Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Agnes Marwa (CCM), ametangaza kuwapeleka bungeni Dodoma, madiwani wa Halmashauri ya Tarime Mjini katika ziara ya mafunzo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche, kutangaza hivi karibuni kuwapeleka madiwani wote wa jimbo lake, bila kujali itikadi zao kwenda Dodoma kwenye ziara ya mafunzo.

Heche alitoa ahadi hiyo hivi karibuni kwenye kikao cha bajeti akisema, “Gharama zote zitakuwa juu yangu, chakula na malazi ili tu ndugu zangu na nyie mwende mkajifunze.”

Lakini kwa upande wa Marwa, mambo yalikuwa tofauti kidogo kwani alisema, licha ya kubeba gharama akaomba Halmashauri itoe usafiri pekee ili kufanikisha malengo hayo.

Kadhalika, alisema: “Kuna haja ya kuwasiliana na Heche ili madiwani wote wa pande mbili (Tarime Mjini na Tarime Vijijini) waende kwa wakati mmoja.

“Mimi bila kujali itikadi za vyama vyetu, madiwani wote wa Halmashauri ya Mji wa Tarime nitawapeleka Dodoma mkapate mafunzo. Mwalimu wa kuwafunza na gharama za malazi na chakula nitalipa mimi.”

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Hamis Nyanswi, aliahidi kulifanyia kazi wazo hilo kwa kuahidi kuwasiliana na Heche ili safari hiyo iweze kuwa ya pamoja, na kuongeza kuwa itakuwa vizuri zaidi kwani itajenga umoja zaidi.

Akichangia hoja hiyo, Diwani wa Kata ya Rebu, Zakayo Wangwe, amepongeza uamuzi huo akisema: “Mbali ya kujifunza tutakuwa pamoja na Mbunge Esther Matiko, ambaye nadhani ni vyema akamuunga mkono Mheshimiwa Marwa.”

“Tumeona jitihada za mbunge wetu wa Viti Maalum, pia na wabunge wengine hawana budi kumuunga mkono ili jambo hili liweza kufanikiwa kwani mpaka sasa Halmashauri yetu haikuwa na mpango wa kutupa mafunzo kwa sababu ya ufinyu wa bajeti,” anasema Zakayo.

Wakati huohuo, Diwani wa Kata ya Nkende, Daniel Komote, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ambako pamoja na mambo mengine amewataka madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tarime kufuata kanuni na taratibu kulingana na viapo vyao.

Baada ya kuchaguliwa, Kamote alisisitiza suala zima la nidhamu katika vikao, jambo ambalo litaendelea kulinda heshima ya vikao vya mabaraza ya madiwani.

“Tumekuwa mashuhuda wa baadhi ya Halmashuri hapa nchini madiwani wakipigana na kurushiana vijembe, huku kamati za maadili zikishindwa kuwawajibisha madiwani hao wanaokiuka maadili ya utumishi, sasa sidhani kama hapa kwetu itatokea hivyo,” anasema Kamote.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini, Athuman Akalama, amezungumza na JAMHURI na kusema wawakilishi wa wananchi – wabunge na madiwani – watakuwa na kazi kubwa katika uongozi wao wa miaka mitano.

Hali hiyo imetokana na Halmashauri hiyo kuandikisha watoto wengi wa darasa la kwanza, mbali na hivyo kuwa na upungufu wa madawati 16,613 pamoja na vyumba 1,188 vya madarasa.

Amesema malengo ya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza ulikuwa ni wanafunzi 16,221 kwa mwaka 2016, lakini waliongezeka na kufikia 18,521 hivyo sasa baadhi ya taifa hilo la kesho wanalazimika kukaa chini.

Amesema vyumba vingi vilivyopo katika shule mbalimbali katika maeneo mengi vimechakaa na Halmashauri imekusudia kusitisha baadhi ya shughuli zake ili kuweka nguvu katika utekelezaji wa utengenezaji madawati na kujenga vyumba vya madarasa.

1735 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!