Wafanyabiashara wa masoko ya Mchikichini na Kariakoo wameonya kuwa kuna uwezekano mkubwa wa bidhaa zinazouzwa kwa wingi katika maeneo hayo kupanda bei maradufu kutokana na uhaba wa bidhaa hizo ulioanza kujitokeza.

Kwa kiasi kikubwa maeneo hayo ni maarufu kwa biashara ya nguo na viatu vya watoto na watu wazima, vifaa vya elektroniki, vifaa vya nyumbani na vifaa vya ujenzi.

Pamoja na kuhudumia wateja wa ndani, pia eneo hilo lina maduka ya jumla ambayo uhudumia wateja kutoka nchi jirani za Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zimbabwe, Rwanda, Burundi na Uganda.

Wakizungumza na JAMHURI hivi karibuni, wafanyabiashara hao wamesema bidhaa zimeanza kuhadimika kutokana na kutoingia kwa mizigo mipya kutoka China, nchi ambayo kwa kiasi kikubwa ndiko zinakotoka bidhaa hizo.

Wamesema kuibuka kwa ugonjwa wa virusi vya corona nchini humo kumesababisha kuzuiwa kwa bidhaa zote zinazosafirishwa kutoka China kwenda nchi nyingine kama sehemu ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo ambao umekwisha kuua maelfu ya watu duniani kote hadi hivi sasa.

Baadhi ya wafanyabiashara wamekwishaanza kukata tamaa kutokana na taarifa kuwa iwapo virusi hivyo havitadhibitiwa haraka, kuna uwezekano wa biashara kutoka China kusimama kabisa.

Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo, Mkatia Issa, amekiri kutikiswa kwa wafanyabiashara wake wanaochukua bidhaa kutoka China.

“Hali sasa hivi si mbaya sana, lakini bei ya bidhaa imeshaanza kupanda kutokana na uhaba wake. Hali itakuwa mbaya sana siku zijazo, hasa ukizingatia kuwa tunaelekea kwenye sikukuu za Pasaka na Idd, na hakuna matarajio ya kupata mzigo mwingi katika siku za karibuni,” anasema na kuongeza:

“Watakaoathirika si wafanyabiashara wa ndani tu, kwani kuna wafanyabiashara wengi kutoka nchi jirani ambao hutumia Kariakoo kama kituo chao cha kununua bidhaa na kuzipeleka kwenye nchi zao, nao wataathirika pia.”

Issa anasema hivi sasa wanasubiri meli mbili ambazo zimo njiani kutoka China ambazo ziliondoka nchini humo kabla marufuku haijawekwa, lakini baada ya hapo hali itaanza kubadilika.

“Kwa kawaida tunapokea meli kama kumi hivi katika misimu hii ya sikukuu, lakini sasa tunasubiri meli mbili tu,” anasema.

Sudi Saidi, mfanyabiashara wa jumla wa viatu, anasema ipo haja kwa serikali kuwasaidia kupata vyanzo vingine vya bidhaa hizo kwa bei ya chini kama ilivyo China ili kuhakikisha kuwa biashara zao hazifi.

“Lakini pamoja na hayo, lazima tukiri kuwa hata hali ya biashara si nzuri hivi sasa, hakuna wateja wengi kama zamani,” anasema Saidi. 

Akitoa mfano, anasema miaka ya nyuma alikuwa akiuza mabalo zaidi ya kumi ya viatu kwa kipindi cha wiki moja tu, lakini hivi sasa huchukua hadi wiki tatu kuuza kiasi hicho cha mzigo.

Katibu wa wafanyabiashara katika Soko la Mchikichini, John Joseph, anasema kutokana na China kuzuia bidhaa kutoka ndani ya nchi hiyo, biashara nyingi zimeathirika, kwani watu wengi walikuwa wanategemea bidhaa kutoka China.

“Lakini pamoja na masuala ya biashara, serikali iwe makini kudhibiti ugonjwa huu usiingie nchini kwani kuna wafanyabiashara wanarejea kila siku kutoka China baada ya kukosa bidhaa. 

Wapo wafanyabiashara wa hapa nchini lakini kuna wengine kutoka nchi jirani ambao hupita hapa kwenda China,” anasema.

Mwenyekiti wa wauza mitumba, Ajari Mohamed, naye amekiri biashara kuathiriwa na virusi vya corona ingawa hali bado haijawa mbaya sana, kwa sababu mitumba inatoka katika nchi nyingi zaidi ya China.

“Ingawa tunaagiza bidhaa kutoka nchi mbalimbali lakini pia tunaitegemea China kwa kiasi kikubwa, hasa kwa nguo mpya,” anasema na kubainisha kuwa ili kukabiliana na hali hiyo tayari wafanyabiashara wa mitumba wameanza kuagiza bidhaa hizo kutoka nchi nyingine, hasa nchi za Ulaya.

Jitihada za kuwapata Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa na naibu wake, Stella Manyanya, kulizungumzia suala hilo ziligonga mwamba. Kwa siku nzima Jumamosi kila simu ya Bashungwa ilipopigwa ilionekana kuwa inaongea na Jumapili haikupatikana kabisa. 

Simu mbili za Manyanya zilipopigwa Jumamosi zilipokewa na mtu aliyesema kuwa naibu waziri huyo alikuwa amezisahau dukani karibu na nyumbani kwake. Simu ya Katibu Mkuu, Prof. Riziki Shemdoe, haikupokewa.

By Jamhuri