuzipeleka.

Askari huyo, Sajenti Michael, ambaye yuko Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), alitiwa mbaroni na askari wenzake wa kikosi cha intelejensia Juni 3, mwaka huu, saa 11 alfajiri akiwa kwenye basi la Mohamed Trans linalofanya safari zake kati ya Musoma na Dar es Salaam.

 

Inaelezwa kwamba Sajenti Michael ni mtunza ghala la silaha katika Jeshi la Polisi. Habari zaidi zinadai kuwa askari huyo amekuwa akituhumiwa mara kwa mara kuchukua silaha na kuwaazimisha watu wanaokwenda kufanya uhalifu maeneo mbalimbali.

 

Sisi tunasema hiyo ni kashfa kubwa kwa Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao. Inawezekana askari huyo amekuwa na mazoea ya kuchukua kinyemela silaha za polisi na kuzielekeza katika matumizi ya vitendo vya uhalifu.

 

Kwa mantiki hiyo, tunasubiri kuona mamlaka husika zinashughulikia suala hilo kwa uzito unaostahili, na kumchukulia askari huyo hatua kali za kinidhamu na kisheria iwapo atathibitika alikuwa anaandaa matumizi mabaya ya risasi hizo 200.

 

Adhabu kali dhidi ya askari huyo itatoa fundisho kwa maofisa wengine wa ulinzi na usalama wanaokiuka maadili ya vyombo hivyo na kuwa chanzo cha uhalifu hapa nchini.

 

Kwa muda mrefu sasa baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi wamekuwa wakihusishwa na vitendo vya wizi na ujambazi katika jamii, lakini mara nyingi wamekuwa hawachukuliwi hatua stahiki.

 

Umefika wakati sasa Jeshi la Polisi na vyombo vya ulinzi na usalama kwa jumla, vijisafishe kwa kuwachukulia hatua kali askari wanaovichafua mbele ya macho ya jamii.

 

Tunasisitiza jambo hili kwa sababu wasaliti wachache ndani ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama wakiachwa waendelee kushirikiana na wahalifu, watavigeuza vyombo hivyo kuwa chaka la wahalifu na kusababisha wananchi kukosa imani na vyombo hivyo.

 

Tungependa kuona Jeshi la Polisi na vyombo vya ulinzi kwa jumla, vinaendelea kulinda hadhi na heshima yake kwa kuhakikisha maofisa wake ni watu waadilifu wanaotekeleza majukumu yao kwa uaminifu mkubwa.

919 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!