Suala la mgogoro wa Loliondo limekuwa likitawala katika vyombo vya habari kwa miongo kadhaa sasa. Safari hii kuna kampeni inayoendeshwa kwenye mtandao kwa wiki kadhaa sasa. Chanzo cha mjadala huo ni kwamba Serikali ya Tanzania inataka kuwaondoa wafugaji wa Kimasai ndani ya Loliondo ili kupisha biashara ya uwindaji wa kitalii. Kampeni hiyo inaendeshwa na mtandao wa Avaaz.

Kinachopaswa kujadiliwa hapa ni uhalali wa hao wanaoendesha kampeni hiyo, kujua kama kweli wana jambo la msingi wanalolipigania, au kuna msukumo uliofichika nyumba ya mkakati huu. Ili kulifahamu vema suala hili, yampasa mtu kufikiria kwa makini, kupembua na hatimaye kufikia suluhisho.

 

Historia

Mgogoro huu upo ndani ya Wilaya ya Ngorongoro, ambayo ni moja kati ya wilaya tano zinazounda Mkoa wa Arusha. Kaskazini inapakana na Kenya, Mashariki kuna wilaya za Monduli na Longido, Kusini ipo wilaya ya Karatu na Magharibi inapakana na Mkoa wa Mara.  Wilaya imegawanywa katika maeneo matatu ya kiutawala; Kusini mwa Ngorongoro kuna Mamlaka ya Ngorongoro (Ngorongoro Conservation Area Authority) yenye matumizi mseto ya ardhi; Kaskazini kuna Loliondo inayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti; Tarafa ya Loliondo inajumuisha Pori Tengefu (Loliondo Game Controlled Area –LGCA). Eneo hili limetengwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori, wafugaji wa asili, kilimo na utalii wa kiikoloji.

 

LGCA ni eneo lenye vitega uchumi vingi. Baadhi ya vitega uchumi katika eneo hili ni:- Otterlo Business Corporation Ltd (OBC). Kwa ushindani mkubwa, waliweza kupata kibali cha uwindaji katika LGCA.

 

And Beyond: Hawa wameweka kambi ya kudumu na kiwanja cha ndege. Shughuli zao zinaweza kuonakena katika tovuti yao ya www.kleinscamp.com Thomson Safaris: Hawa wanaendesha shughuli zao za utalii wa asili katika maeneo ya Sukenya, Soitsambu. www.thomsonsafaris.com

 

Dorobo Tours and Safaris: Hawa wanaendesha utalii wa kiikolojia. [http://www.tanzanianorphans.org/dorobo.html]na[http://www.marilynmason.com/dorobo.html]

Sokwe Asilia: Hawa wana kambi za kudumu na za muda. www.asiliaafrica.com/ Nomad Safaris: Kampuni hii inamiliki kambi. www.nomad-tanzania.com/

 

Haiwezi kushangaza kuona kuwa hitimisho la yote haya ni mambo makuu matatu. Mosi, masilahi kutokana na utalii. Pili, vita ya kiuchumi, na tatu, huwezi kushindwa kubaini kuwa washindani wengi katika vita hii wanasukumwa na ukwasi uliopo Loliondo-wanalitaka eneo hilo.

 

Hoja hizi ndizo zinazosababisha uwepo wa nguvu za kisiasa zinazopenyezwa kupitia ushindani wa kibishara. Kila kundi linajitahidi kujiwekea mazingira ya kuhakikisha linafaidi mazo ya utalii katika Loliondo.

 

Utafiti wa kitalii unaonyesha kuwa Loliondo ni eneo pekee lenye vivutio vya aina yake katika mazingira ya asili ambavyo vinavutia watu wengi. Hali hiyo imewafanya washindani wengi watumie mbinu mbalimbali kuhakikisha wanafaidi rasilimali katika eneo hilo.

