Wabunge jana walianza kujadili Bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/2013. Kama ilivyotarajiwa, mjadala wa bajeti ya mwaka huu wa fedha ni mkali.

 

Wiki iliyopita wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliitwa katika Kamati yao ambayo Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

 

Kufanyika kwa kikao hicho kulikuwa ni maandaizi ya kuwaweka sawa wabunge wa CCM ambao ndiyo wengi, waweze kuipitisha bajeti hiyo. Hilo ni jambo la kawaida katika mabunge, hasa yenye mseto wa wabunge wanaotokana na vyama vingi vya siasa.

 

 

 

Wapo wabunge ambao wameshaonyesha msimamo wa kutounga mkono bajeti hiyo. Wametoa sababu nyingi, lakini kubwa ni kwamba haiwezekani asilimia 70 ya fedha za bajeti yote zielekezwe kwenye matumizi ya kawaida. Tafsiri ya haraka haraka ni kwamba asilimia hiyo 70 ni kwa ajili ya mishahara, posho za semina, safari za viongozi, kuhudumia magari, takrima na kadhalika.

 

Mtazamo wa wabunge na wananchi wanaopinga bajeti ni kwamba bila kuweka fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo, Tanzania itabaki kuwa na bajeti ya ulaji tu. Pamoja na kwamba jambo hili linaonekana kuwa ni la kisiasa, lakini kuna ukweli ndani yake.

 

Tunasema hivyo kwa sababu Watanzania hawajawahi kuambiwa kuwa Serikali imekosa fedha za safari za viongozi ndani na nje ya nchi, lakini mara zote tumesikia upungufu wa fedha za miradi ya barabara na huduma nyingine za kijamii.

 

Kwa mfano, kwa sasa wananchi wanaougua saratani wanateseka mno katika Hospitali ya Ocean Road , Dar es Salaam kutokana na upungufu na uchakavu wa mashine za mionzi, vifaa tiba, dawa na hata vitanda vya wagonjwa.

 

Wakati hospitali hiyo kubwa na muhimu ikikosa mashine na vifaa, fedha za maonyesho (ambazo hutafunwa kweli kweli), zipo tele.

 

Bajeti ya Serikali haionyeshi ni kwa namna gani tatizo la mabweni, hasa kwa shule za sekondari za wasichana, litapunguzwa. Hakuna mkakati wowote wa kitaifa unaoonyesha ni kwa namna gani Serikali itatumia rasilimali ya mbao tulizonazo nchini kumaliza kabisa tatizo la wanafunzi kukosa madawati.

 

Wakati matatizo makubwa yakiwakabili Watanzania, wananchi wanambiwa kuwa maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru yaligharimu karibu Sh bilioni 60. Fedha nyingi zilitafunwa, na pale zilipotumika, basi ilitengenezwa mifuko ya matairi ya magari (wheel cover). Hivi kweli “wheel cover” inamsaidia Mtanzania?

 

Tunasema wabunge ikosoeni bajeti hii bila hofu kwa sababu ni wajibu wenu. Komaeni hadi hapo Serikali itakapojua kwamba fedha za umma si za kutumbua, bali ni za kumaliza kero zinazowakabili Watanzania walio wengi.

3829 Total Views 18 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!