Leo naomba kuanza makala yangu kwa kukutakia heri ya Krismasi mpendwa msomaji wangu. Lakini pia nichukue fursa hii kuwashukuru nyote mlioniletea salaam za pole kwa wiki yote iliyopita wakati nimelazwa na kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam.
Kipekee niwashukuru Dk. Juma na Dk. Victor Sensa wa Muhimbili kwa vipimo na tiba walizonipatia hadi sasa naandika makala hii.
Sitanii nitakuwa mwizi wa fadhila nisipowashukuru Dk. Muga wa Kairuki Hospital, wauguzi na madktari wote walionitibu hadi nafanyiwa upasuaji na kwa nguvu ya Mungu nikarejea uraiani. Niwashukuru wahariri, umoja wa Twemanye na Nyanga Club ambao kimsingi wamenihudumia nikafarijika.
Najua si vyema kusikia hospitali, ila nalazimika kusifia huduma bora za Hospitali ya Kairuki,  kiwango cha usafi,  uchangamfu na kujituma kwa madaktari na manesi wanaohakikisha wodi ni safi  saa  24, madaktari wanapita wodini   kujulia wagonjwa hali  hadi saa 8 usiku wakiongozwa na Dk.  Muga,  hakika hospitali hii wanatoa zaidi ya kuhudumia wagonjwa na Mungu awabariki sana.
Sitanii, baada ya utangulizi huo niliodhani ni vyema nikausema, naomba sasa kuingia kwenye mada niliyoianza tangu Oktoba, mwaka huu naendelea nayo sasa na nitahakikisha naendelea nayo hadi fursa hii ya Watanzania kulima na kuuza mihogo China waipate nai kunufaikanayo.
Waziri wa Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga wiki iliyopita ametembela China. Katika ziara hii Balozi Mahiga amekutana na wawakilishi wa Kampuni ya Shandong Taianguiyu Food Co., Ltd na wakazungumzia nia ya kampuni hiyo kujenga kiwanda cha kutengeneza vyakula vya aina mbalimbali (noodles) kwa kutumia muhogo kwa ajili ya soko la China.
Kampuni hiyo imeeleza kwamba mwezi Machi, 2018 itatuma timu ya kufanya maandalizi ya uwekezaji nchini Tanzania. Wameeleza kwamba kiwanda kitakapoanza kazi kitahitaji kununua muhogo tani 3,000 kwa siku kwa ajili ya uzalishaji.
Balozi Mahiga ameikaribisha kampuni hiyo kuja Tanzania na pia ameitaka ilete nchini teknolojia ya kuongeza tija (productivity) katika kilimo cha muhogo kuwapa wakulima fursa ya kuzalisha kwa wingi na kuuza muhogo kwa kampuni hiyo.
Waziri Mahiga pia amekutana na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mipango ya China ambaye amemhakikishia Balozi Mahiga kwamba Tanzania itaendea kupewa kipaumbele cha juu katika mpango wa Serikali ya China wa kuhamishia viwanda barani Afrika.
KiongoI huyo wa Tume ya Mipango ameeleza kwamba China itatoa pia kipaumbele kwa Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya One Belt, One Road inayojumuisha ujenzi wa miundombinu ya umeme, reli, na ndege.
Hadi sasa Tanzania imetia saini na kampuni moja tu ya Kichina kwa ajili ya kununua muhogo. Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mathew Mtingumwe amesema hivi karibuni kuwa Tanzania imesaini mkataba na kampuni ya Tanzania Agricultural Export Processing Zone Limited and Epoch Agriculture (TAEPZ). Mkataba huu utaiwezesha Tanzania  kupata kiasi cha Sh trilioni 2.5.
Sitanii, haya yote yanayotokea ni kwa nguvu na msukumo wa Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki. Balizi Kairuki ameandaa haki mikutano kati ya Tanzania na China ila ni bahati mbaya kuwa Waziri mwenye dhamana na Kilimo,  Dk. Charles Tizeba hashauriki.
Nimekwishasikia anawambia  watu mbalimbali eti mimi namtafuta. Bila aibu anasema namtafuta afukuzwe kazi ya uwaziri kwa kumtaka atimizi wajibu wake. Mkataba  wa kuuza muhogo China ulioingiwa kati ya Tanzania  na China unaitaka wizara  ya Kilimo kutoa elimu ya kilimo cha muhogo na kusajili kampuni zitakazozalisha, kununua na kusafirisha muhogo kwenda China.
Sitanii, bahati mbaya Dk. Tizeba  amelala. Anaendelea kusingizia historia. Anasingizia Wazungu kuwa wanatoa ruzuku kwa wakulima wao na hivyo anaona nchi yetu ni kazi ngumu kuendeleza kilimo. Anatumia mfano wa mbaazi alizokosea kuhamasisha wananchi walime bila kuwa na mkataba na India ikakataa  kuzinunua hivyo anaona hata muhogo unaweza kukataliwa.
Binafsi nasema kwanza sina sababu ya kumtafuta Waziri huyu. Mimi si mwanasiasa ila nataka kuona Watanzania wanapata fursa zinazojitokeza. Pili, nasema Waziri huyu akitimiza wajibu wa kutoa elimu ya kilimo cha muhogo na kusajili kampuni za kulima muhogo, wala hataona makala yangu yoyote ikimtaka ahamasishe wananchi badala yake nitaandika makala za pongezi.
Waziri wa kilimo hapaswi kuvaa suti na kuishia kwenye kupiga majungu na umbea. Namhakikisha nika kila taarifa juu ya anavyonisema, lakini namhakikishia pia sitalala nikaacha na kuendelea kuwa mtazamaji huku mambo yakiharibika. Nitachimbua zaidi na zaidi hadi atomize wajibu wake.
Kampuni hii iliyojitokeza ni fursa naomba Watanzania tuichukue na ikifika mwakani, hapana shaka watakuwa wameweka utaratibu wa jinsi ya kulima mihogo, kiwanda hicho kitajengwa wapi na wakulima watapewa elimu juu ya aina ya mbegu za kupanda, muda wa kulima aina ya udongo na viwango vingine. Kwa leo naishia hapa, ila naanza kuona mwanga wa kilimo cha muhogo hata kama Dk. Tizeba atanichukia.
2488 Total Views 15 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!