 

Wanaharakati, kwa kelele zao nyingi za kutunga, na kwa kuzingatia masilahi yao, wameifanya Serikali ya Tanzania iingilie kati suala la Loliondo na kutoa tamko. Hata hivyo, baada ya tamko hilo, wanaojiita wanaharakati wamejipanga na wadau wao wengine kuendeleza mapambano. Kabla ya msimamo wa Serikali hapakuwapo kundi lililojitambulisha kama (Avaaz) ambalo lilishiriki katika kuukuza mgogoro huu.

 

Kana kwamba jambo limefikia machweo, kundi hilo likajitokeza na kujitangaza kama la wanaharakati wa haki za binadamu. Vyovyote iwavyo, matamko yake yanaonyesha wito wake kwa Serikali ni kuhakikisha kuwa Ortello Business Corporation Ltd, inanyang’anywa leseni.

 

Lakini jambo ambalo linazua maswali mengi ni kuhusu wawekezaji wengine walioko Loliondo. Kwanini hawahusishwi katika mpango wa kuondolewa au kwenye tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu? Hapa huhitaji maarifa zaidi kutambua kuwa mlengwa kwa mpango wote huu ni Ortello Business Corporation Ltd. Wengine wameachwa bila kuguswa.

 

Ilitarajiwa kuwa kama suala ni la wafugaji ndani ya Loliondo, wawekezaji wengine nao wangekuwa na la kusemwa. Thomson Safaris katika mradi wao wa Sukenya waliwazuia wafugaji kunywesha mifugo yao katika eneo la Mto Pololet wakati wa ukame mkali kweli kweli. Je, hiyo haikuwa uvunjaji wa haki za binadamu? Kwa kuwa Thomson si mlengwa kwenye mkakati wa kuondolewa Loliondo, hawaguswi.

 

Chukulia himaya za kampuni za Klein’s Camp, Dorobo Tours & Safaris je, ni rafiki wa wafugaji? Jibu ni hapana. Suala hapa si kampuni gani, bali kwanini mkakati huu umeelekezwa kwa kampuni moja pekee miongoni mwa kampuni nyingi zilizoko ndani ya eneo moja la Loliondo?

 

Wanaojiita kuwa watetezi wa haki za binadamu wana ajenda yao mahsusi. Miezi kadhaa iliyopita kulikuwa na kutoelewana kati ya wafugaji wa Kijiji cha Ololosokwan na kampuni ya Kleins camp; Thomson dhidi ya Sukenya. Iliripotiwa kuwa baadhi ya watu walipoteza maisha. Je, si NGONET, PINGOS Forum, Oxfam Ireland na wengine waliolifikisha suala hili katika Universal Periodic Review of Human Right process (UPR-process) na sasa hawasemi lolote? Kitu gani kimewazima?

 

Ushiriki wa mashirika ya kiraia

Ushiriki wa mashirika ya kiraia katika migogoro ya Loliondo si jambo jipya. Kinachoonekana kuwa kipya ni aina ya kempeni. Uongo ulioibuliwa safari hii ni kwamba serikali inataka kuwaondoa wafugaji wa Kimaasai ili kupisha uwindaji wa kitalii. Kampuni inayotajwa kuwapo kwenye mpango wa kupewa eneo hilo ni Ortello Business Corporation Ltd.

 

Uzushi huu unawafanya wafugaji wengine wawaonee huruma wenzao. Ni kampeni yenye malengo nyuma yake. Hao wanaoendesha propaganda hizi hawazungumzi lolote la kuwahusu wawekezaji wengine walioko Loliondo. Hii ni sababu tosha kwamba suala si la Wamasai wafugaji kuondolewa Loliondo, bali ni Ortello Business Corporation Ltd ndiyo inayotakiwa iondoke, vinginevyo wawekezaji wengine waliopo eneo hilo nao wangehusishwa.

 

Pia hapa ikumbukwe kuwa Oxfam ni shirika linaloongozwa na wazungu. Ortello ni kampuni ya waarabu. Wanaochochea vurugu hizi ni kampuni za wazungu. Haihitaji akili kubwa kutambua kwamba hapa mwarabu anapigwa vita ili wazungu walitwae eneo hilo kama walivyofanya katika maeneo mengi nchini.

 

Kinachoenezwa kwamba ni mgogoro kati ya Otterlo Business Corporation Ltd na wafugaji katika LGCA si kinachochochea mgogoro kati ya pande hizo mbili. Inajulikana wazi kwamba Otterlo Business Corporation Ltd inachangia kwa kiwango kikubwa mno maendeleo na ustawi wa wafugaji katika eneo hilo, inachangia maendeleo ya Wilaya ya Ngorongoro, sambamba na kuongeza pato la Taifa. Lakini mtu anaweza kujiuliza, inakuwaje kampuni inayoongoza kutoa mapato makubwa kama hayo, ionekane kuwa haina manufaa kwa Loliondo na Taifa kwa jumla?

 

Uchunguzi umebaini kuwa NGOs zenye mlengo wa kibiashara zinashirikiana na Oxfam Ireland. Shirika hilo la misaada ndilo linalofadhili NGONET, Ujamaa Community Resource Trust (U-CRT) na PINGOS. Asasi hizi ndizo zinazosabambaza sumu ya chuki, na kwa sasa ni juu ya uongo wa kwamba serikali inataka kuwaondoa wafugaji Loliondo. Kinachopaswa kuhojiwa hapa ni kwamba iweje asasi hizi za kibiashara ziitumie Oxfam Ireland ambayo miaka kadhaa iliyopita imefunga miradi yake Loliondo?

 

Kuna ushahidi unaojitosheleza kuwa baadhi ya NGOs hizi zinazoendeleza chokochoko zinafadhiliwa moja kwa moja na Sokwe Asilia na Rubin Hurt Safaris, NGONET kupitia Tanzania Natural Resources Forum (TNRF); ilhali Dorobo Tours and Safaris inafadhili U-CRT na PWC. NGOs hizi zimekuwa zikijihusisha na masuala ya Loliondo kwa miongo kadhaa sasa.

Kadhalika, mtandao wa Avaaz ambao sasa umevalia njuga uongo huu, inataka kujionyesha kuwa imeguswa mno na suala la wafugaji katika Loliondo. Hata hivyo, hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa wamechukua hatua kama hizo kwa maeneo mengine nje ya Loliondo. Je, hii ni kutaka kusema kwamba wafugaji katika maeneo mengine nchini Tanzania hawakabiliwi na changamoto zinazohitaji kutatuliwa? Kwa hakika yapo maeneo mengine nchini, lakini Loliondo ndipo penye kile wanachokitaka.

 

NGOs zimekuwa zikienda nje zaidi ya kile ambacho zimekuwa zikijinasibu nacho, yaani kuwatetea wafugaji. Zimekuwa na masilahi na kampuni za utalii ambazo zimetajwa hapo juu. Oxfam Ireland, PINGO’s Forum, U-CRT, NGONET na Pastoral Women Council (PWC) zimekuwa zikihaha kuwa na uhusiano wa karibu wa kibiashara na kampuni za kitalii na mashirika mengine ya kimataifa nchini Tanzania.

 

Kinachonyamaziwa, na ambacho kwa muda mrefu hakijawekwa wazi ni kwamba NGOs hizi hazijihusishi moja kwa moja na kwa uwazi na masuala ya kibiashara, lakini nyuma yake ni za kibiashara zaidi.

 

Dorobo Tours and Safaris ndiyo wafadhili na waendesha mambo mengi ya U-CRT na PWC.

Kulithibitisha hilo ni kwamba ofisi za U-CRT na PWC zipo ndani ya ardhi inayomilikiwa na Dorobo Tours and Safari. Ushirikiano huu hauhitaji maono ya ziada kuweza kutambua kilichofichika.

 

Unaweza kujiuliza, inawezekanaje kwa NGO inayojihusisha na ‘haki za matumizi ya maliasili’ iwe pamoja na kampuni ambayo kazi yake ni kusaka faida? Hapa ikumbukwe kuwa ni kampuni hizi hizi zinazojihusisha na biashara za utalii ambazo zinalalamikiwa kwamba zinapora rasilimali za nchi na kuiacha jamii inayohusika ikiwa masikini.

 

Kadhalika, David Peterson ni mmoja wa wakurugenzi wa Dorobo Tours and Safaris na U-CRT. Kwa hali kama hii huhitaji kuhangaika kujua ni kwanini U-CRT na PWC wanajihusisha mno kwenye mgogoro wa Loliondo.

 

Katika kuthibitisha haya, tovuti ya Dorobo Tours and Safaris imeweka bayana. Waweza kujioneahayakupitia [http://www.tanzanianorphans.org/dorobo.html]na[http://www.marilynmason.com/dorobo.html]

Kadhalika, Sokwe Asilia imekuwa na maslahi Loliondo, na kwa kuyalinda wamejipenyeza kwenye NGO.  Wamefanya hivyo kupitia asasi ya “Honey guide Foundation” ambayo inaifadhili TNRF.

 

Muhimu hapa ni kwamba David Bell ni mmoja wa wajumbe mahiri kabisa wa Kamati ya Utendaji ya TNRF na pia ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa nyumba za wageni na kambi za Sokwe Asilia. Anapatikana zaidi katika kambi ya Suyan iliyo katika Kijiji cha Ololosokwan, Loliondo.

 

Katika “klabu” yao ya TNRF, Keith Roberts ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji, lakini pia ndiye anayeendesha Friedkin Conservation Fund ambayo inaendesha shughuli zake katika vitalu karibu 14 sehemu mbalimbali nchini Tanzania. Sasa wamekusudia kuongeza kitalu kingine cha 15 endapo watafanikiwa katika mgogoro huu wa Loliondo!

 

Ni wazi kwamba wafugaji katika maeneo mengine nchini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali. Wafugaji waliopo Kilosa, Bunda, Mvomero, Kilombero, Mbarali, Rufiji na sehemu mbalimbali za Tanzania wanahitaji kusaidiwa kuyakabili matatizo wanayopata. Lakini hawa wanaojiita wawekezaji, wakiwamo Oxfam kupitia NGOs mbalimbali wamejikita Loliondo pekee kana kwamba hakuna wafugaji sehemu nyingine za Tanzania.

 

Hitimisho

Kwa maelezo haya ya awali, lakini yanayojitosheleza, Watanzania na walimwengu hawapaswi kufundishwa tena kutambua nani wapo nyuma ya mchezo huu mchafu wa Loliondo.

 

Kinachopaswa kujulikana sasa, na ambacho tunapaswa kwenda mbali zaidi, ni kujua ni nani hasa huyo mkubwa aliye nyuma ya “sinema” hii yote? Bila kukwepesha maneno, ni wazi kuwa Oxfam ndiyo wapo nyuma ya mchezo huu.

 

Ndiyo wafadhili wakuu wa vikundi hivi. Wametafuta uongo wa kila aina kuhalalisha vurugu na migogoro isiyokoma katika Loliondo. Safari hii wamekuja na hoja ya kwamba Serikali ya Tanzania inataka kuwaondoa wafugaji wa Kimasai Loliondo. Huu ni upuuzi unaopaswa kudhibitiwa ili Loliondo na Tanzania iendelee kuwa ya amani.

 

Katika matoleo yajayo tutaeleza mjadala ulivyokuwa – kwa kila aliyezungumza wakati NGOs zilipokutana kwa ufadhili wa Oxfam mjini Arusha na kutoa tamko la kuiunga mkono Avaaz.

 

By Jamhuri